Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

MHE. VITA R. KAWAWA K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Spika, kwanza nami naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuja kuifunga hoja yetu hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi, Usalama. Katika eneo letu walichangia watu watatu na mmoja ni Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa sababu mijadala hii inaonekana eneo kubwa limechangiwa sana na Kamati ya Maliasili na Utalii. Kwa hiyo, waliochangia kwenye Kamati yangu ni Mheshimiwa Chumi, Mheshimiwa Christopher Ole- Sendeka na Mheshimiwa Mkenge.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Chumi alizungumzia sana ongezeko la biashara (balance of trade) katika Kanda zetu za Afrika Mashariki na Jumuiya ya SADC. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwanza kwa kuifungua nchi yetu. Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia alipoapishwa alifanya ziara katika nchi za Afrika Mashariki na nchi za SADC. Hii imesaidia sana katika biashara yetu na tumeelezwa katika Kamati kwamba Itifaki ya Biashara ya mwaka 1996, nchi wanachama wa SADC zinatekeleza na zinaondoa vikwazo ambavyo vinasababisha biashara isifanyike vizuri.

Mheshiwa Spika, kwa hiyo, hii imesaidia baada ya Mheshimiwa Rais kwenda kuzungumza, sasa urari wa biashara umeongezeka kwa asilimia kubwa. Kwa mfano, nchi yetu katika kipindi hiki tumeweza kuuza na kupandisha biashara katika kipindi cha mwaka 2021 kutoka dola 1,235,000 mpaka dola 1,458,000 katika ukanda wa SADC. Takwimu zinaonesha kwamba balance of trade kwa mfano kati yetu na South Africa, sisi tunauza zaidi South Africa kuliko wao wanavyonunua kwetu sisi. Hii imetokana na juhudi kubwa za Mheshimiwa Rais na Wizara ya Mambo ya Nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Chumi alizungumzia kidogo kuhusu Kamati ya Mawaziri Nane ambao walienda kutaka kutatua migogoro vijijini. Mwaka 2021 Kamati ililetewa tatizo lililokuwa limejitokeza Mbarali; kuna vijiji ambavyo vilikuwa vinaingiliana na eneo la maliasili na kulikuwa na mauaji ya watu watatu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kulishughulikia suala lile, tulilopewa na Spika tuliwaita pia Mawaziri wa Kisekta ambao mmojawapo walikuwa hawa wanane na tulishauriana nao tukawaambia waende wakakamilishe lile zoezi walilolifanya la kuzunguka nchi nzima na waliifanya kazi hiyo, wamezunguka na wakatoa kauli. Sasa Kamati inaishauri Serikali imalizie ile kazi nzuri waliyoifanya ya kuwapa vijiji vile maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, mwisho Mheshimiwa Mkenge naye alizungumzia mambo ya NIDA, pia amepongeza sana; amezungumzia mtangamano wa Jumuiya ambao nimeshauelezea. Vile vile amezungumzia kuhusu MSD kuteuliwa kuwa supplier wa dawa katika nchi za Kikanda za SADC. Sisi tunaipongeza sana juhudi ambazo zimefanywa na Wizara ya Mambo ya Nje kushawishi mpaka nchi yetu kuteuliwa kuwa eneo ambalo litakuwa supplier mkubwa wa dawa katika nchi za SADC. Kwa hiyo, hili tunaliunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaipongeza Nyumbu kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kamati inaishauri Serikali kwamba iendelee kuipa Nyumbu fedha za kutosha kuweza kufanya kazi yake nzuri kwa sababu sasa hivi inatengeneza magari ya fire ambapo tuna uhaba sana wa magari ya fire. Kwa hiyo, tunapenda sana iwe inapewa fedha za kuweza kufanya kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Spika, mwisho Mheshimiwa Chumi alizungumzia pia kuhusu Maafisa wa juu wa Magereza, ni kweli ili kuleta mageuzi katika Jeshi letu la Magereza, Kamati inashauri Serikali kuziba nafasi zile za Maafisa wa Juu kulingana na Muundo wa Jeshi la Magereza.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naliomba Bunge lako Tukufu kuunga mkono hoja Kamati yetu ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, naafiki.