Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Itifaki ya Mkataba ya Umoja Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi wa Mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongea neno ugaidi, haraka haraka kichwani linakujia jambo linalohusiana na vifo, ukosefu wa udhibiti na amani, uharibifu wa majengo na miundombinu, kuzalisha vikundi vya uhalifu kwa maana ya insurgency groups; kuzalisha vikundi vya Itikadi kali kwa maana Extremists groups; lakini pia na umaskini katika nchi zetu. Sisi kama Taifa tumeamua kupitisha Itifaki hii ya Kuzuia na Kupambana na Ugaidi. Kwanza niipongeze Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inayoongozwa na Mheshimiwa Masauni, Naibu wake Mheshimiwa Sagini, lakini pia na Katibu Mkuu Ndugu Christopher Kadio; wameweza kufikisha Itifaki hii kwenye Bunge letu Tukufu na leo tunakwenda kuridhia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamechangia faida zitakazotokana na kupitishwa kwa Itifaki hii, nami kama Mbunge pia ningependa kuchangia machache ambayo naamini kama Taifa letu litanufaika kutokana na kupitishwa kwa itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza na la msingi kama Taifa wajibu wetu ni kuhakikisha ulinzi na usalama. Hiyo ndiyo dhamana kuu ya Taifa lakini pia ndiyo dhamana ambayo tumepewa sisi Chama cha Mapinduzi kupitia Serikali yetu hii ya Awamu ya Sita; kuhakikisha kwamba tuna ulinzi na usalama katika Taifa kwa maana ya political stability. Tutakaporidhia Itifaki hii, basi tutakuwa tunatengeneza mazingira mazuri ya kuhakikisha Taifa letu lipo salama na shughuli zote zinazofanya na wananchi zinaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo kama Taifa tutafaidika na Itifaki hii, ni kupata na kujengewa uwezo wa mafunzo na mbinu mpya za kupambana na udhibiti wa ugaidi. Kama ambavyo Itifaki inasema tutashirikiana na mataifa ya wenzetu na Jumuiya za Kikanda, tuna Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC lakini pia Jumuiya mbalimbali za Kikanda ambazo tutashirikiana nao. Pia tutaendelea ku-share experience kwa maana ya uwezo kupitia vyuo vyetu mbalimbali vya mafunzo, sisi kaka Taifa tuna NDC - Nation Defense College ambapo tumekuwa tukiona mataifa mengine yanaleta pale watu, Wakufunzi lakini pia na Maafisa mbalimbali wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa ajili ya ku-share experience. Kwa hiyo, kama Taifa tutajenga uwezo na tutapata mafunzo na mbinu mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu na la muhimu litakalotusaidia ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Sisi Waafrika katika makuzi na malezi yetu tunaamini akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki, kwa maana ya kwamba tutakaposhirikiana kwenye changamoto mbalimbali za kukabiliana na hivi vikundi kama Boko Haramu, Anti Balaka, Ansar Dine, Al-Qaida, Al-Shabab, hivi vikundi mbalimbali vya kigaidi tutakaposhirikiana na mataifa mbalimbali, basi tutakuwa tunaimarisha ushirikiano wa kikanda, lakini pia inafanya tunakuwa wamoja na matatizo ya majirani zetu na sisi yanakuwa matatizo yetu. Atakapopata jambo Msumbiji, basi Tanzania utakwenda mbele, utakapopata jambo Tanzania, Malawi atakwenda mbele na hivyo hivyo ndivyo tunavyojenga ushirikiano wa Kikanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne na la mshingi ambalo tunaweza kulipata kupitia Itifaki hii ni kuweza kutumia kanzidata ambayo ipo Algeria kama ambapo Waheshimiwa Wabunge wamesema. Katika kupambana na ugaidi nyenzo muhimu kuu ni mbili; kwanza ni taarifa na jambo la pili ni fedha. Sasa kwenye suala la taarifa tutapata access ya data kupitia itifaki hii tutakapoiridhia kama Taifa. Hii itatusaidia sana kuwa na taarifa, lakini pia ugaidi unashamiri sana kwa kupitia pia taarifa na fedha. Kwa hiyo, hivi vitu vinategemeana, lakini kama Taifa kwa kuwa tumepata access ya hii kanzidata maana yake tutakuwa tunapata taarifa mapema lakini pia tunaweza kujiimarisha na kudhibiti ugaidi katika Taifa letu lakini pia katika Jumuiya ya Kikanda zinazotuzunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano na la muhimu, ni kuimarisha kwa uchumi wa nchi, kuongeza uwekezaji na ustawi wa jamii. Katika mataifa ambayo yanakabiliwa sana na wimbi la ugaidi, ni vigumu sana kwa uchumi kuimarika lakini pia na wawekezaji wanakuwa na mashaka ya kuwekeza mitaji yao. Kwa hiyo, kama Taifa tunaishukuru Serikali kwa kuweza kufikia hatua hii katika hili jambo zito na la muhimu, tuendelee kuimarisha usalama wa Taifa letu na kuhakikisha tunavutia uwekezaji na hatimaye kukuza ustawi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)