Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kwanza kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia mjadala huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru na kuipongeza sana Kamati yetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mheshimiwa Vita Kawawa kwanza kwa jinsi ambavyo wanatupa ushirikiano na hata katika hoja iliyoko mezani. Mchango wao ulitusaidia sana, na leo hii hali kadhalika maoni na mapendekezo yao; nimuhakikishie Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kamati kwa ujumla kwamba yote ambayo wameyawasilisha tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikianza kuwashukuru waliochangia wote nianze na wewe Mwenyekiti kwa kuwasilisha mchango mzuri kwa niaba ya Kamati na wachangiaji wengine ambao walipata fursa ya kuchangia, ambao ni Mheshimiwa Chumi, Mheshimiwa Seleman Zedi, Mheshimiwa Ighondo, Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mheshimiwa Zahor, Mheshimiwa Ally Kassinge, Mheshimiwa Nollo pamoja na Mheshimiwa Tadayo. Pia nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Jumanne Sagini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla maoni ya wachangiaji kwa asilimia kubwa sana au kwa asilimia zote niseme yanaonekana kuunga mkono Azimio hili ama Itifaki hii. Tunashukuru sana kwa kuunga mkono Azimio hili, lakini tunashukuru kwa kuweza kusaidia kuongezea kuelezea faida nyingi zaidi, ambazo kama taifa tutapata kwa kuridhia Itifaki hii, tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa kwa maelezo hayo na kwa maoni ya wachangiaji sitakuwa na mengi ya kuzungumza hapa leo kwa sababu mengi yaliyozungumzwa yanaenda sambamba na malengo na matarajio ya uwasilishwaji wa hoja yetu. Hata hivyo kuna mambo machache ambayo niliomba nitumie nafasi hii kuweza kuyapatia ufafanuzi kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ambayo ningeomba nichangie ni hoja ambayo iliwasilishwa na Mheshimiwa Sophia Mwakagenda. Mheshimiwa Sophia Mwakagenda alihoji juu ya kwa nini tumechukua muda mwingi sana tangu Itifaki hii ilivyopitishwa na kusainiwa na kuweza kuwasilishwa leo hapa Bungeni kwa ajili ya kuridhiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, na nitajibu suala hili nikichanganya na hoja ya Mheshimiwa Nollo ambaye alitoa juu ya umuhimu wa kutofanya mambo kwa kufuata matakwa ya mataifa mengine ya nje, ambayo wakati mwingine hutumia changamoto ya ugaidi kwa maslahi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba taifa letu kama nchi tunafanya vitu kwa umakini mkubwa. Na kama ambavyo mnafahamu ilibidi tuangalie mambo mengi na tutafatakari kama taifa kabla ya kuwasilisha hapa Bungeni juu ya wakati gani ni mwafaka kuiwasilisha hatua hii. Na hiyo inadhihirisha juu ya uhuru wa taifa letu wa kuamua mambo yake yenyewe, kwamba hatufanyi mambo kwa kushinikiza. Pale ambapo tumeona sasa ni wakati ni muafaka kulingana na mazingira ya sasa hivi; na bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kwamba ni kweli taifa letu halijakumbana na changamoto za kigaidi, lakini tumeshuhudia viashiria mbalimbali vya kigaidi vikitokeza katika nchi hii katika nyakati kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata majirani zetu na wenyewe wamekumbana na matatizo ya kigaidi, na mfano mzuri ni hivi karibuni nilieleza hapa katika hotuba kwamba tulifanikiwa kuweza kuwapeleka watuhumiwa wawili wa kigaidi kutokana na tukio lililotokea Uganda. Hii inaashiria kwamba umuhimu wa Itifaki hii iko moja katika madhumuni yake makubwa ni kusaidia kubadilishana taarifa, kubadilishana uzoefu, kubadilishana mafunzo na ujuzi mbalimbali. Na pengine Itifaki hii itasaidia sana sasa kuweza kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sophia pia alizungumzia juu ya dhana nzima ya matumizi mabaya ya hoja hii ya ugaidi. Nataka nifafanue kwamba Tanzania tuna bahati kwa sababu tumekuwa ni nchi ambayo imejengeka katika misingi ya amani. Na kama ambavyo walizungumza, nadhani Mheshimiwa Zahor, kwamba vitu hivi havijaja kibahati mbaya. Kuna mambo mengi ambayo yamesaidia nchi yetu kuwa katika hali hii ya amani ambayo imekuwa ni mfano wa kuigwa Barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini moja ya sababu ambayo imechangia kufanya taifa hili liendelee kuwa na amani, ni kwamba misingi ya nchi yetu tangu imeanzishwa tumekuwa makini kudhibiti visingizio ambavyo vinatumika na baadhi ya nchi au baadhi watu katika nchi mbalimbali kufanya vitendo vya kigaidi. Nchi yetu visingizio hivyo tumevidhibiti kwa kiwango kikubwa na jambo hilo limefanyika kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vyetu vya usalama, lakini kubwa zaidi na waasisi wa taifa hili ambao walipata fursa ya kuongoza nchi hii katika miaka ya nyuma, vilevile pamoja na nchi hii kuweza kuwa katika mikono salama ya chama kilichopo madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, misingi hiyo imesaidia sana kuvifanya visingizio vya kigaidi ambavyo vimekuwa vikitumika, aidha visingizio vinavyotokana na sababu za kikanda, visingizio vya kikabila, iwe visingizio vya kidini visipatikane katika nchi hii kutoka na uongozi dhabiti na imara ambao nimeeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka nilichangie, ni kwamba labda pengine Itifaki hii inaweza ikachangia matumizi mabaya yenye uhalifu wa kigaidi. Kwamba mtu anaweza tu akasingiziwa kwa sababu tu ya kutoa maoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli uhuru wa kutoa maoni upo kwenye Katiba, lakini kwenye Katiba hiyo hiyo uhuru huu umewekewa; maana katiba inasema bila kuathiri sheria za nchi; kwa hiyo uhuru huu umewekewa mipaka ya kikatiba. Uhuru wako unaishia pale uhuru wa mwingine unapoanzia. Na sheria za kudhibiti hizi ambazo zimeelezwa zipo sheria nyingi. Kwa mfano kuna Sheria ya Mtandao ambayo inatumika kuweza kudhibiti matumizi mabaya ya uhuru. kwa mfano leo hii huwezi ukasema una uhuru ukaanza kusambaza picha za ngono hovyo hovyo kwenye mitandao ya kijamii au ukazusha tu taarifa za uongo za kudhalilisha watu wengine, au ukazusha taarifa za kuchochea ubaguzi aidha wa kikabila, wa rangi au mwingineo na tukakaa tuseme tu kwamba huo ni uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimtoe wasiwasi kwamba tunazo sheria ambazo zinadhibiti mipaka ya uhuru. Hatuwezi kutumia sheria ya ugaidi ama Itifaki hii kudhibiti uhuru wa watu, lakini uhuru wa watu utadhibitiwa pale ambapo utavuka mipaka ya kisheria kulingana na sheria zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho ambalo nataka nilizungumze ni kuhusu umuhimu wa sheria hii kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi wameeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi waliochangia, wamezungumzia juu ya umuhimu wa sheria hii katika kuimarisha usalama katika nchi hii. Na usalama wa nchi hii ni jambo ambalo ni muhimu sana katika kusaidia kufanikisha hata kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Kuna hoja zimezungumzwa kuhusu jinsi ambavyo taifa letu limepiga hatua kubwa sana hasa katika kipindi cha karibuni katika sekta ya utalii. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Utalii amezungumzia vizuri hilo. Hatuwezi kuendelea kutumia fursa hiyo ya uchumi wa utalii kama amani katika nchi hii haijaendelea kutulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na matatizo ya kigaidi yamekuwa na athari kubwa sana katika kuteteresha amani ambayo inaathiri si tu utalii peke yake, yanaathiri utalii, uwekezaji, utabiri wa kimasoko (market uncertainty), lakini hata uingiaji wa fedha za kigeni nchini (Foreign Direct Investment). unaathiri vilevile uwezo wa uchumi wa mtu mmoja mmoja, unaongeza umaskini. Kwa hiyo athari za kiuchumi zinazosababishwa na ukosefu wa usalama katika nchi ni nyingi, na ugaidi ni moja ya chanzo kibaya sana cha kuteteresha usalama wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mataifa mengi yakipata athari kubwa za muda mrefu, athari za kupoteza maisha, athari za kusababisha walemavu katika nchi husika, athari za matatizo ya kisaikolojia ambayo yanatokana na matatizo ya kigaidi. Pia athari za uharibifu wa mazingira na uharibifu wa miundombinu. Miji mingi imeharibika ambayo ilikuwa imejengeka vizuri tu kwa miaka mingi sana na kwa nguvu kubwa lakini leo hii imeharibika. Pia machafuko ya ndani na matatizo mengi sana ambayo yanasababishwa na matatizo ya kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nichukue fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kuunga mkono Azimio hili. Ni dhahiri kabisa Itifaki hii itakapopitishwa itasaidia sana kama taifa kuweza kujenga mahusiano na ushirikiano katika nchi yetu na mataifa mengine katika kukabiliana na athari za kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache naomba sasa nimalizie kwa kutoa hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.