Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, kwanza nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kukubali jambo hili na kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja yangu hii ya Bodi ya Mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni juzi tu tulimwona Waziri wa Elimu katika vyombo vya habari akisema kwamba aliunda tume maalum ya kuchunguza Bodi ya Mikopo, lakini Waziri akawa analalamika kwamba ile tume aliyoiunda imeshindwa kupata ushirikiano. Kwa hiyo, maana yake Bodi na Serikali haviko pamoja ndiyo maana Waziri ameunda tume na tume haijaweza kutoa ushirikiano kwa Serikali. Kwa hiyo jambo lile likanishtua kidogo.

Mheshimiwa Spika, lakini weekend yote hii baada ya majina kutoka na wanafunzi kuanza kudahiliwa na wengine kuripoti mimi nimepokea simu nyingi sana kutoka jimboni kwangu, wazazi wengi wanafunzi wao wamekosa mikopo, wote wanakimbilia kwa Mbunge. Sasa solution hata mimi nikawa naona nikirudi kwa Waziri yule ambaye nilimwona kwenye vyombo vya habari analalamikia tume, sidhani kama ningeweza kupata jibu la haraka, ndiyo maana nikasema Bunge ndicho chombo cha wananchi hivyo nilete hoja katika Bunge ili Bunge liweze kujadili hatimaye tupate majibu na tutoke na maazimio ya Bunge ili tuweze kuielekeza Serikali nini ifanye kuweza kuwakwamua watoto hawa ambao wamekwama katika maeneo haya. (Makofi!)

Mheshimiwa Spika, niki-refer ukurasa wa 49 wa hotuba ya Waziri wa Elimu aliyoitoa humu Bungeni, tumeona alikuwa anasema kwamba katika mwaka huu uliopita wa fedha, tumetoa mikopo ya takribani Shilingi bilioni 569. Tukaona ni jambo zuri, na katika mwaka huu wa fedha ambao tunaendelea nao wa 2022/2023 tulikuwa tunategemea kwamba fedha ilikuwa inaongezeka. Alikuja pia na shilingi bilioni 200 kutoka NMB ambazo zingeenda kukopesha wafanyakazi na watu wengine ambao wanao uwezo wa kukopesheka kutokea huko, mpaka na watu wa diploma waweze kupata huo mkopo.

Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza, niko na fomu hapa ya mtoto wa mkulima ambaye ameandika, mama ni farmer na baba ni farmer. Mtoto huyu ni miongoni mwa watoto reference katika Taifa hili ambaye amepata division 1.7 O’level, Msalato Sekondari (shule ya Serikali). Akiwa na “A” saba mtoto wa kike, form five na form six akabaki Msalato palepale. Mtoto huyu wa kike akapata division 1.7 tena. Mtoto huyu amechaguliwa kwenda kusomea udaktari Chuo cha KCMC. Ajabu ni kwamba alichokipata, anapewa ile fedha ya kujikimu lakini hajapewa ada.

Mheshimiwa Spika, ada ni shilingi 5,600,000. Mtoto wa mkulima ambae amesoma Msalato miaka yote sita, anapata wapi ada hii ya kuweza kusomea udaktari? Maana yake tunachokiona ni nini? Hata watoto wadogo walioko pale waliomwona kama role model wao aliyepata division one ya pointi saba watakata tamaa ya kusoma maana ndoto zao zinakatizwa kwa sababu hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kigezo ambacho nashindwa kukielewa kipindi wanachambua. Katika masharti yaliyowekwa humu kwenye Loan Board hapa, kipo kigezo ambacho, baada ya viongozi wa Serikali ya kijiji kusaini fomu ya mtu huyu, tumeambiwa kwamba endapo itakuwa wametaja taarifa za uongo, watatozwa faini ya shilingi milioni moja na nusu au kifungo cha miezi sita jela au vyote kwa pamoja. Sasa tunajiuliza, kama watu wanasaini fomu na zinapita kwa viongozi na sheria mmeweka, sijasikia kama kuna kiongozi wa kijiji hata mmoja ambaye amepelekwa mahakamani kwamba alijaza fomu za uongo na akashtakiwa, that means taarifa za watoto hawa ni sahihi lakini watoto hawa wananyimwa mikopo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kutoa hoja sasa kwamba Bunge lako lipokee hoja yangu na lijadili hili jambo ili tuone jinsi ya kuwakwamua hawa watoto ambao wamekwama na wengine bado wako majumbani na hata walioripoti vyuoni bado hawajapewa fedha hiyo pia bado wanahangaika mtaani.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika naafiki.