Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru sana na kukupongeza kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Naibu Spika wetu katika Bunge hili tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara nipende kwa namna ya pekee kushukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Wajumbe wote kwa vile ambavyo wanatupa ushirikiano katika kuhakikisha kwamba tunatekeleza mipango ya Serikali, na hivyo basi imekuwa desturi ya Kamati hii kutushauri kwa umakini mkubwa kwa nia ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inathamini sana ushauri wa Kamati hii, na tutandelea kufanya nao kazi kwa ukaribu kuhakikisha yale ambayo wanatuelekeza tunayatekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara tunaendelea kupitia sera zetu, kuanzia Sera ya Uwekezaji, Sera ya Viwanda Vidogo (SMEs) na biashara ndogo na biashara ili ziendane na mazingira ya sasa ikiwa ni pamoja na kujumuisha vipaumbele na mipango ya maendeleo ya Taifa kwa ajili ya mabadiliko yanayoendelea katika dunia ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara tunatekeleza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunatekeleza blue print. Baadhi ya vitu ambavyo vimelalamikiwa sana ni kuwa na sehemu moja ya kuhudumia wawekezaji. Tanzania tunatengeneza sasa kitu inaitwa Tanzania Electronic Investment a single window ambayo hiyo itawezesha sasa wawekezaji kuwa na sehemu moja ambako watapata huduma nyingi ambazo zinatolewa na taasisi zetu. Kwa kuanzia tutaanza na BRELA, TIC na TRA ambazo zitaunganishwa pamoja katika mfumo huo ili kupunguza usumbufu kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunaendelea pia kuhamasisha ujenzi wa viwanda vidogo kwa maana ya kuwa na kungani za viwanda ambazo zitasaidia sana, unajua sekta kubwa ya viwanda ni viwanda vidogo, vya kati, lakini pia hatusahau viwanda vikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali tunaendelea kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi ili kuwe na ujenzi wa viwanda katika maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunaangalia pia kwa namna ya pekee kuona mifuko ya kuwezesha wajasiriamali inaongezewa fedha, lakini kuhakikisha pia inaboreshwa kwa kuunganishwa ile ambayo inawezekana ili iweze kuwa na tija kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa hili muhimu sana la utekelezaji miradi ya kimkakati ambayo imeongelewa sana. Nia ya Serikali hasa ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan, ameelekeza tuone sasa namna ya kukwamua miradi hii mikubwa ambayo itakuwa na impact kubwa sana katika maeneo ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tutaenda kuishughulikia kwa haraka iwezekanavyo, lakini kwa kuangalia kwa weledi ili kuhakikisha tija na manufaa ya nchi nzima kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo ili utajiri huu na maliasili hii tuliyonayo katika hii miradi ya kimkakati ambayo iko chini ya sekta hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inakuwa na tija kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini pia nashukuru Kamati na Wabunge wote ambao wametushauri, ushauri wao tunaenda kuufanyia kazi ili kuhakikisha tunaendelea kuhakikisha tunajenga uchumi wa viwanda kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii. Nakushukuru sana. (Makofi)