Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja kwa sababu mimi ni mjumbe wa Kamati ya Bajeti, lakini pili nitambue suala la mkopo wa trilioni 1.3 ambao ulifanywa kwa uwazi, Watanzania wakaelewa. (Makofi)

Kwa hiyo tuombe huu utamaduni wa hii mikopo tunayokopa kwa sababu wananchi ndio wanalipa, uendelee kuwa wazi huko tunakoendelea; uwe mkopo wa biashara, ama uwe mkopo usio na riba, ama uwe mkopo wa riba nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitazungumzia eneo dogo tu; uzuri Waziri ameji-commit hapa kwamba hizi fedha zitafuatiliwa mpaka mwisho na CAG atafanya kazi yake kwa ufanisi. Kwa hiyo tunategemea tunakoelekea tutapata taarifa mahususi kabisa jinsi hizi fedha zilivyotumika.

Mheshimiwa Spika, lakini mchango wangu utajikita kwenye shilingi bilioni 693 ambazo tunakwenda kukopa mkopo wa biashara kuziba nakisi. Mpaka sasa hivi kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Fedha, deni la Serikali ni shilingi trilioni 68.5, maana yake huu mkopo wa shilingi bilioni 693 unakwenda kuongezea deni la Serikali. Tukijumlisha na wa sekta binafsi ni trilioni 85. Kwa hiyo hapa tunazungumza deni la Serikali kwa taarifa za Wizara ni trilioni 68.5.

Mheshimiwa Spika, tunakwenda kuongeza bilioni 693, ambayo mimi siipingi kwa sababu ni sehemu ya timu ya Bajeti. Lakini bado kuna trilioni mbili za hati fungani ambazo tumeingia mkataba kwa ajili ya kulipa mifuko ya hifadhi, sehemu ya deni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tafsiri yake ni nini; kwamba hivi karibuni deni letu la Taifa lita-shift from the current 68 trillion to almost 70 trillion. Sasa ni jambo ambalo ni muhimu sana kama Taifa tuendelee kujifanyia tathmini na ili tuweze kwenda mbele vizuri.

Mheshimiwa Spika, majuzi hapa Kamati zako za Kisekta na Kamati za Fedha zimeileza Serikali ni maeneo gani ambayo kuna mianya ya fedha za umma kupotea ama kwa makusanyo mabovu au kwa mifumo kutokusomana, kwa hiyo watu wanatumia hayo madhaifu kupiga deal. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi ninatarajia Serikali ichukue yale maazimio ya Bunge kama sehemu ya kuongeza mapato yetu, siyo tukiwa tuna gap tunakimbilia kwenda kukopa. Kukimbilia kukopa inawezekana ni kujifinyisha uwezo wa kufikiri na uwezo wa kufanyia kazi changamoto zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Februari, CAG alituletea taarifa kwenye Kamati yetu ya Bajeti akielezea; na ninashukuru Dada Subira juzi alizungumza hapa kiujumla jumla. CAG akatuambia, juzi, tarehe 8 Februari, makusanyo gani ama mapato gani ambayo hayajakusanywa na Serikali ambayo ameelekeza kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, CAG anasema mapato ambayo hayajakusanywa ni shilingi trilioni 356. Na ukiangalia uchambuzi wa CAG…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa inatokea upande gani?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, kwa Hussein Nassor.

SPIKA: Mheshimiwa Hussein Amar.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ninataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba yule ni Mheshimiwa Subira, siyo Bwana Subira. Ahsante.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nimesema dada yangu Subira jamani, mbona ananitoa kwenye pozi.

SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee, malizia mchango wako.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nimesema Dada Subira, na yeye anajua yule ni Balozi wa Kodi, namzungumzia hapa Balozi wa Kodi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuna trilioni 356 ambazo Serikali imezikalia haijazikusanya, na CAG anasema sababu ya fedha kutokukusanywa; mosi, anasema kuchelewa utatuzi wa mapingamizi ya kodi. Kwa nini? Anasema kuna watumishi wachache ambao wanatakiwa wawepo kwenye zile Mamlaka za Rufaa za Kikodi. Liko ndani ya uwezo wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, CAG anasema TRA, wakusanyaji mapato, wana watumishi wachache.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie.

SPIKA: Dakika moja.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, namalizia.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali mkifanyia kazi kwa ufanisi hoja za Kamati za Bunge, hoja za CAG, biashara ya kwenda kukopa nje tutaiacha, tupunguzie nchi mizigo isiyokuwa na sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)