Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa afya njema siku ya leo kutimiza wajibu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia kwa niaba ya Waziri wangu, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, nimshukuru Mheshimiwa Rais kuendelea kutuamini tuweze kuhudumu katika Wizara hii muhimu ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Mheshimiwa Rais tunakushukuru sana pamoja na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ni Wizara mtambuka, ina sekta tatu, inagusa maisha ya Watanzania lakini ajira kwa vijana wetu. Nishukuru Kamati yetu ya Bunge ya Huduma za Jamii chini ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti pamoja na Wabunge wenzetu, wamekuwa wakitushauri kwa dhati namna gani tunaweza tukafanya vizuri katika sekta hizi ambazo ni muhimu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi nimshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wamekuwa wakituelekeza tufanye nini kwenye sekta ya sanaa, sekta ya michezo na sekta ya utamaduni. Nianze kwenye sekta ya utamaduni; Kamati kwa ujumla imezungumzia mambo matatu, imezungumzia suala la BMT, suala la Bodi ya Filamu na BAKITA, nami nitajikita huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa utamaduni nishukuru sana jitihada ambazo anazifanya Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan. Rais wetu wakati anakuza diplomasia ya uchumi pamoja na wasaidizi wake wametusaidia sana kwa upande wa utamaduni na kwa upande wa kukuza Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana UNESCO imetangaza Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7 Julai. Hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, pamoja na wasaidizi wake. Sisi Wizara tunawashukuru kwa sababu kazi yetu inakuwa imerahisishwa na viongozi wetu na wamekuwa wakitupa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo halitoshi, chini ya Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan tumeona juzi tarehe 6, mwezi huu wa Februari wakati Makamu wa Rais akituwakilisha, akimwakilisha Mheshimiwa Rais wetu katika vikao vya Wakuu wa Nchi na Serikali katika Makao Makuu ya Afrika, pale Ethiopia, Makamu wa Rais alipeleka maombi maalum kwa niaba ya nchi yetu na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wetu kwamba Kiswahili sasa iwe lugha ya kazi. Mheshimiwa Rais tunakushukuru sana na AU waliridhia hili. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu, hii ni hatua kubwa sana kwa Taifa letu lakini pia kwa sekta yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge na sisi tumefanya nini? Kwa kuwa mmezungumzia kupitia Kamati hii, kazi ambayo tumefanya, tumeielekeza BAKITA – Mheshimiwa Waziri Mkuu tunamshukuru sana, alikuwa BAKITA juzi, ametupa maelekezo mahususi. Sisi na BAKITA tumeandaa mpango mkakati wa kubidhaisha Kiswahili wa miaka kumi, kuanzia 2021 mpaka 2031 ambao una thamani ya bilioni 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii inaendelea chini ya BAKITA, dada yetu Consolatha na timu yake wanafanya kazi nzuri na hata balozi mbalimbali wameshaanza kupata wataalam kupitia BAKITA; Ubalozi wa Korea Kusini, Nigeria na Balozi zingine kazi hii imeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kazi hii tunaifanya kwa kasi kubwa na tunaamini pia kadri ambavyo wanatupitishia bajeti kazi hii itakuwa rahisi sana. Hii ni heshima kwa Taifa letu na tunaomba tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa kazi hii ya kubidhaisha Kiswahili na kutuelekeza na tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu na kubwa, tunamshukuru pia Makamu wa Rais kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lilikuwa ni suala la Baraza la Michezo (BMT). Kamati imeshauri mambo kadhaa na wamekuwa wakitushauri sana kwa upande wa michezo. Wametushauri tuongeze mahusiano na Serikali za Mitaa, ma- DAS na ma-RAS wetu ni Wenyeviti katika Mikoa yetu kusimamia michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati wamezungumzia pia kuhakikisha utawala bora unapatikana katika vyama na vilabu vya michezo. Kwa niaba ya Waziri wangu, Mheshimiwa Mchengerwa, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba. kazi hii tunafanya, na tumekuwa tukifanya vikao na Maafisa Utamaduni na Maafisa Michezo, lakini ma-RAS na ma-DAS wetu tukipeana maelekezo nini cha kufanya kuboresha michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisipowapongeza Waheshimiwa Wabunge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)