Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa mwisho kwa upande wa Wabunge. Awali ya yote ninawashukuru Wakuu wa nchi zetu za Afrika kwa sababu iliwapendeza miaka hiyo ya nyuma ya 2004 kuandaa Itifaki hii. Ni jambo la kimapinduzi na la kipekee kwa sababu tumezoea kuwa na Itifaki za Umoja wa Mataifa au Taasisi zake kubwa za Kimataifa, lakini tunapofikia sasa mahali pa kuanza kuwa na Itifaki ambazo zinatokana na Afrika kwa ajili ya Afrika ni jambo linalofurahisha sana kwamba AU sasa inarejea katika kazi yake ile ya msingi. Mwanzoni ilikuwa ni mambo ya ukombozi lakini baadaye ikaendelea kuwa sasa masuala ya uchumi, usalama na ustawi wa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba huwezi ukaitaja AU au OAU bila kuitaja Tanzania. Mwalimu Nyerere pamoja na wenzake waliokuwepo enzi hizo ndio waliokuwa waanzilishi na mbegu ile ndiyo inayomea mpaka sasa hivi. Kwa hiyo, kipekee kabisa kwa kweli leo tunaporidhia Itifaki hii tunapaswa kabisa kutambua, kupongeza na kushukuru juhudi za Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo ameendelea kufanya juhudi za kutufanya tubaki pale turudi kwenye nafasi yetu, katika Itifaki ya Afrika na ya Kimataifa na katika mambo ya Kidiplomasia ya Afrika na ya Kimataifa hasa katika maeneo yanayohusu maslahi ya Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine hiyo ni sehemu ya jibu kwamba kwa nini tunaridhia Itifaki hiyo leo, Itifaki ya mwaka 2004, hizi ni zama sasa za kutokuchelewesha mambo ya Kimataifa ni zama sasa ya kuyatekeleza, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais na kwa kuridhia Itifaki hii leo tunaunga mkono hizo juhudi zake ambazo dunia nzima imeshaziona tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri nikataja kidogo juu ya hii tarehe kwa nini tunaridhia leo tusiwe wanyonge sana kwamba ni kuanzia 2004. Ukienda Ibara ya 10 ya Itifaki hii utaona imeelekeza kwamba mpaka nchi 15 zitakapokuwa zimesaini na ku-deposit (zimeridhia) ndipo ile Itifaki itaanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi hizi 15 zilifikiwa mwaka 2014 miaka 10 baada ya ile Itifaki. Kwa hiyo, leo hii tusiseme kwamba tunafanya kazi ya mwaka 2004 hapana, hata tungeifanya hivyo isingekuwa hatujafanya kazi yoyote bila nchi 15 ambazo zilifikiwa mwaka 2014.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugaidi kama ambavyo wengi wamesema ni uhalifu wa Kimataifa na unaovuka mipaka, ni tofauti na uhalifu mwingine. Tunayo Sheria ile ya Kuzuia Ugaidi Sura ya 19 ambayo kwa kweli inatuwezesha zaidi kupambana na ugaidi wa ndani (Domestic Terrorism) lakini haitoshi tunapokwenda kwenye ugaidi wa Kimataifa, kwa sababu, ugaidi wa Kimataifa sasa hivi unaweza ukapigwa hapa na mtu aliyepo kilometa 10,000 kutoka hapo ulipo au mtu anaweza akapiga hapa lakini baada ya nusu saa ameshatoka nje ya nchi hii. Kwa hiyo, ni muhimu kuridhia Itifaki kama hizi ambazo zinapanua wigo wa kuweza kushughulika na jambo kama hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo Sheria nyingine inaitwa Mutual Assistants in Criminal Matters Act Cap. 254 ambayo inasaidia katika kuchukua ushahidi katika kupekua na kukamata vitu ambavyo vimepatikana katika upelelezi na katika kukamata watu wanaokimbia ambayo inatumika kwa nchi mbalimbali, lakini bado hata yenyewe hiyo inashughulika na makosa yote siyo kama hii ambayo ni maalum kwa ajili ya ugaidi. Kwa hiyo, pamoja na Sheria hiyo lakini bado tumeendelea kupata changamoto kwenye suala la ugaidi kutokana na upekee wake. Kwa hiyo, kutokana na upekee wake ni lazima tuingie kwenye Itifaki kama hii ambayo itatusaidia kupambana na hili jambo kwa kushirikiana na wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugaidi hata usipotokea hapa Tanzania ukatokea nchi nyingine bado unaweza kutuathiri sisi. Kwa mfano, naamini kabisa magaidi walivyopiga pale Westgate Kenya siyo Wakenya peke yao ambao walidhurika na kufa ni watu wa Mataifa mbalimbali inawezekana hata Watanzania. Hata kule Chuo Kikuu - Garisa pia siyo Wakenya peke yao nakumbuka kabisa kwamba katika watu waliokamatwa kupanga na kutekeleza ile njama, sisemi kupatikana na hatia mimi nazungumzia kukamatwa kama walipatikana na hatia hiyo ni baadaye, lakini mmojawapo alikuwa ni kijana wa Kitanzania. Kwa hiyo, maafa haya yanakwenda kila mahali hata Septemba 11 kule Marekani iligusa watu wengi duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la ugaidi pia linagusa haki ya kuishi (right to life) ambayo ndiyo Mama wa haki zote kwa hiyo, kwa kuridhia Itifaki hii pia tunatekeleza matakwa ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya kulinda haki ya msingi ya kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache labda ninashauri tu mambo mawili. Jambo la kwanza kwenye utekelezaji wa Itifaki hii hasa kwa upande wa mambo ya movement ya finances (fedha) ni vizuri tukawa waangalifu sana, kuna watu wengine huwa wanatumia tusiwe Wakatoliki kuliko Papa mwenyewe. Tusije tukaitekeleza hii Sheria kwa ukali mpaka tukazuia vijana wetu ambao wanataka kuibukia katika biashara za Kimataifa sasa. Tuwe na uchunguzi wa kina kabla hatujachukua hatua kwenye haya mambo ya fedha kwa sababu yanaweza yakatumika pia kufifisha juhudi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge ninayetoka Jimbo la Mpakani ninazo taarifa kwenye baadhi ya maeneo ambapo sisi tumekuwa wakali mpaka kuzuia biashara kwa upande wetu lakini wenzetu kule wakalegeza wakafanya biashara. Kwa hiyo, tuwe makini kidogo kwenye hilo kwamba tusije tukajiumiza wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu elimu sahihi juu ya ugaidi ni kitu gani na gaidi ni nani ili tusije tukaingia kwenye mtego wa kushabihisha ugaidi na kabila fulani na Taifa fulani na dini Fulani, jambo ambalo ni la hatari sana. Ni vizuri tu tukajua kwamba ugaidi ni uhalifu wa Kimataifa ambao unalenga tu maeneo yenye udhaifu either kwa kukosekana kwa haki kwenye uchumi au kukosekana kwa haki kwenye siasa na mambo ya uongozi, basi wanapenyea hapo hapo na kuingiza mambo ya ugaidi lakini hauna msingi wowote katika kabila lolote, hauna msingi wowote katika dini yoyote wala katika katika Taifa lolote lile. Elimu ni muhimu sana katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumaliza tu nirudi kuipongeza Serikali kwa kuleta Itifaki hii sasa hivi, pia Kamati kwa kweli mimi binafsi, kwa sababu sitoki kwenye Kamati husika wameni-impress sana kuanzia taarifa yao na Wajumbe wa Kamati walivyochangia, kwa kweli wameonesha umahiri mkubwa wa kuelewa Itifaki hii ambayo wameileta, wametufungulia hata sisi ambao siyo Wajumbe wa Kamati na hatujawahi kuchangia kwenye Kamati kupata ukereketwa wa kutaka kuchangia kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono na ninaomba Bunge lako Tukufu liunge mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)