Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza kwenye Bunge lako kwanza nianze kwa kuipongeza Kamati ya Nishati na Madini kwa kazi kubwa ambayo tumeifanya katika kipindi cha utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi iliyotekelezwa kwa kipindi cha mwaka uliopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia masuala yanayohusu TANESCO peke yake. Mimi ninatokea kijijini, ukifika vijijini sasa hivi tuna taharuki kubwa sana ya masuala ya bei yaliyotolewa na TANESCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati mwaka jana tulikaa tukakubaliana kwamba tuchukue hata vile vijiji vya mjini tuviweke kwenye bei moja sawa na vijiji vya vijijini ili wananchi wengi waweze kuingia kwenye mfumo wa 27,000, lakini ghafla mabadiliko yametokea na kuwatenga watu wa mjini na watu wa vijiji. Sasa najiuliza, muda mwingi niko Dodoma na kijijini kwangu; nawaona hata Wagogo maskini wako humu humu ndani kwenye kata za mjini, lakini nikitoka nje ya mji nakuta kuna watu wako vijijini wana hadi ghorofa tatu wanaishi na familia zao. Sasa hiyo hesabu iliyopigwa kwa kweli ukiangalia kiundani naona kama kuna upendeleo. Niishauri Serikali, kwamba ni vizuri wakafuata ushauri wa Kamati, kwamba ile bei ya 27,000 iendelee mpaka kwenye zile kata za mjini ambazo nazo zina watu maskini kama walioko kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, suala la kukatika kwa umeme. Hili suala linaleta taharuki kubwa sana. Tuseme ukweli, Kamati imeona kwamba hakuna sababu za msingi, ukisikiliza ni kama ubabaishaji fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke, wakati umeme umeanza kukatika tulimwona Mheshimiwa Waziri wetu, Mheshimiwa Makamba aliruka hadi na helikopta akiionesha Tanzania kimataifa, kwamba tuna upungufu wa maji, mito imekauka. Chief Hangaya akaomba tukapata mvua, tumerudi tena kwenye mashine. Sasa, hii mitambo inaendeshwa kwa masaa, ndiyo maana Kamati tumeomba TANESCO walete schedule ya miaka mitano iliyopita service ilikuwa inafanyikaje na si kutuambia mitambo haikufanyiwa service. Kwa mtambo ambao haukufanyiwa service, kwa mitambo ya kisasa hii itapiga honi hakuna mtu atakayekaa humu ndani. Sasa ni kama ubabaishaji tu, hakuna sababu za msingi za kutukatia umeme mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeshauri kwamba ifanyike service kimkoa, angalau kiupande upande na si kufanya kwa nchi nzima, inakaa gizani na Serikali imehamasisha watu waingie kwenye soko la viwanda vidogo vidogo na viwanda vikubwa. Hii inaleta taharuki kubwa sana. Tuombe TANESCO ije na sababu maalum inayotusababisha sisi tukose umeme katika sehemu nyingi za biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la bwawa la umeme. Niko kwenye Kamati sasa hivi ni mwaka wa sita, ninamshukuru Mungu. Kamati tumeanza kwenda kwenye bwawa hili tangu likiwa pori tukakuta kimondo. Tumerudi mara ya pili na mara ya tatu, ukifika kweli unaona kazi zinafanyika. Sioni sababu ya hizi swaga zinazoendelea, kwa sababu wakati Mama Samia anaingia tulilipa trilioni mbili, certificates zote zilikuwa zimelipwa, hakukuwa na madeni na Mheshimiwa Mama Samia amelipa trilioni moja, hatuna certificate inayodai, tatizo liko wapi? Ni swaga zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnakumbuka hapa Mheshimiwa Waziri alitueleza kwenye Bunge hili kwamba mitambo imefika, tunasubiri crane iko barabarani. Sasa hivi crane imefika bado tunaambiwa yale mashimo ya kuweka ile mitambo iliyokuwa inashushwa kule chini yamejengwa substandard. Unajiuliza, wasomi wenzangu mnaniaungusha sana. Mnaniangusha sana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na wakandarasi wako pale, tuna watu wanasimamia, mainjinia wamesoma, Watanzania na Wazungu, tunamaliza kujenga foundation ile tunaambiwa imejengwa substandard.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)