Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami niungane na Wabunge wote kukupongeza kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Spika wa Bunge letu, nasi kama Wabunge tupo tayari kukupa ushirikiano wa asilimia mia moja. Ondoa shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi zote hizi, nirudie maneno yako ambayo nilikunukuu siku umekalia Kiti hicho kwa mara ya kwanza. Ulisema, sisi Wabunge ni daraja kati ya wananchi na Serikali. Tunapokuja humu, tumeleta mawazo ya Watanzania zaidi ya milioni 60 kwenda 70 waliopo nje. Tunayaleta matatizo katika Serikali yetu. Nami niseme, nina imani nawe, ninaamini kwenye daraja hili utakuwa kiungo kizuri cha kuweza kutufikishia maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna asiyejua kwamba lengo la kuja humu kusema ni kuishauri Serikali na Serikali kupokea mawazo yetu. Leo tunaposema huko nje Watanzania wote wanafahamu tuna changamoto kubwa ya ukatikaji wa umeme, hakuna asiyejua. Kila mahali umeme ni changamoto. Kwa hiyo, tunapokuja humu kuishauri Serikali, basi isitokee mtu akaona kama tunamwonea, hapana. Tunatoa tu maelekezo ayafuate mawazo yetu ili tukatatue tatizo na kuwasaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, nimeanzia hapo kwa sababu gani; leo tumekuja hapa kuchangia ripoti ya kamati mbili za PAC na LAAC. TANESCO wana matatizo makubwa sana, leo tukisema TANESCO kwenye ripoti ya CAG inasema imetengeneza faida mwaka 2019/2020 walitengeneza faida ya bilioni 45, kama waliweza kutengeneza faida kwa nini bado kuna changamoto?

Mheshimiwa Spika, nimnukuu Mheshimiwa Waziri alisema hapa, tuna matatizo mengi. Mchangiaji mmoja hapa amesema ukiangalia assets na madeni ya TANESCO ukiyalinganisha hakuna TANESCO. Kwa hiyo, tumekuja kutoa changamoto zilizoko katika Shirika letu la TANESCO watusikilize na changamoto ni kuipitia hii Ripoti ya CAG itawaonesha nini changamoto inayoikabili TANESCO kuliko kuanza kukimbia. Kama hukunitaka kwa nini unataka nini?

Mheshimiwa Spika, hakuna mtu ambaye anataka cheo cha mwenzake hapa. Kwa hiyo, tunapokuja humu tunaleta mawazo ya wananchi. Tunapokuja humu tunaishauri Serikali iende ikafanyie kazi. Kwa hiyo, nilitaka niseme TANESCO bado changamoto ipo na tusipokwenda vizuri bado tutaendelea kuwa na changamoto.

Mheshimiwa Spika, CAG amebainisha baadhi ya changamoto, lakini sasa ukija kuangalia inawezekana wamepikapika tu hesabu kuonesha wana faida, ili waturidhishe watanzania, lakini hakuna kinachoendelea katika shirika letu ndio maana hata wanaongeza gharama za kuunganisha umeme. Kwa hiyo, Serikali ichukue hatua ikiwemo kusikiliza na kufuatilia nini CAG aliandika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za TANESCO, lakini kumekuwa na changamoto kubwa sana. Wote sisi Wabunge kuna miradi inayoendelea ya REA, hii miradi inayoendelea ya REA fedha zinazotumika ni za watanzania wote, tumeongeza fedha kwenye tozo za mafuta kwa lengo la kufikisha huduma za umeme katika vijiji vyetu.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Venant Daudi, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Sophia Mwakagenda.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe Taarifa mchangiaji anayechangia sasa kwamba, anatoa mchango mzuri sana unaohusu nishati, lakini hapo najua ni hoja ya kamati, lakini Waziri wa Nishati wala Naibu wake hayupo. Kwa hiyo, wakati unachangia ufahamu hilo, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge nilishawahi kutoa ufafanuzi huko nyuma, nirudie tena; Serikali iko Bungeni. Serikali iko Bungeni na kwa kuwa, Serikali iko Bungeni tusiwe na wasiwasi mawazo yetu tunayoyatoa yote yanapokelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Venant Daudi malizia mchango wako.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru, ninafahamu watapitia hata kumbukumbu za Bunge, watayakuta haya.

Mheshimiwa Spika, kuna kiradi inayoendelea katika maeneo yetu, miradi hii gharama inayotumika au fedha zinazotumika ni za watanzania. Leo, kama kamati, tulikwenda kutembelea miradi mitatu katika mikoa mbalimbali, tuliyoyakuta huko Mungu atusaidie.

Mheshimiwa Spika, tumekwenda kukuta mkataba unasainiwa, labda mradi utatekelezwa kwa bilioni 30, wamefanya tathmini TANESCO, anakuja REA anabadilisha tena anasema mlikosea kufanya tathmini nitatekeleza kwa bilioni 37, inaongezeka bilioni saba zaidi ya asilimia 20. Kama yule wa kwanza alibaini biloni 30 kwa nini huyu anakuja miezi mitatu baadaye bilioni saba zaidi?

Mheshimiwa Spika, mimi nikuombe, dakika moja kwa kumalizia, nikuombe kupitia Bunge lako iundwe kamati maalum ambayo itakwenda kuchunguza miradi ya REA tangu tumeanza na ilete ripoti katika Bunge lako tukufu. Ahsante nakushukuru sana. (Makofi)