Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. FATMA H. TOUFIQ – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge waliochangia katika Taarifa yetu ya Kamati ya Masuala ya UKIMWI kwa mwaka 2021/ 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia ni saba, lakini pia upande wa Serikali tumepata ufafanuzi kutoka kwa Mawaziri wawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wabunge waliochangia, naomba kwanza nianzie upande wa Serikali ambapo Naibu Waziri wetu Mheshimiwa Ummy Nderiananga, ameipongeza sana Kamati na amekubali kwamba ushauri wote ambao Kamati tumeutoa utachukuliwa na utakwenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba kwa niaba ya Kamati niendelee kuipongeza sana Serikali na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa kinara wa kuhamasisha wanaume kwenda kupima. Naamini kabisa, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kinara, basi wanaume wengi zaidi watajitokeza na jamii kwa ujumla watakwenda kupima ili kusudi tuweze kupunguza hili suala zima la maambukizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Naibu Waziri amezungumzia kuhusu programs za vijana, tunashukuru sana. Basi nasi tunaendelea kusisitiza program hizi ziendelee ili kusudi tuweze kuwanusuru vijana wetu, kwa sababu tumeona kwamba kundi ambalo limeonesha kabisa kwamba linaathirika kwa sana ni la vijana kati ya miaka 15 – 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amezungumzia kuhusu suala zima la elimu hasa kwa Community Health Workers kuhusu magonjwa yasiyo ambukiza. Tunashukuru sana kulichukua hilo, tunaamini kabisa yote yatafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, amezungumzia kwamba uratibu umeshaanza chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, hili nalo sisi kama Kamati tunaendelea kuishauri Serikali ione namna bora kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu i-take lead kwa sababu hili jambo ni suala mtambuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba niendelee kuipongeza sana Serikali hasa kwenye hili suala la magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu kumekuwa na political will, tumeona kabisa jinsi gani Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekuwa akiongoza matembezi ili kuhakikisha kwamba Watanzania tunaendelea kuwa afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tumeona Mheshimiwa Makamu wa Rais akiongoza matembezi na Mheshimiwa Waziri Mkuu; yote haya inaonesha kabisa kwamba Serikali ina nia ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba suala zima la magonjwa yasiyoambukiza nchini kama siyo kupungua basi linakwisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niende kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia hoja hii. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia ni saba, akiwemo Mheshimiwa Abdul-Hafar, Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mheshimiwa Tecla Ungele, Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mheshimiwa Dkt. Alice, Mheshimiwa Dkt. Nyamoga na Mheshimiwa Mama Mushashu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ushauri wao, tumegundua kwamba jambo kubwa ambalo limezungumziwa hasa kwenye suala zima la Ukimwi, ni kuhusu Aids Trust Fund. Miongoni mwa ushauri ni kwamba hii kuwe kuna chanzo mahususi cha kutunisha mfuko huu. Naamini kwamba hili Serikali watakuwa wamelipokea, kwa sababu tunatamani hili suala la afua ya Ukimwi, fedha zitokane na sisi kwa fedha zetu za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye suala zima la elimu ya Ukimwi ni kuhusu matumizi ya condom. Mheshimiwa Abdul-Hafar amesisitiza suala la matumizi ya condom na pia kuhabarisha vijana wetu ili kusudi wasiende kuianza ngono mapema, lakini kama ikibidi, basi waweze kutumia zile njia za kujizuia ili mwisho wa siku wasiweze kupata maambukizi mapya.

Meshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limezungumziwa ni kuwepo na Tume itakayoshughulikia maradhi yasiyoambukiza. Hapa Waheshimiwa Wabunge watatu wamelizungumzia hili, nami kama Mwenyekiti wa Kamati pamoja na Kamati yetu, katika taarifa yetu, maoni na ushauri pia tumelizungumzia hili kwamba, kama ikiwezekana, basi tunaishauri Serikali iundwe tume maalum ya kuweza kushughulika na masuala ya magonjwa yasiyoambukiza; na ikiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, itakuwa ni nzuri zaidi kwa sababu hili ni jambo linahusu masuala mtambuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine uliotolewa kwenye issue ya elimu ya magonjwa yasiyoambukiza ni kwamba lazima kuwepo na suala la elimu ili watu waweze kujua, waweze kuchukua tahadhari mapema na kuweza kujinusuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla Waheshimiwa Wabunge wote wameongelea kuhusiana na suala zima la elimu ili kusudi wananchi au jamii iweze kuchukua tahadhari mapema wasiweze kupata magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limetolewa ushauri ni kuhusiana na wataalam wa physiotherapy. Mheshimiwa aliyetoa ushauri huu ni Mheshimiwa Nyamoga, kwamba wataalam hawa inabidi waende hadi katika ngazi ya Wilaya na ikiwezekana Serikali ione umuhimu sasa wa kujenga vyuo vya kutosha vya physiotherapy kwa sababu inaonesha kabisa kwamba magonjwa ya kuambukiza yanaongezeka. Kwa hiyo, hii itasaidia kukidhi magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumziwa ni kubadili mtindo wa maisha. Kwamba ili kuweza kukabiliana na suala zima magonjwa yasiyoambukiza, tuweze kubadilisha mtindo wetu wa maisha ili mwisho wa siku tuweze kuyazuia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumziwa ni kuhusiana na madawa ya kulevya, ambapo imezungumziwa kuhusiana na waraibu kwamba itakuwa ni vizuri waweze kupatiwa miradi. Kwamba, kuna vituo ambavyo vimekuwa vikitoa hii huduma ya methadone na kuna waraibu wengine ambao wamekuwa wakipona kabisa. Sasa je, baada ya kupona wanakwenda wapi? Basi, Serikali ione umuhimu sasa wa kutafuta miradi midogo midogo kama ikiwezekana kuwapa mikopo na kadhalika hao waraibu ili kusudi waweze kurudi katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, suala la lishe limeonekana kwamba nalo pia ni muhimu ili mwisho wa siku hawa vijana wanaotumia methadone waweze kupata lishe ambayo ni bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Haya yote naamini kabisa kwamba Serikali itayachukua na kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naliomba Bunge lako Tukufu kuunga mkono hoja yetu ya Kamati ya Masuala ya Ukimwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.