Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa hiii nafasi, lakini sitakuwa nimetenda haki kama nami sitaungana na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Peramiho, kumshukuru sana sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya na wananchi wangu wa Jimbo la Peramiho wamesema kwa kweli wanamshukuru sana sana kwa fedha nyingi alizozipeleka kwenye Jimbo la Peramiho, kwa ajili ya kuleta maendeleo. Tunamwambia, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Peramiho wamesema kwa kweli wanakubaliana na ule usemi unaosema, unapokutana na mtu ambaye yuko strong, kazi yako wewe ni kum-support. Kwa hiyo, sisi tunam-support Rais yetu kwa sababu yuko very strong, ameamua kuleta mabadiliko kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, tunam-support lakini wananchi wa Jimbo la Peramiho wanasema, Mheshimiwa Rais kwa sababu ameamua kuwa hard worker, Waswahili wanasema, mtu wa namna hiyo anatakiwa kuwa encouraged. Kwa hiyo, nasi tunam-encourage Mheshimiwa Rais kwa kazi yake nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa niyaseme hayo kwa sababu nisingewatendea haki wananchi wangu wa Jimbo la Peramiho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye Kamati yetu ya Sheria Ndogo. Kwa niaba ya Serikali naomba nichukue nafasi hii kwa kweli kumshukuru sana sana Mwenyekiti, Mheshimiwa Rweikiza, Wakili msomi. Pia namshukuru sana Wakili msomi mwingine, Mheshimiwa Ridhiwani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo; na Wajumbe ambapo Wajumbe wa Kamati hiyo kwa kweli ni wabobezi na ni wataalam kabisa kwenye mambo haya ya sheria na wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwa Serikali katika kufanya mapitio ya hizi Sheria Ndogo na kutushauri mambo ya msingi sana. Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ninaomba niwashukuru sana, ahsanteni sana kwa kazi hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tunayo safari ndefu katika kufanya mageuzi ya kutosha katika uandishi wa Sheria Ndogo.

Naomba niwakumbushe tu watumishi wa Umma na hasa hawa ambao wamekuwa wakitusaidia kutuandikia hizi Sheria Ndogo kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Taifa kwa ujumla. Ibara ya 35(1) inaeleza wazi kwamba shughuli za utendaji za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zitatekelezwa na watumishi wa Serikali, lakini wanatekeleza shughuli hizo kwa niaba ya mwenye Serikali yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana, wanapokuwa kwenye kazi hii ya kutunga Sheria Ndogo wajue wamekasimiwa jukumu hili na mwenye mamlaka ya Serikali hii. Kwa hiyo, umakini katika utungaji wa Sheria Ndogo unahitajika kwa viwango vya juu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana kama hatutakuwa tunaelewana ndani ya Serikali na hasa hawa watumishi wa Serikali ambao wamekasimiwa madaraka ya kutusaidia kutunga Sheria Ndogo kwa mujibu wa Bunge; limekasimu madaraka kwa Serikali ili kutunga Sheria hizi Ndogo kwa ustawi wa Watanzania. Sasa wanapokiuka misingi bora ya utungaji wa sheria, kwa kweli hawatendi haki kwa Serikali yetu. Kama makosa hayo yanajirudia siku kwa siku, nawaomba sana wakae chini, watafakari na kufanya marekebisho ya kutosha kwa kuzingatia maoni na ushauri wa Kamati ya Sheria Ndogo ambao wamekuwa wakiutoa kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunafanya nini sisi ndani ya Serikali? Tunafikiri tufanye mapitio kwa ujumla wake. Kwanza, tunataka sasa tuangalie hivi ni sekta zipi ambazo zinaongoza kwa kuwa na Sheria Ndogo mbovu, ambazo zinakataliwa kila siku ndani ya Kamati ya Sheria Ndogo? Ni lazima ifike mahali sasa tunakubaliana ndani ya Serikali tujue sekta hizo ambazo zinarekebishwa kila siku lakini bado hazina umakini katika utunzi wa Sheria Ndogo. Ni sekta zipi zinazoongoza? Tukijua hivyo, tutajua je, ni makusudi ama je, wataalamu wetu kwenye sekta hizo wanaotusaidia kutunga Sheria hizi Ndogo umahiri na ubobezi katika kazi hiyo ni wa chini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeamua sasa kwa kweli hebu tujitafakari tutazamane kwanza sisi wenyewe kwenye hizi sekta. Ni sekta ipi inayoongoza? Tukijua hilo, itatusaidia kutoka mahali hapo. Vinginevyo itakuwa ni marudio, marudio. Kamati ya Sheria ya Ndogo itakuwa inasema tunapokutana makosa ni hayo hayo, ni hayo hayo. Lazima tutafute mwarobaini na jambo hili liishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa ninapongeza Wabunge wamesema hapa, ukiangalia trend kwa sasa hivi, makosa yanazidi kupungua, siyo kama tulivyoanza huko nyuma. Huko nyuma akina Mheshimiwa Aida wanajua, ilikuwa Kamati ikija kusoma hapa taarifa yake, makosa hayo yanaweza kufika 400 mpaka 500. Sasa hivi tunapopongezwa leo Serikalini, kwa kweli juhudi imefanyika na wala siyo ya kwetu sisi kama Serikali tu, Bunge limetusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mwenyekiti anapokuja kusema makosa yako 70, hiyo kwa kweli kwangu mimi ambaye ninajua historia, tulikotoka mpaka tulikofika, ni achievement kubwa. Hatuwezi kujipongeza peke yetu, tunawashukuru sana Bunge na tunaishukuru sana Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, uko usemi wa Kiswahili kwamba mgema akisifiwa tembo analitia maji. Tusingependa tufike hapo, kwamba tumepunguza hayo makosa mpaka kufika 70 leo kwenye ripoti ya Kamati, tungependa yaishe kama inawezekana. Ila yakiisha Kamati ya Sheria Ndogo sasa kazi itakuwa…, lakini tungependa yaishe. Ikiwezekana yaishe yote na hilo ni kazi yetu kama Serikali lazima tujitahidi tufanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu kwamba kwa kuwa hali ni hiyo, ni lazima tuungane pamoja na Kamati ya Bunge kuona ushauri wanaotupatia unaweza kutekelezwa kwa kiwango kikubwa ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii ndani ya Bunge lako Tukufu, kwanza ninapokea maelekezo ya Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo kama yalivyowasilishwa hapa kama hoja ya msingi na mtoa hoja atakuja kuhitimisha, lakini nitumie nafasi hii mbele ya Bunge hili kuwaagiza Watendaji wa Serikali wote huko ambako wanatutungia hizi Sheria Ndogo, wale waliokasimiwa hayo majukumu yetu ya kutunga Sheria Ndogo mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kuhakikisha sheria zote zilizopitiwa na Kamati Ndogo na zikaonekana zina dosari na hasa zile zinazokinzana na Sheria Mama yaani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wafanye marekebisho hayo haraka sana wawasilishe kwa Waheshimiwa Mawaziri ili sheria hizo ziweze kurudi kenye Kamati ya Sheria Ndogo zikiwa zimeondoa tatizo hilo la ukinzani kati ya Sheria Ndogo, Sheria Mama na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Sheria Mama yenyewe. (makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niwaombe sana wajitahidi kuondoa tatizo hilo la ukinzani wa Sheria Ndogo na Sheria ya Msingi ambayo imeruhusu uwepo wa hiyo Sheria Ndogo yenyewe, kwa hiyo mimi naomba nichukue hilo agizo na niseme hapa na mimi nitakwenda kufatilia Waheshimiwa Mawaziri wenzangu tuko hapa Mawaziri wote tutakwenda kufatilia kwenye sekta zetu kuangalia tatizo hilo linaondoka. Pia liko tatizo hili la uandishi bora wa sheria kwa kutumia vifungu vya Sheria Mama na maudhui yake ambavyo vinakwenda kujiwakilisha kwenye tafsiri ya Sheria Ndogo, kwa hiyo jambo hilo pia tumelichukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana tunapokea huo muktadha uliooneshwa mbele ya Bunge lako Tukufu ni namna gani Sheria Ndogo imetungwa ambayo haiakisi uhalisia wake wa kutumika nchini, lakini inavunja pia matakwa ya kikatiba ya usawa wa binadamu kwa kubagua makundi ya watu, kwa hiyo jambo hilo kwa kweli siyo jambo jema tutarudi tutaona ndani ya sheria hizo zilizorudishwa na Kamati Ndogo kuona namna gani tunafanya. Tutaendelea kushughulikia na niendelee kuwakumbusha wale Waandishi wetu wa Sheria ambao sheria zao zimerudishwa kwa sababu majedwali yanatofautiana na Sheria Ndogo na Sheria Mama, jambo hilo pia tutakwenda huko kulifanyia kazi ili kuhakikisha linafanyiwa marejeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa michango ya Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa Pindi Chana alitaka kujua magazeti ya Serikali kama yanapatikana na kama yanapatikana yanapatikana wapi. Huko nyuma Magazeti ya Serikali yalikuwa yanauzwa shilingi 1,000 kwa nakala moja, Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu ya Sita, imeamua tufanye marekebisho makubwa katika mfumo mzima wa upatikanaji wa Magazeti ya Serikali. Jambo la kwanza ambalo tumelifanya Ofisi ya Waziri Mkuu imekwisha kutoa maelekezo, magazeti haya sasa yatakuwa yanapatikana bure nchi nzima ya Tanzania bila ya kulipiwa, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la Pili Mheshimiwa Pindi Chana ameeleza jambo la msingi sana, haya magazeti tunao vijana sasa hivi wasomi mikopo hii ya elimu bure wasomi wetu wapo wengi huko kwenye maeneo yetu, wangeweza kuyapata na kuyatafsiri na kuwasaidia wananchi kulelewa magazeti ya Serikali yanasema nini. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kupitia Mheshimiwa Pindi Chana aliyetoa hoja hapa, sasa hivi kuanzia tarehe Mosi Mwezi Novemba, magazeti haya yote ya Serikali yanapatikana kwenye website ya ofisi ya Waziri Mkuu na website ya ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwa hiyo, yanapatikana huko bure hawa vijana wetu wasomi wanaweza kuyapata huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wako wananchi wengine hawawezi kufikia kwenye hayo maeneo ambayo wanaweza kuyapata kwenye website, tumeagiza mamlaka zetu kwenye Serikali za Mitaa wanao uwezo pia wa ku download hayo magazeti na kuyaweka kwenye ofisi zao, kwa hiyo sasa hivi magazeti haya yatakuwa yanapatikana na kigezo cha kuuzwa haya magazeti kwa sasa hivi hakipo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu ninaomba niwashukuru sana Wabunge na niendelee kutoa commitment yetu kama Serikali, kwanza Mawaziri wote mimi na wenzangu pale tutakapohitajika mbele ya Kamati ya Sheria Ndogo, tutakuja kupokea na kutoa maelezo katika kila sheria ambayo Sheria Ndogo wanataka tuje tuitolee maelezo. Pili tutakwenda kusimamia kuhakikisha sheria hizo zinafanyiwa mabadiliko zile ambazo zilikuwa zina matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nikuombe, Kamati ya Sheria Ndogo itusaidie wanapopitia Sheria Ndogo zile sekta ambazo zimeonesha kufanya vizuri katika utunzi wa Sheria Ndogo tungeomba kwenye ripoti ya Mheshimiwa wa Kamati sekta hizo basi na zenyewe zingekuwa zinatajwa ili tujue akina nani angalau wameweze sasa kubadilika na kufanya vizuri katika utungaji wa Sheria Ndogo, ambazo zinakidhi maudhui na mawanda ya uwepo wa Sheria Ndogo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikia na ofisi ya AG basi tutayatekeleza hayo yote kwa ustawi wa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)