Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuongea katika Bunge hili la Kumi na Mbili kama Waziri wa Afya, niruhusu nianze kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniamini kuendelea kuwa msaidizi wake. Nimwahidi Mheshimiwa Rais, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwamba mimi na Mheshimiwa Dkt. Mollel tutaifanya kazi hii kwa kasi, ubunifu na weledi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kila Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kwa kuunga mkono hoja za Kamati zetu mbili; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya UKIMWI. Niishukuru sana Kamati zetu zote mbili na Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri. Tumepokea na niwaahidi kwamba tutafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda niseme mambo makubwa matatu. Jambo la kwanza ambalo limeongelewa kwenye Kamati na Waheshimiwa Wabunge ni suala la upatikanaji wa dawa. Katika Bunge hili zamani tunapoongea suala la dawa tulikuwa tunaongea ukosefu wa fedha za dawa, lakini tunamshukuru Rais Samia suala la dawa siyo suala la ukosefu wa fedha za dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukiri kwamba tunahitaji kujipanga zaidi katika kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana, kwa sababu tangu Rais Samia ameingia madarakani tayari Serikali imeshapeleka MSD zaidi ya bilioni 333. Sasa hivi kila mwezi tunapokea bilioni 15 kwa ajili ya dawa, vifaa na vifaatiba.

Kwa hiyo nikiri kweli, maana ukificha maradhi kifo hukuumbua, hali ya upatikanaji wa dawa hairidhishi. Kwa hiyo tunaangalia, tutaendelea kuboresha utendaji wa MSD ili iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya ununuzi, utunzaji na usambazaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili nilishafika MSD nikawaambia badala ya kupima upatikanaji wa dawa kwa kuwa na dawa za mwezi mmoja tutawapima kwa kuangalia dawa za miezi mitatu. Kuna Mheshimiwa Mbunge amesema dawa zinapelekwa wiki moja zinaisha kwa sababu dawa za miezi mitatu zinapelekwa dawa za siku mbili au tatu. Kwa hiyo hili tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, siyo tu MSD, MSD anaweza aka-procure dawa, lakini upatikanaji wa dawa katika ngazi za vituo vya kutoa huduma za afya kuanzia zahanati hadi hospitali zetu. Kwa hiyo pia tutaimarisha usimamizi wa suala zima la upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye usimamizi tumeona, na nashukuru Kamati pia imezungumzia suala la ulinganifu wa usambazaji wa dawa kwenye vituo. Kwa hiyo tutafufua zile timu za upembuzi yakinifu wa mahitaji ya dawa kulingana na magonjwa katika eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, saa nyingine navyo vituo vyetu kila mtu anajua top ten diseases katika eneo lake. Sasa badala ya kufanya quantification ya dawa anazohitaji kwa watu anaowahudumia analeta makisio madogo; kwa hiyo hili pia tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwa upande wa usimamizi wa dawa, kuna Mwongozo wa Taifa wa Matibabu (Standard National Treatment Guidelines), inasema dawa gani zinatakiwa zitolewe katika level gani. Tumeona, watu wetu badala ya kutoa, sisi kama Serikali tunatumia dawa ambazo ni generic, siyo brand, kwa hiyo unakuta mtu ameandikiwa paracetamol daktari anamuandikia Panadol, Panadol hazipo katika vituo vyetu vya kutoa huduma za afya kwa sababu ile ni brand, sisi tunatumia generic.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa ya matibabu ya maambukizi kwa mfano, flagyl, flagyl ni brand, kwa hiyo daktari unapomwandikia mgonjwa flagyl wakati mwongozo unakwambia ni metronidazole, tumeona pia ni tatizo, kwa hiyo tutaimarisha wataalam wetu wazingatie Mwongozo wa Taifa wa Matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda unakwenda. Suala la pili ni suala la bima ya afya kwa wotee… kabla ya hili, MSD kuhusu uzalishaji wa ndani wa dawa tunashukuru sheria imepita na tayari Serikali imeshatoa fedha zaidi ya bilioni 15.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MWENYEKITI: Nakuongezea dakika moja uzungumzie hilo suala la bima ya afya kwa wote.

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bima ya afya kwa wote, tumepokea maoni na ushauri. Tayari tulishakwenda kwenye Baraza la Mawaziri, tumepokea maelekezo ya Baraza la Mawaziri, tumeyafanyia kazi sasa hivi tuko tayari kurudi tena kwenye Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuomba kupitisha Sheria hiyo ya Bima ya Afya kwa kila Mtu. Kwa sababu tunaamini kwa kweli ndiyo itaweza pia kuwawezesha Watanzania kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo cha fedha. Tunaona Watanzania wanauza mashamba yao, wanauza baiskeli pale ambapo wanapata mgonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tumepokea maoni na ushauri kuhusu non-communicable diseases (magonjwa yasiyo ya kuambukiza), tutawekeza kwenye elimu pamoja na community health workers (wahudumu wa afya ngazi ya jamii) ili waweze kutoa elimu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, tayari ameshaanza kuratibu implementation ya activities mbalimbali katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Kwa hiyo suala hili tayari Waziri Mkuu yupo on-board na analisimamia kwa ukaribu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, tunashukuru kwa maoni na ushauri na tutayafanyia kazi. (Makofi)