Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii. Nianze kwa kukupongeza wewe pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuaminiwa na Kamati Kuu, lakini pia kwa kupitishwa kwa kishindo na Bunge lako hili Tukufu. Nimwombe Mwenyezi Mungu aendelee kuwasimamia na kuwaongoza katika majukumu yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze pia CAG pamoja na ofisi yake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, lakini pia nadhani wajumbe wa Kamati ya LAAC, PAC na PIC wanafahamu namna ambavyo mafunzo yake yametusaidia na sasa tumekuwa kama ni ma-CAG wadogo. Niwapongeze pia Wenyeviti wetu wa Kamati hizi mbili, wame-present vizuri sana hoja za Kamati. Kwa hiyo nimesimama hapa kuunga mkono hoja za Kamati zote, hizi mbili kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na machache sana ya kuongezea katika taarifa ya LAAC. Nianzie na ubora wa majengo; kwa mujibu wa taarifa ya CAG tumekuwa tukipata taarifa mara kwa mara na hasa kwa hii taarifa ya mwisho aliyoileta CAG, kuna baadhi ya majengo ambapo akikagua utakuta kuna nyufa katika kuta na katika sakafu na hii haileti afya katika matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, ukichunguza sana utakuta sababu mojawapo ni kwamba baadhi ya halmashauri hazina Wahandisi wa kutosha, lakini hata wale Wahandisi ambao wapo wanakuwa hawana vitendea kazi, kwa mfano, usafiri. Kwa hiyo utakuta kwamba, hasa kwenye hii miradi ambayo inatumia force account, kwa kweli ni shida kwa sababu wanajenga tu wale mafundi ambao wameaminiwa, lakini Wahandisi wetu wanapokuwa wakihitajika kukagua, hawana usafiri, kwa hiyo hawafiki pale kwa wakati. Unakuta order imetolewa kwamba tunataka ndani ya mwezi mmoja wanafunzi wawe wameshaingia darasani, kwa hiyo wanaamua tu leo ameweka msingi, anapandisha tofali, moja kwa moja anaendelea lenta na kupaua, kwa hiyo yanakuja kutokea madhara kama hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nitoe ushauri tu kwa Serikali kwamba sasa ihakikishe kwamba kunakuwa na Wahandisi wa kutosha, lakini vile vile wapatiwe vitendea kazi kama usafiri ili waweze kwenda kwa wakati, wafanye ukaguzi kwa wakati na vilevile kutoa ushauri ili kuweza kupata majengo yenye ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee kidogo tena hoja yangu ya pili ambayo ni ya mikopo ambayo inatokana na asilimia kumi ya fedha za ndani kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu. Niseme tu maswali ya jana na leo katika eneo hili ni indication tosha kabisa kwamba kuna tatizo katika eneo hili la mikopo. Tatizo lipo na panahitajika ufuatiliaji wa karibu.

Mheshimiwa Spika, zipo halmashauri ambazo zinafanya vizuri katika eneo hili kwa upande wa marejesho ya mikopo na utakuta kuna wengine wanaorodhesha vizuri kabisa kwamba mikopo iliyorejeshwa kuna kiasi kadhaa ambacho kimepelekwa tena kwenye vikundi vingine. Hata hivyo, kuna baadhi ya halmashauri ambazo zinahitaji uangalizi na ufuatiliaji wa karibu kabisa ili kuweza kujua hizi fedha ambazo zimerejeshwa zinakwenda wapi na zinakopeshwa vipi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe tu Ofisi ya CAG kwa sababu mpaka sasa hakuna utaratibu wa kuzikagua hizi fedha ambazo zimerejeshwa, hatujaona utaratibu huu. Kwa hiyo niombe Ofisi ya CAG ifanye ukaguzi kuangalia hizi fedha ambazo zimerejeshwa zinakopeshwa na zinakopeshwa kwa namna gani na atoe taarifa ili kusudi Kamati iweze sasa kupata msingi wa kuhoji hizi halmashauri na kujua nini kinachoendelea. Niombe pia mamlaka husika itoe format katika halmashauri, namna bora ya kuweza kuzitolea taarifa hizi fedha ambazo zimekopeshwa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa halmashauri niombe halmashauri zijifanyie tathmini zenyewe, je, hii mikopo wanayotoa ina tija? Niseme tu kwamba, kama mikopo hairejeshwi, ina maana kabisa na ni indication moja wapo kwamba hakuna tija katika hii mikopo.

Mheshimiwa Spika, kimsingi tuna watumishi wa aina mbalimbali katika halmashauri kuna Maafisa Biashara, lakini utakuja kushangaa kwamba, unaona wanawake wengi na vijana na watu wenye ulemavu, ambao wamekopa wanajikita kwenye biashara za uchuuzi wa bidhaa ya aina moja katika eneo moja na utaona kwamba hawafuati zile principle za demand and supply na matokeo yake ni kwamba wanakosa wateja na mwisho wa siku wanakuwa wameshindwa kurejesha mikopo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba niombe halmashauri zetu ziwe intergreted, zishirikiane ili kusudi kuweza kuwasaidia hawa wanaochukua mikopo tuweze kutimiza malengo ambayo tunayakusudia katika utoaji wa hii mikopo.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)