Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kuweza kusimama na kuchangia. Pia naungana na wenzangu wote kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali yake kwa jinsi ambavyo anafanya kazi kwa umahiri mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakushukuru wewe kwa kuniruhusu kuchangia mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi wa mpango huu na bajeti hii ya mpango wa maendeleo wa mwaka huu 2022/2023 ambao ni mpango wa pili katika Mpango wa miaka mitano wa 2021 mpaka 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina sababu zote za kumpongeza pia Waziri wetu wa Mpango na Fedha na timu yake yote; na vile vile nampongeza Mwenyekiti wa Kamati kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye mapendekezo ya Mpango, eneo la vipaumbele vya Mpango. Kwenye eneo hili kuna mambo mengi sana, lakini mimi naomba nichangie kipengele cha kuchochea uchumi shindani na shirikishi. Hapa yapo mambo mengi yamezungumzwa, mazuri sana. Kuna suala zima la mapinduzi ya TEHAMA, tunawapongeza Serikali imewezesha kabisa kuanzisha mfumo wa Taifa wa anuani za makazi, pilot study ikiwa Mwanza, lakini mimi nitajikita kwenye suala zima la kuimarisha miundombinu na mifumo ya kitaasisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna suala zima la kuboresha mifumo ya kiutawala na Menejiment ya Utumishi wa Umma na Mifumo ya Utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi. Ukiangalia kwenye mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi, inaonekana kwamba kipaumbele cha kugharamiwa itakuwa ni masuala mazima ya miradi ya maendeleo, sensa ya watu, mishahara, deni la Serikali na huduma za jamii, yaani maji afya na elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, kwa sababu Serikali sasa imekuja na jambo zuri sana, imekuja na suala zima la mfumo wa kuwezesha mifumo kuweza kubadilishana taarifa. Hili ni jambo kubwa limeanzishwa, labda kama watu wengine hawafahamu. Huu mfumo utawezesha mifumo yote kuingiliana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Serikali ishafanya pilot study na mifumo mengine, kama mifumo mbalimbali ya taasisi mbalimbali kama NIDA, BRELA, NHIF, TAMISEMI yenyewe, Ofisi ya Ajira, Hazina kwenye payroll, kote sasa hivi imefanya pilot study.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazungumzia hilo? Kuna suala zima la kuhusisha mifumo hii ili kusaidia utumishi na wananchi. Kwa nini nasema hivyo? Serikali sasa hivi imeanzisha mfumo wake wenyewe wa taarifa za utumishi na mishahara. Zamani tulikuwa tunatumia Lawson ya wageni, sasa hivi tuna mfumo unaitwa Human Capital Management Information System. Kwa hiyo, Serikali ina mfumo wake wenyewe. Kupitia huu mfumo, kuna taarifa zote za watumishi. Kwa hiyo sasa, mfumo huu unaingiliana na mfumo huu mkubwa ambao umeanzishwa ambao utakuwa unawezesha mifumo yote kubadilishana taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauzungumzia kwa sababu gani? Ni kwa sababu mfumo huu utasaidia sasa, kwa mfano mtumishi anatarajiwa kustaafu mwakani, kwenye taarifa zake kwenye mfumo zinaonekana. Kwa hiyo, moja kwa moja mfumo utapeleka kwenye mfumo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao wameshaunganisha. Kwa hiyo, moja kwa moja mtumishi atakuwa hana shida tena kuanza kutafuta documents.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyowahi kusema, mtu kaajiriwa Kigoma kaja kustaafu Kibaha; kwa hiyo, sasa hivi huu mfumo utakuwa unarahisisha kwani taarifa zote ziko pale. Kwa hiyo, kama anataka information kutoka NIDA, inakuja kwenye ule mfumo ambao unawezesha mifumo ya kuwasiliana; kama inatoka kwenye NHIF, unakuja pale. Kwa hiyo, mtumishi sasa atakuwa hana shida tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiishi hapo tu. Huu mfumo unaendelea, kuna suala zima limeanzishwa linaitwa e- mfejesho. Nazungumzia suala la Serikali kuhudumia wananchi kupitia hii mifumo. Sasa hivi huu mfumo ulioanzishwa na umeanza kufanya kazi, unamwezesha mwananchi wa kawaida kuleta malalamiko yake, mapendekezo, pongezi na ushauri kupitia simu ya kawaida tu, massage au kupitia internet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukasema kuna tatizo la TEHAMA, lakini ngoja nikwambie; naipongeza Serikali chini ya Mheshimiwa Mama Samia sina wasiwasi wa speed yao ya kuongeza mifumo ya mawasiliano. Kwa nini nasema hivyo? Mpaka sasa hivi tumeona katika mwaka huu wa Mpango unaoishia, kumeweza kufungwa mkonga wa Taifa wenye kilomita 409, utaunganisha kutoka Msumbiji mpaka Mtwara; na pia mkongo mwingine ambao umekamilishwa ni wa kutoka Namanga mpaka Arusha. Hii inaonyesha jinsi Serikali ina dhamira kabisa ya kuhakikisha mawasiliano yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la mwananchi wa kawaida kuwasiliana na Serikali au kupitia internet, baada ya muda kwa speed ninayoiona kwa ufanyakazi wa Mheshimiwa Mama Samia na Serikali yake, tutakuwa hatuna shaka. Kwa nini nazungumzia suala hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali au bajeti inayokuja iseme suala la kuwezesha huu mfumo. Ni mfumo muhimu sana ambao utaleta harmony kule chini kwa watumishi wetu. Kwa sababu kama mfumo utaweza kuwasiliana na mifumo ya hifadhi ya jamii; sasa hivi naishukuru Serikali kusema kweli, wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Serikali sasa hivi imeweza kulipa mafao shilingi trilioni 1.5, imelipa pension shilingi bilioni 449 mpaka sasa; na mpaka sasa hivi Serikali imeanza mchakato wa kuhakikisha kwamba unalipa Hati Fungani maalum zisizo taslimu kiasi cha shilingi trilion 2.1. Hata kama haijalipa zote, lakini unaona nia njema ya kuendelea kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa mama Jenista hapa anapambana kila siku ya vikao vya wafanyakazi pamoja na taasisi tusimvunje moyo.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba, nia ya Serikali ni njema...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Alice pokea taarifa.

T A A R I F A

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja iliyozungumzwa hapa mapema ambayo inajibiwa, iliyozungumzwa Mheshimiwa Bulaya, inayojibiwa na mtu ambaye hatakiwi kujibu, ni hivi, kwa mujibu wa hesabu jumuifu za Taifa, kama ambavyo imekuwa reported na CAG kwenye report iliyotolewa Machi mwaka huu, madeni ya mifuko kiujumla wake, kama inavyokuwa reported 2017/2018 ni shilingi trilion 19. Kwa hiyo, hoja hapa ni kwamba, kama umechukua fedha za mifuko shilingi trilioni 19, unakuja kwenye Mpango unatuambia shilingi trilioni mbili, tena inahusu pre- 1999 ambapo kwenye pre-1999 mlikuwa mnadaiwa shilingi trilioni saba. (Makofi)

Mheshimiwa Menyekiti, kwa mambo haya, tusifanyie mzaha. Imefika kipindi sasa mifuko inabidi makusanyo yao kwa mwezi ndiyo wanalazimika kulipa pension na hayatoshi, inabidi wakatafute kwingine. Kwa hiyo, hakuna mtu mwenye nia mbaya, hakuna mtu ambaye hatambui, kwa sababu tunasema tunatambua hicho kidogo kilichofanyika, lakini kuna mzigo nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampa taarifa Mheshimiwa Mbunge ili aweze kuipokea tu kiroho safi. Hapa hatutafurani mchawi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Taarifa hiyo Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage unaipokea?

DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii siipokei kwa sababu mimi nipo katika ku-support na kuona nguvu ya Serikali inayofanyika kutatua whether ni shilingi trilioni 20 au shilingi trilioni 30, lakini nia thabiti ya Serikali tunaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya.

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Ester Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa anayezungumza, kwanza hakuna nia njema yoyote ya Serikali hapa. Hiyo shilingi trilioni mbili ya non cash bond kwenye shilingi trilioni saba, huu ni mwaka wa 22, tangu mwaka 1999. Hakuna nia nzuri ya Serikali. Serikali yenyewe haijapeleka michango, inadaiwa deni sugu shilingi bilioni 171. (Makofi)

MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage unaipokea?

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Naomba niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali inapokuja na Mpango huu ioneshe nia thabiti na kwa mapema sana kuhakikisha kwamba ina-support mfumo huu... (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Alice Kaijage pokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nchi.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuungana na Mheshimiwa Mbunge anayechangia kwamba nia njema ya Serikali inaonekana kwa sababu, kama nia njema ya Serikali haingekuwepo, hatungefanya utathmini wa hiyo mifuko kuangalia sustainability yake; lakini kama nia njema ya Serikali ingekuwa haionekani, hatungehimiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii, kazi ya mifuko hiyo kwa mujibu wa sheria ni kuandikisha wananchama, kukusanya michango, kufanya uwekezaji na kulipa mafao ya wananchama. Kwa hiyo, ili haya mambo yote yatimie, ndiyo maana Serikali kila jambo linalotokea ambalo ni hatarishi, linaloweza kuizamisha sekta, Serikali imekuwa ikisimama imara kufanya marekebisho na kuhakikisha kwamba sekta inaendelea kuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli nia ya Serikali ipo. Kila tatizo ni lazima tupambane nalo ili kuweka ustawi wa sekta kwa ujumla wake. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt Alice Kaijage, unapokea hiyo taarifa.

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili taarifa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niseme kwamba Mpango utakapofika, bajeti ioneshe nia njema na kwa haraka ku-support mfumo huu ambao utawezesha mifumo yote kuwasiliana. Utarahisisha wafanyakazi kuhudumiwa na Watanzania kwa ujumla. Tumeona Mheshimiwa Mheshimiwa Waziri wa Utumishi ameanzisha ile “Sema na Waziri wa Utumishi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe nimeshawasiliana kwa simu, inawezekana. Kwa hiyo, Watanzania wataweza kuwasiliana na matatizo yao yatakuwa solved haraka na pia ina uwezo wa ku-counter check kwamba aliyeomba swali lake au hoja yake imejibiwa, anaona. Kwa hiyo, huyo ambaye hajajibu kama ni mtumishi mtendaji anawajibishwa. Kwa hiyo, ni jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba bajeti itakapokuja ihakikishe kwamba imechangia au imewezesha mfumo huu mkubwa ambao utawezesha mifumo yote kubadilishana taarifa, uko vizuri na umeimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)