Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Azimio hili muhimu, Azimio la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Kuongezewa Mamlaka Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hili ni jambo muhimu sana na sisi kama Taifa, naona kama tulichelewa lakini kwa kuwa limekuja leo, tunashukuru kwa sababu limefika na kama Bunge tutimize wajibu wetu, lakini kuna mambo kadhaa ambayo nataka niyashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kukua kwa Jumuiya hii ya Afrika Mashariki kumepelekea kuridhia Itifaki kadhaa, Itifaki ambazo zimeshazungumzwa, Itifaki wa Umoja wa Forodha, Itifaki ya Soko la Pamoja lakini Itifaki ya Umoja wa Sarafu pamoja na Itifaki nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilitazama jambo hili leo tunapozungumzia kuongeza mamlaka, lazima jambo hili liendane sambamba na kupunguza baadhi ya mamlaka zilizopo kwenye mahakama zetu, pamoja na kwamba tunasema haitaathiri, kwa sababu tunapoongeza mamlaka kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki tunaenda kuiongezea nguvu. Ili uiongezee nguvu kuna baadhi ya vitu lazima vitoke huku viende kule kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo hayo kwa sababu na sisi lazima tuone tunanufaika vipi, unapozungumzia mahakama ni chombo ambacho kinakwenda sasa ku-balance mizani kwenye hizi Nchi Wanachama. Lazima tujue tumejiandaaje kama Taifa kuandaa Wanasheria wetu lakini na ushiriki wa Majaji kwenye mahakama hiyo ili kama Taifa tuweze kunufaika kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sisi tumeridhia na tumeshachunguza kwa sababu inawezekana huu muda ambao tumechelewa kuleta hapa au kuridhia walikuwa wanachunguza kwamba je, kuna athari gani kwenye taifa na mambo gani, lakini lazima tujue tunapoamua kuridhia leo lazima pia tuheshimu maamuzi yanayotolewa na Mahakama hii ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo kadhaa ambayo yalishatolewa maamuzi, mfano pekee, ni ile sheria ya vyama vya siasa, lakini mpaka leo kama Taifa hatujatekeleza yale maamuzi yaliyotolewa na Mahakama hii. Ni vizuri kama tumeamua kuingia na hapa kwenye ushauri wangu kwa sababu wanachama waliopo kwenye jumuiya hii, kama tumeamua kuongeza mamlaka basi sisi nchi wanachama tuheshimu mamlaka ya hiyo mahakama na maamuzi ambayo yanatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongezewa mamlaka kwa mahakama hii ya Afrika Mashariki ni lazima iendane na kuiwezesha kwenye teknolojia, iendane na hali ya sasa. Lazima kuwepo kwa nguvu kazi ya kutosha ikiwepo nguvu kazi ya kutosha hata maamuzi yatafanyika kwa haraka na haki itatolewa kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunazungumzia kuridhia kwenye Itifaki hii, tumewaandaaje wafanyabiashara wetu kwenye hizi Itifaki kadhaa ambazo tumeshapitia na pia tumejiandaaje kuondoa huu utitiri wa kodi na tozo ambazo zinaweza zikawa vikwazo kwenye hii jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado elimu inahitajika sana hata kwa wananchi wetu, kuona umuhimu wa hii mahakama, lakini ni vizuri kama tumepitisha leo tukajikita zaidi kuwapa elimu wananchi wetu wakajua faida ya mahakama hii ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana kwa sababu tunapozungumzia jumuiya hii tunazungumzia pia soko la ajira, tumewaandaaje vijana wetu waweze kunufaika na hii fursa kwenye suala la ajira kwenye umoja wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kitu unapokuwa unataka fursa lazima uangalie kwamba kuna ushindani. Tumejiandaaje na huo ushindani, kama hatujajiandaa watanufaika wengine tutabaki kuwa wanachama tu, kwa sababu lazima tupime ni wapi ambapo kama Taifa tumejipima, ni kweli tunaendana na huo mfumo? Mifumo yetu ni rafiki ya kwenda ku-compete kwenye huo Umoja wa Afrika Mashariki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe na umakini wa kutosha tuweze kutumia kama fursa katika nafasi hiyo ambayo tutakuwa tumeipata. Pamoja na kwamba tumeingia muda mrefu lakini kuna mambo ambayo kama Taifa tuone, ni kweli sisi hapa tulipofikia haya manufaa tunayoyapata ndiyo yanatosha kwa wananchi wa Taifa hili kama wanachama wa Umoja wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo lazima tuyatazame, leo unapozungumzia biashara tuna changamoto ya wakulima wetu kwenye biashara, hata bima tu kwa mkulima kwa ajili ya biashara yake bado ni changamoto kwenye Taifa letu. Je, tunakwenda kunufaikaje sisi na hiyo Itifaki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa leo nilikuwa nataka kujikita kwenye kushauri na nasema kwa umoja wake Kamati ya Katiba imefanya kazi kubwa sana ya uchambuzi, wamechambua kwa kina, lakini ni vizuri umakini ukaongezeka, zile ambazo tunaziona ni fursa tuzitumie na kuwasaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)