Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsate sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja ambazo ziko mezani. Nitachangia zaidi kwenye Kamati ya Miundimbinu. Nianze tu kwa kuipongeza Serikali na Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuijenga nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nitaongelea zaidi kwenye upande wa miundombinu nitajikita sana kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara, nitaanzia eneo hilo. Tumepitia vizuri taarifa zote za Kamati zinazoelezea utendaji kwa mwaka mzima. Tumeona namna ambavyo fedha za kuwezesha miradi mbalimbali zilivyoletwa, miradi ambayo iko kwenye majimbo yetu na nchini mwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo kubwa ambalo nitalieleza zaidi ni eneo la hizi barabara ambazo zinaunganisha mikoa. Hizi ni barabara ambazo zinasaidia uchumi katika nchi yetu. Kulikuwa na fedha ambazo zimetengwa, barabara katika maeneo mbalimbali zilitangazwa kwamba zitajengwa. Nitaeleza barabara chache, barabara ya Singida – Kwa Mtoro kwenda hadi Kibrashi Tanga, Barabara ya Mkiwa kupitia Itigi mpaka Makongoros Mbeya na barabara nyingine ambazo zinatoka Singida – Hydom, ni barabara ambazo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi ninavyoongea bado barabara hizo hazina wakandarasi. Tusitegemee katika muda wa mwaka wa fedha uliobaki, tukianza leo kutangaza kama barabara hizo zitakamilika. Kwa hiyo niiombe Serikali iweze kuhakikisha kwamba barabara hizo zinaanza kujengwa ili kufikia malengo yaliyopangwa na bajeti hii tunayoimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili pia naomba niseme kwamba, kumekuwa na kikwazo cha GN ambazo ni Wizara ya Fedha. Wizara ya Fedha imekuwa kikwazo katika kutoa GN kwa ajili ya kuruhusu barabara hizi zijengwe hata kama tumetenga fedha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali ikae pamoja. Haiwezekani Wizara ya Ujenzi inailalamikia Wizara ya Fedha, haiwezekani Wizara ya Mawasiliano inailalamikia Wizara ya Fedha, haiwezekani kwa sababu Serikali ni moja. Niombe sana, kupitia Kamati hii tumejadili, tunaendelea kuishauri Serikali ihakikishe GN inatoka mapema ili kuruhusu barabara hizi zijengwe kwa wakati ili kuweza kuharakisha maendeleo ya kweli ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo niipongeze sana TANROAD, wanafanya kazi nzuri sana ya kurekebisha barabara na kujenga barabara mpya. Pia katika kuwasimamia wakandarasi wamekuwa mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikihama eneo hili, niombe sana niende kwenye mawasiliano. Hapa nitaeleza zaidi kwenye bundle tunazoweka kwenye simu zetu. Kumekuwa na malalamiko makubwa sana na zaidi ya hapo tumeeleza sana TCRA kwamba wawasimamie watoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaweka bundle la wiki moja, kabla hujamaliza wiki, zile fedha zinaondoka ilhali ulilipia mwenyewe. Wananchi wanalalamika, tunaiomba Serikali kuhakikisha kwamba inawasaidia wananchi ili waweze kuwa na haki hayo ya msingi wakiweka bundle kwenye simu. Hili limekuwa ni tatizo, na hakuna majibu; hata customer care wanapopigiwa simu hawana majibu ya moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana Serikali ilifanyie kazi eneo hili ili kuwapa haki hawa wanaoitwa wateja, ambao ni wananchi wetu huko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili tumezungumza kwenye Kamati, lakini na hapa nimeona pia nilieleze ili Bunge lako Tukufu liweze kufahamu na wananchi wajue kwamba Wabunge tunawasemea kuhusiana na eneo hili ambalo limekuwa ni changamoto sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu nitaelezea Kampuni yetu ya Ndege ya ATCL. ATCL wanafanya kazi nzuri, wamehuishwa, tumewanunulia ndege za kutosha zinazozunguka nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili kuna maeneo mawili ambayo ni changamoto kubwa. Kwanza ni kuhusu bei; tumekuwa na changamoto ya bei za tickets za ndege. Leo hii ukiangalia bei kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma gharama inaanzia laki nne mpaka laki saba, kwa wale ambao wamekwenda Dubai; ni kama vile unaenda Dubai ilhali uko Tanzania. Kwenye hili kumekuwa na changamoto na hakuna majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi kumekuwa na changamoto pia ya kwamba leo mnafanya booking ya ndege; nimeangalia leo, ukiangalia hata kwenye schedule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, unga mkono hoja Mheshimiwa.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja mkono, lakini niiombe sana ATCL waangalie upya bei zao. Ahsante sana. (Makofi)