Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na binafsi nikupongeze kwa sababu najua umechaguliwa siku ile nami nikaapishwa; kwa hiyo mimi ni Mbunge wako uliyemuapisha kati ya Wabunge wote waliopo kwenye Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, pia niipongeze Kamati kwa taarifa yao nzuri. Hata hivyo nitoe taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba eneo la Ngorongoro haliwezi kufa, kwa sababu wananchi walioko katika Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni wananchi ambao ni wahifadhi namba moja tofauti na wahifadhi wa vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi waliopo Tarafa ya Ngorongoro au Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo inaongozwa kwa mfumo wa ardhi mseto ni wananchi ambao katika eneo hilo wameishi miaka 60 bila kula wanyama na bila kuwa wawindaji. Wananchi hao sasa hivi tukiona kwenye vyombo vya habari wako very victimized, wanaitwa ni majangili, ni watu maskini ndani ya Tanzania, as if kwamba kuna ombaomba katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, kuna vyombo vya habari ambavyo sasa hivi kila siku ni kuandika kuhusiana na eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, kwamba wananchi sasa hivi ni tatizo. Nadhani Serikali kwanza ingewatambua wale wananchi kama wahifadhi waliohifadhi kwa niaba ya wananchi wengine milioni 60 wa Tanzania, lakini si kuwaona kama tatizo.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa kwamba, kwenye eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro watoto wanakwenda shule, si kama inavyotangazwa kwenye vyombo vya habari vya akina Kitenge. Kule kwetu kuna shule za msingi 30 na watoto wanakwenda shule; kuna vituo vya afya, kuna zahanati, kuna maendeleo mengine ambayo Watanzania wengine wanayo. Kama imefika sehemu tunaona labda ni tatizo, mheshimiwa Rais tarehe 16 mwezi wa Kumi, akiwa Arusha alisema kwamba ni lazima tukae na wananchi ili tutafute suluhu ya changamoto zilizopo katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niishauri Kamati pamoja na Wizara, kwamba ni lazima kukaa na wale wananchi. Kwa hali ilivyo kwa sasa, kumekuwa na enmity kubwa sana kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wananchi waliopo ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro; huku tukijua kwamba wananchi hao wako kisheria, hawajavamia. Wale wananchi walikuwepo na waliingia mkataba na mkoloni mwaka 1959 wakati walipofanya makubaliano kutoka Moru – Serengeti kutoka mwaka 1918 mpaka mwaka 1948, ndipo wananchi wale wakaamua kuhama kutoka Serengeti na kuja katika maeneo ya higher land ambayo ni Ngorongoro ya sasa (Makofi).

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunawaona wale wananchi kama ni wananchi ambao ni wavamiaji. Hao waandishi wa habari wa mitaani, anatoka mtu anasema nimesafiri kilometa 400 kumtafuta tembo Ngorongoro, hiyo si kweli. Ngorongoro tembo wako njiani kwa wale waliokwenda na ni wapi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro unaweza ukasafiri kilometa 400 katika eneo la square kilometer 8,100? Hakuna. Sehemu ya mbali ni Nayobi ambayo ni kilometa 80 na sehemu nyingine ni Kakensya ambayo ni kilometa 75, hakuna sehemu unayoweza ukatembea hivyo. Kwa hiyo, niombe, kwanza, Serikali iingilie kati utumiaji wa vyombo vya habari kwa ajili ya kuwaonesha wananchi wale kama hawafai.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ole-Sendeka amesoma lile gazeti. Ukisoma kama mwananchi uliye Ngorongoro, ukaona jinsi unavyoandikwa, unaishi na wanyama, unaishi na pofu, unaishi na wanyama wote na pundamilia, wanalala mpaka bomani, lakini unaonekana kama mtu ambaye hufai. That is totally haihitajiki katika maisha haya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi ni…

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Olelekaita.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Ngorongoro kwamba sheria nchi hii hairuhusu kabisa aina ya reporting iliyofanyika na magazeti hayo na kwamba kuna regulation inaitwa The Electronic and Postal communication (online contempt regulation, 2018) inakataza aina ya publication inayo-cause public disorder, bad language, discouraging, abuse na calculated words to offend a particular group ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo sheria za nchi zinakataza na ni suala tu la Mheshimiwa Attorney General na Serikali kuliangalia hili ili haya yasitokee. Ahsante sana.

SPIKA: Mheshimiwa Emmanuel Shangai.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na eneo la Pori Tengefu la Loliondo; najua pori hilo lilitangazwa pamoja na mapori mengine 49 mwaka 1974 kwa G/N 459, lakini ukijaribu kuangalia, baada ya kutangazwa mwaka 1974 Waziri alitakiwa kutangaza ndani ya miezi 12, lakini hayakufanyika hivyo.

Mheshimiwa Spika, eneo la pori tengefu tunaloliongelea watu wengine huku nje tunaona kama vile ni ardhi ambayo haina watu. Ardhi ile inakaliwa na wananchi zaidi ya 80,000, kuna vijiji zaidi ya 23, kuna kata nane. Sasa leo hii ukisema uchukue kilometa 1,500 wale wananchi hawana sehemu nyingine ya kwenda na wala hawana sehemu ya malisho kwa ajili ya mifugo yao na huku tukijua kwamba Wilaya yetu ya Ngorongoro asilimia 95 ni wafugaji, wanategemea mifugo.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya Mkuu wa Mkoa alikwenda Loliondo, amekwenda kutoa matamko ambayo yameleta taharuki ndani ya Wilaya ya Ngorongoro. Kwa sasa hivi wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na niiombe Serikali kutafuta namna ya kutuliza hali ile ambayo inatumika na magazeti na baadhi ya watu ambao hawana nia na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, niiombe tu Serikali, kama ina nia njema ya kutatua matatizo ya Wilaya ya Ngorongoro ni lazima ikae na wananchi meza moja na kutafuta njia ya kutatua changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, Kamati imeweka vizuri, kwamba tutafute namna bora ya kutatua matatizo yale. Kwa sababu wananchi wetu wanategemea kwamba Serikali yao itawasaidia, itawasikiliza na kuwaletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)