Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, nami nitangulize kutoa shukrani za dhati kwako kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu kwa kazi nyingi anazozifanya. Niwapongeze na Mawaziri ambao wamepata uteuzi hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie suala la Hifadhi ya Ngorongoro. Hifadhi yetu ya Ngorongoro ilianza rasmi mwaka 1954. Hifadhi hii wakati inaanzishwa kulikuwa na takriban watu kama 8,000. Watu 8,000 kwa wakati huo walikuwa ni wachache sana, lakini leo tunapozungumza hapa Bungeni kuna watu takriban 110,000. Sasa ni nini nataka nizungumze. Kama tunakwenda kuwa na hifadhi ina watu zaidi ya 110,000, hatuwezi kuiita hifadhi kwa kweli, tusidanganyane kwenye Bunge hili. Lakini hii ni rasilimali ya Taifa.

Mheshimiwa Spika,tukiangalia rekodi za mapato ya makusanyo ya fedha wenye Hifadhi yetu ya Ngorongoro; mwaka 2018 tulikusanya bilioni 143.

T A A R I F A

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Simwoni anayeomba taarifa, ni nani!

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, niko hapa.

SPIKA: Nimekuona tayari, Mheshimiwa Jafari Chege.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, sina budi na wala sina namna ya kumwondoa mchangiaji kwenye hoja yake ya msingi, naaka tu nimpe taarifa kwamba nje ya watu zaidi ya 100,000 wanaopatikana pale tunachozungumza ni pamoja na aina ya shughuli zinazofanyika kwenye ile hifadhi ya Ngorongoro. Mojawapo ikiwa ni kwamba miaka hiyo ambayo watu walikuwa ni zaidi ya 8,000 ng’ombe waliokuwa kwenye hifadhi walikadiriwa kuwa 12,000. Leo tunavyozungumza kuna ng’ombe zaidi ya laki moja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka nimpe taarifa ili aende akijua kwamba hayo yote yanafanyika kwenye Hifadhi ya Ngorongoro.

SPIKA: Sasa kabla sijakuuliza Mheshimiwa Mtenga uendelee na mchango wako, nilikuwa najizuia kidogo kusema kanuni zetu, maana nachukua muda wenu kidogo, nilikusudia kuwakumbusha baadaye. Kwa sababu usipomsikiliza Mbunge mwenzako kumaliza hoja yake, huenda hilo jambo, yaani unatakiwa umuingizie taarifa akiwa amemaliza kile anachokisema ili ujue kuwa kuna jambo amelisahau. kwa sababu pungufu ya hapo maana yake wewe unamuingizia taarifa yako, sasa haelewi kama mtiririko wake aendelee nao ama vipi.

Kwa hiyo tuwe wavumilivu kidogo. Leo taarifa zinaruhusiwa kabisa, wala msiwe na wasiwasi, lakini mwache yule mwenye hoja amalize ile hoja, anapokwenda kwenye hoja nyingine unagundua kwamba amesahau hii sasa ngoja nimuongeze, ndilo lengo hasa la hiyo kanuni yetu ya Taarifa.

Mheshimiwa Mtenga.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza niipokee taarifa, lakini nilikuwa nazungumzia mwaka 1820 mapato ya Ngorongoro yalikuwa bilioni 143. Tulipoingia 20…

SPIKA: Samahani, ulikusudia kusema 1820 au 2018.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ni mwaka 2018, Mheshimiwa Chege alinitoa kidogo kwenye mstari.

Mheshimiwa Spika, tulipoingia mwaka 2019 tukakuta tuna fedha ambazo tulizikusanya bilioni 124, lakini 2020 tukakusanya fedha bilioni 31.

Mheshimiwa Spika, sasa naziweka hizi record ili tuone jinsi hifadhi yetu inavyokwenda kuteketea na masuala ya mifugo pamoja na kaya ambazo zipo kwenye hifadhi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwenye hifadhi hii kuna kaya zaidi ya 22, lakini leo tunapotaka kuzungumzia watalii wanaoingia Ngorongoro imekuwa ni hali ya hatari. Watalii wanapoingia Ngorongoro kwanza lazima wakutane na ng’ombe, mbuzi pamoja na kondoo ndipo waingie huko ndani.

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi kuna vitu vinafichwa kwenye Ngorongoro. Leo kuna watu wanauawa na simba, wanazikwa usiku, haya hayazungumzwi. Wanafika mahali kuwazika watu hawa usiku Serikali isije ikaelewa na ikatambua kwamba wananchi wao wanauawa mbugani.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe ushauri na ushauri wangu, pale tunapozungumza kwamba tunataka hifadhi iwepo lazima tufike mahali tukubaliane kwamba hifadhi hii iwepo. Kwa sababu kwa mujibu wa sheria, kama hawa watu walikuwa 8,000, leo wako 110,000, wametokea wapi zaidi ya 102,000? Kwa mkataba upi unaozungumzwa? Lazima vitu hivi tuviangalie.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe angalizo moja. Kwetu kule Mtwara kulikuwa na mradi wa gesi. Mradi ule wa gesi ukazua mambo mengi sana, lakini kwenye Bunge hili ikasemwa kwamba mradi ule ni wa kitaifa na Serikali ikachukua maamuzi na gesi ile ikatoka Mtwara ikaja Kinyerezi – Dar es Salaam na sasa ndiyo imekuwa sehemu ya msaada wa umeme wa gesi ya Mtwara. Hakuna sehemu tulipozungumza kwamba sasa katika hii rasilimali tugawane mbavu, hakuna. Hata hivyo, huku tunapoelekea kwenye suala la Ngorongoro, leo kuna wafugaji wako mle ndani, twendeni kwa wale wafugaji wakaombe mifugo waliyokuwa nayo halafu wataowaona watu walio nyuma ya mifugo ile.

Mheshimiwa Spika, wale waliopo ndani ya Ngorongoro si wenye mifugo yao; na hili lipo, si kwamba ni jambo ambalo tunalizungumza tu hapa. Sasa kama kuna matajiri wako nje, wanafanya kazi wao kugeuka kuwa NGOs na NGOs sasa hivi ziko kule zinaelimisha watu jinsi ya kutohama.

Mheshimiwa Spika, kwa suala la Ngorongoro tufike mahali kama Bunge tuchukue hatua. Hali ya Ngorongoro ni mbaya. Naishauri Serikali, hizi kaya 22 twendeni tuwatafutie makazi au tuwalipe fidia, hawa watu tuwaondoe kwa utaratibu.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu ambacho kipo ndani ya pazia; leo tunazungumza wenzetu wapo mle ndani, wanafuga; si wao tu, kuna wenzetu wa nchi Jirani wanafanya kila njia Ngorongoro ife na sisi tumejifungia humu Bungeni. Pia wako wenzetu wanatumika. Huko nje kuna matajiri, kwenye hoteli kuna matajiri kutoka Ngorongoro. Lazima tuelezane humu ndani. Wamekuja kufuata nini matajiri? Mbona hatujawaona Wamasai wamekuja na lubega wanasema mimi ndiye mwenye ng’ombe 200? Wanakuja matajiri hapa wanakaa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii inaumiza sana. Nimezungumza kwa uchungu kwa sababu Jimbo langu mimi la Mtwara Mjini ni Jimbo ambalo ni masikini, na ndiyo maana leo ninazungumza kwa ukali sana. Hata tukiangalia kwenye bajeti, mimi nimetoa gesi kuileta huku, kwenye bajeti, tuiangalie Arusha, sisi tunapata sawa na Arusha? Arusha sawa na Mtwara? Si vitu viwili tofauti? Mtwara haiwezi kuingia Arusha hata kwa mara 200 wala kwa mara 100, haiwezi kuingia Arusha, lakini tunapoingia kwenye kutafuta rasilimali ya Taifa, keki tunagawana sawasawa. Kuna haja gani sasa ya wenzetu kuzuia hiyo keki wao wanataka kuihujumu hiyo keki? Hili halikubaliki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale kuna Baraza la Wafugaji. Baraza lile la Wafugaji ndicho chanzo chote mnachoona kwenye mgogoro huu tuliokuwa nao. Ngorongoro wenyewe walikuwa wanawapa hela zaidi ya bilioni tatu kwa mwaka kuendesha shughuli zao. Zile bilioni tatu sasa ndizo zimegeuka kuwa chungu kwa Serikali. Tunapigwa na fedha zile ambazo tulikuwa tunawapa Baraza la Wafugaji.

Mheshimiwa Spika, kanuni sizijui sana, lakini kuna maneno ningesema hapa, naogopa sana unaweza ukanifukuza kutoka nje, ila nikuombe, kama walipeleka Mtwara kule vifaru, ma-bulldozer pamoja na vitu vingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HASSAN S. MTENGA: …kwamba rasilimali ile ya taifa iwe keki ya Taifa, tunaogopa nini? Au kwa sababu kuna matajiri?

Mheshimiwa Spika, ni vyema sasa, kama waling’ata jongoo Mtwara wang’ate hao jongoo na sehemu nyingine. Tukiiacha Ngorongoro kesho tutakwenda Mfinga Iringa, kesho kutwa watahamia Serengeti na mwaka ujao watakuja pale Mbeya; halafu tunakaa humu tunajifungia, tunaona ni vitu vya kawaida tu?

Mheshimiwa Spika, tufike mahali…

SPIKA: Dakika moja, malizia Mheshimiwa.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru sana. Zingekuwa mbili ningekushukuru zaidi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa namna moja au nyingine mgogoro ule hauwezi kwisha kwa mazungumzo kama wanavyodai, kwa sababu wenzetu wanatoka wanakwenda kule wanashawishi watu, leo hii wameshajipanga, wanasema njia zote tu-block, tuanze Maandamano pamoja na vitu vingine.

Sasa hawa ni wenzetu wanafanya vitu hivi. Huo mgogoro wanakwambia wewe uende ukazungumza, ukazungumze na nani? Ahsante sana.