Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja hizi mbili za Kamati.

Mheshimiwa Spika, naomba ni-declare kwamba mimi ni mdau mkubwa sana wa mazingira; lakini ukiacha hivyo, hapa Bungeni mimi ni mdau mkubwa sana wa meno ya tembo, ninayetetea tembo wasing’olewe meno.

Mheshimiwa Spika, nimeguswa sana na mjadala unaoendelea nchini juu ya hili suala la Ngorongoro. Labda nishauri kabla sijaendelea, ipo haja kubwa ya Wabunge kutembelea hifadhi zetu. Mimi ni mdau mkubwa sana. Ipo haja kubwa ya kuzitembelea ili tuone tunapokuwa tunazizungumzia tunamaanisha nini? Najua hilo unaliweza, utupeleke tukazitembelee hizo hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 1979 Hifadhi ya Serengeti na Hifadhi ya Ngorongoro zilipewa hadhi ya Urithi wa Dunia; siyo wa Tanzania, ni Urithi wa Dunia. Mwaka 2018 UNESCO iliipa hadhi Ngorongoro kuwa ni moja kati ya Eneo la Utalii wa Miamba (Global Geopark), Aprili, 2018.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, hadhi hii haitolewi ovyo ovyo. Afrika hadhi hii ya Geopark iko kwenye nchi mbili tu; ipo kwenye nchi ya Tanzania na Morocco. Ni nchi mbili tu kwa Afrika. Yaani duniani ziko nchi tano tu zenye hadhi hii; zinaongezeka Brazil hapo na nchi nyingine. Kwa hiyo, ni nchi tano tu zina hadhi ya kuwa na utalii wa miamba, moja kati ya nchi hizo ni Tanzania kupitia Ngorongoro Park. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu tumepewa hadhi hiyo mwaka 2018, ndiyo ile aliyokuwa anasema kaka yangu pale, ndiyo kwa mara ya kwanza Tanzania tuliweza kuingiza mapato ya nchi shilingi bilioni 148 kwenda shilingi bilioni 150 baada ya kupewa hadhi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kupanga ni kuchagua. Tanzania ni nchi kubwa sana, tuchague lile eneo liwe la makazi ya watu au liwe moja kati ya Urithi wa Dunia, Utalii wa Miamba na chanzo cha tatu cha mapato kwenye nchi hii? Kupanga ni kuchagua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimekwenda Ngorongoro hivi karibuni. Nimefika pale, hilo eneo ambalo wanasema ndugu zangu wanaishi Wamasai, hali ni mbaya. Wale watu pale wamesema ng’ombe ziko laki moja, siyo kweli, kuna mifugo zaidi ya laki nane iko mle ndani, lakini mifugo inayomilikiwa na wazawa wa pale, wale Wamasai ni asilimia tatu tu. Sasa swali tujiulize, ile mifugo mingine inamilikiwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkitaka tuweze, Mheshimiwa Waziri Mkuu yuko hapa, toa tangazo kesho kwamba wale wananchi ng’ombe wanazomiliki zote ziwe za kwao, utaona anapigwa mwingine, analia mwingine. Utaona! Zile ng’ombe siyo zote ni za wale Wamasai. Vyombo vya dola si vipo! Au kazi yake ni kutumwagia sisi maji ya washawasha! Si waende wakafanye research pale! Wamasai wale hawamiliki zile ng’ombe wala kondoo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye haya mambo ya uhifadhi, haya mambo kidogo ni ya kitaalam, kibaya kuliko vyote, wale ndugu zetu siku hizi hawafugi ng’ombe, wanafuga kondoo; na kazi ya kondoo ni moja, kwenye uharibifu wa mazingira kondoo ndiyo inaongoza. Yeye akila, hali majani, anang’oa lile jani lote na mizizi yake. Maaana yake ni kwamba lile eneo litaota mmea ambao siyo rafiki kwenye eneo lile. Tunaenda kuua ule uwanda, na kile kivutio cha Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, tena nimesahau, hii shilingi bilioni ninayosema 148 au shilingi bilioni150 iliyozalishwa mwaka 2018, siyo ya Ngorongoro yote kwa ukubwa wake, ni kale ka- crater tu, kale ka-Ngorongoro Crater ndiyo kamezalisha hela zote hizo. Sasa imagine, eneo lote lile lingefanyiwa uwekezaji, kwa sababu crater pale ziko zaidi ya maja; ziko tatu sijui, zote zingefanyiwa uwekezaji, zote zingefanyiwa uendelezaji, nchi hii ingekuwa na fedha kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine watu wanajificha huko kwenu, ni majizi wengine. Yaani wanajificha chini ya siasa kumbe ndio ananyonya Taifa hili halafu mwisho wa siku anasema nawatetea; hawatetei watu, anatetea mali zake ambazo zimetunzwa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

T A A R I F A

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Olelekaita.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba tu nimpe taarifa mzungumzaji kwamba ukurasa wa 37 wa Ripoti ya Kamati, inasema hivi na ninaomba ninukuu: “Serikali imekuwa ikitumia mfumo wa matumizi ya ardhi mseto (multiple land use system) katika Hifadhi ya Ngorongoro kwa mujibu wa sheria na umeiletea Tanzania sifa ya kuitwa hifadhi na sehemu ya Urithi wa Dunia.

Mheshimiwa Spika, nataka nimpe tu taarifa mzungumzaji, wakati Ngorongoro inapewa hiyo hadhi ya Urithi wa Dunia, wafugaji hao walikuwepo na maisha yalikuwa yanaendelea; na sheria inaruhusu.

Mheshimiwa Spika, nampa mzungumzaji taarifa hiyo. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nimetoa ufafanuzi hapa wa matumizi ya ile kanuni ya kutoa taarifa na ndiyo maana hapa mbele huwa kuna nafasi zinatolewa za Mbunge kuchangia. Taarifa aliyoitoa sijaelewa ni eneo gani la Mheshimiwa Salome, labda ni sehemu ya kwanza aliyokuwa anatoa takwimu au ulikuwa unampa taarifa hiyo kwenye hoja ipi? Kwa sababu mimi nasikiliza ule mtiririko unavyokwenda, yaani hii taarifa uliyoitoa hapa ni kwenye mchango wake upi?

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, napenda tu ku-clarify. Alianza kwa kuelezea Ngorongoro kutambuliwa na UNESCO na kwamba imepewa hadhi ya Urithi wa Dunia. Kwa hiyo, nataka tu nimwambie kwamba Taarifa ya Kamati inasema hivyo na hao watu walikuwepo tu kipindi kile.

SPIKA: Sawa.

Waheshimiwa Wabunge, kabla hujasimama Mheshimiwa Salome; Kanuni ya 77 ngoja nisimame ili tuelewane vizuri. Kanuni ya 77 ndiyo inayozungumza kuhusu taarifa. Ukitoa taarifa sehemu ambayo siyo unayotolea ufafanuzi, unamfanya kwanza mchangiaji asielewe kama apokee taarifa yako ama asipokee. Ndiyo nasema lazima msikilize anapoingia kwenye hoja nyingine. Kwa sababu hapa alishaingia kwenye hoja nyingine ya kuashiria kwamba kuna watu wengine ambao mifugo yao ipo kule na sio wale wakazi wa pale. Kwa hiyo, nilitarajia taarifa inayokuja inataka kuzungumza ufafanuzi kuhusu uwepo wa mifugo ya watu wengine, kwa sababu kwenye hoja ile kuhusu maelezo ya tangazo la UNESCO, tangazo la World Heritage Site alikuwa ameshamaliza akahamia kwenye hoja nyingine.

Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, nawaomba sana, taarifa unatakiwa uitoe pale ili pia hata taarifa zetu Rasmi za Bunge, ziweke vizuri, yaani kwamba kuna Mbunge alisimama akafafanua vizuri ama akampa taarifa Mbunge kuhusu hoja hii. Sasa ikiwa mbali kule, hata sisi huku kwenye taarifa zetu, mtu anakuwa haelewi Mbunge aliyetoa taarifa, ilihusu nini? Kwa sababu kanuni ya 77 inavyoeleza kuhusu taarifa, ni kwamba aidha mtu amesahau jambo fulani au kama hajasahau, basi unataka kufafanua labda kuna jambo yeye hajaelewa.

Nadhani hapo tumeelewa ni wakati gani tutoe hizi taarifa; na kama nilivyosema, leo taarifa nimewaachia mtaendelea kutoa, lakini mzitoe wakati ule unaopaswa ili nasi taarifa zetu Rasmi za Bunge zikae sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Salome Makamba.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba niendelee na mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, nasisitiza, kupanga ni kuchagua, maamuzi yako mikononi mwetu. Sisi kule kwetu Shinyanga ni moja kati ya watu ambao tumeathirika sana na hili suala la kuhamishwa kupisha maeneo ya migodi. Kwanza wamesema vizuri ambao wanawatetea Wamasai waendelee kubaki ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, kwamba watu hawa miaka ya 1950 walitolewa Serengeti wakaletwa Ngorongoro na walikuwa ni watu 8,000; kwa maana walioletwa ni 4,000 na wale waliokutwa pale 4,000 wakawa 8,000.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi watu wale watu wameshafika laki moja na kitu. Asilimia 64 ya watoto wa wakazi walioko pale hawajui kusoma na kuandika. Utaenda wapi katika nchi ya Tanzania ukute asilimia 64 ya population hawajui kusoma na kuandika? Ilikuwa wakati ule wa Mwalimu Nyerere. Wako pale, wanasema madarasa yapo. Wale watoto hawasomi, kazi yao ni kuchunga ng’ombe za mabeberu ambao wamewapelekea kuchunga kwa ajili ya kuwasaidia kuwapa hela.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Taarifa ya Spika. Taarifa!

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, kesho na keshokutwa twende pale tukatembelee…

SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba kuna taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, ukisimama na gari la tour, watoto wanakuja kuomba kwenye gari. Ile picha iliyopo kwenye gazeti siyo ya uwongo.

SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba kuna taarifa kutoa kwa Mheshimiwa Emmanuel Shangai.

T A A R I F A

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Mheshimiwa Salome, anasema kwamba qatoto wengi waliopo Ngorongoro hawapo shuleni, wanachunga tu. Naomba nimtaarifu tu kwamba Tarafa ya Ngorongoro ina shule 30 na watoto wanasoma. Waliofaulu mwaka 2021 ambao Mheshimiwa Mama Samia amewapeleka shule ni zaidi ya watoto 1,000 wako Sekondari.

SPIKA: Sawa. Sasa ngoja…

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, kama anasema kwamba watu asilima 64 hawajui kusoma na kuandika, hiyo ilikuwa ni taarifa ya NBS ya 2017 iliyopikwa ambayo ilisema Kata ya Olbalbal wananchi asilima 47 wanategemea...

SPIKA: Mheshimiwa ngoja tuongozane vizuri ili taarifa yako ikae vizuri. Yeye kasema asilimia 64, nawe unakubali kwamba ni kweli isipokuwa ilipikwa. Sasa nitakusamehe kwa sababu ndiyo umekuja, lakini kanuni za humu ndani maana yake unachokisema ni kwamba Mheshimiwa Salome Makamba anasema uwongo; na kanuni zinazozungumza kuhusu Mbunge kusema uwongo ni kanuni nyingine, haiusiki hii ya taarifa. Ukishamtuhumu Mbunge kusema uwongo, tunaanza kufuata utaratibu wa wewe kuleta takwimu nyingine.

Kwa hiyo, ili nikuongoze vizuri utoe taarifa yako vizuri, kama siyo zile 64 wewe unazozijua, ni ngapi? Yaani ndiyo unaweza kusimama kwa kifungu hicho cha taarifa nilichoelezea. Yaani wewe unasimama unasema siyo 64 ila ni hizi.

Kwa mfano, sasa hivi hapa umesema watoto 1,000 wamefaulu. Swali litakuja, watoto 1,000 kati ya wangapi? Kwa sababu ndiyo utoaji wa taarifa. Yaani hapa ukisema 1,000 ukaniambia mimi ni asilimia 100, hilo linakuwa limeisha, kwamba watoto wamefaulu na wako shuleni kwa asilimia 100. La sivyo, tunaanza kuulizana sasa maswali ya kitakwimu hapa halafu tunaweza kuwa hatuna. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, nadhani tunaelewana vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Shangai, ulikuwa umemaliza? Nilikuwa nakuongoza ili taarifa yako itoke vizuri.

(Hapa Mhe. Emmanuel L. Shangai aliinama kuashiria kukubali kwamba alimaliza kutoa taarifa yake)

SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kutuongoza vizuri. Kwanza Mbunge aliyekaa anasema anazidi kudhihirisha tu kwamba population ni kubwa. Yaani watu walioko pale ni wengi kuliko wale 8,000 waliotegemewa, waliotungiwa hiyo sheria anayosema Mheshimwia Olelekaita. Sheria ilitungwa kwamba wakae 8,000 kwa sababu it was manageable, lakini sasa hivi hali ni mbaya. Kwa mujibu wa NBS, asilimia 50 ya wakazi wa Ngorongoro ni masikini. Sasa hao unaosema asilimia 50 ni masikini halafu kuna mifugo laki nane, wanakuwaje masikini na watu wana ng’ombe laki nane? Yaani ukiangalia tu hizi data unaona kabisa hapa kuna watu wachache wamepeleka mifugo yao ndani ya hifadhi ambao wanatetea maslahi yao binafsi, wameachana na maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya eneo la Ngorongoro ni very potential na kuna nchi jirani ambayo pia kuna vita ya kibiashara kwenye utalii. Juzi nimemwambia Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, ziko NGOs ambazo zimesajiliwa, ziko ndani ya nchi hii zinafadhiliwa na nchi Jirani; headquarter ni nchi Jirani. Ukienda kwenye NGO, wote wanaongea lafudhi ya nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ngorongoro ni yetu sote. Serikali ije na mkakati siyo kuwapiga watu mabomu, siyo kuwahamisha watu kwa nguvu. Hawa watu waandaliwe, wajengewe nyumba, wajengewe shule, Kituo cha Afya, wajengewe miundombinu ya kutosha, wahamishiwe pale na wenyewe waishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amesema vizuri ndugu yangu kwamba ndiyo maana hujaona Masai aliyevaa lubega amekuja hapa kuandamana kwamba hawataki kuhama. Nami nimeenda kwenye hifadhi, wale watu wapo ambao wameomba kwa barua, wameandika wanaomba kuhamishwa kwenye Hifadhi ya Ngorongoro. Wapo! Hata kesho Serikali itangaze, anayetaka kuhama Ngorongoro, uone kama watu hawajajitokeza! Wale watu wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa. Watoto wao hawasomi, hao matajiri wenye ng’ombe na kondoo, ziko biashara.

Mheshimiwa Spika, pale Hifadhi ya Ngorongoro imeripotiwa; ukienda kusoma ripoti ya Ngorongoro, mwaka 2021 peke yake tembo zaidi ya 20 wameuawa na faru mmoja. Chanzo cha kifo cha tembo wale na faru ni sumu. Wanawekewa sumu na wakazi wa pale; au wanawekewa sumu na watu ambao ni adui wa tembo na adui na faru. Tunahitaji tuambiwe na nani ili tujue kwamba Hifadhi ya Ngorongoro ni urithi wetu? Tunahitaji tuambiwe na nani ili tujue kwamba Hifadhi ya Ngorongoro ni utajiri wa dunia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakubali, inaweza kuwa yapo maslahi, lakini maslahi ya Taifa yanakuja kwanza. Hakuna mtu ambaye hapendi kuishi vizuri, hakuna! Pia hakuna mtu anayeweza kukubali kuona anazaa watoto hawajui kusoma, hawajui kuandika na mwisho wa siku anaishi kwenye umasikini. Kuna nyumba gani pale Ngorongoro? Nyumba wanazokaa, kwanza sheria haitaki waezeke zile nyumba kwa bati. Kwa hiyo, wanakaa kwenye nyumba ambazo zimewezekwa kwa manyasi. Leo Mbunge anasimama ndani ya Bunge hili anatetea watu wakakae kwenye nyumba za nyasi, mbona yeye hakai kwenye nyumba za manyasi? Kwa sababu Sheria ya Ngorongoro haikubali kujenga nyumba ya bati, yenye mbona anakaa kwenye nyumba nzuri ambayo imeezekwa vizuri! (Makofi)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Salome kwa sababu nilikusudia kukuongeza dakika moja ya kuchangia, Mheshimiwa Ole- Sendeka.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKE: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa dada yangu mpendwa Mheshimiwa Salome. Ngorongoro katika Wilaya zote za wafugaji ndiyo inayoongoza kwakuwa na wasomi wengi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ni Ngorongoro ndiyo iliyomtoa Jaji wa Kwanza Mmasai ambaye ameteuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Juzi; ni Ngorongoro ndiyo ina Ph.D. holders wengi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania… (Kicheko/Makofi)

MBUNGE FULANI: Ng’ombe wa nani? Ng’ombe wa nani? Ng’ombe wa nani? (Kicheko)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ole-Sendeka. Mheshimiwa Salome Makamba.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, hii ni sehemu ya mkakati. Wanachokifanya sasa, wale watoto wakibahatika wakapenyapenya wanaambiwa mkasome sheria ili wakija kule ndani watetee wasitoke kule ndani. Ni sehemu ya mkakati, yaani hii ni sehemu ya mkakati. Waangalie Wamasai wengi waliotoka kule kwanza wana ufadhili, lazima wapate ufadhili wa kwenda Chuo Kikuu. Anayemfadhili nani? Mimi sijapata mfadhili, natoka Shinyanga. Akipata mfadhili, condition namba mbili ni lazima akasome sheria ili kusudi aje akapambane nao. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua Serikali ina vyombo. Hii ni sehemu ya mkakati. Naomba Serikali ije na mpango wa kuwahamisha wananchi wanaoishi maisha ya kimasikini ya wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na mpango huo ujumuishe hawa watu kujengewa nyumba nzuri, wapewe ardhi nzuri ya ufugaji na pia wawekewe miundombinu mizuri ya kutosha ambayo itawafanya waishi kwa raha.

Mheshimiwa Spika, juu ya yote, Serikali itangaze, wale Wamasai zile ng’ombe kuanzia leo ziwe zao. Hilo ndiyo litakuwa mwisho wa matatizo. Ng’ombe, kondoo, mbuzi, ziwe za wale Wamasai wa mle hifadhini. Nakushukuru sana. (Makofi)