Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mimi pia niungane na wenzangu kumshukuru sana Mheshimiwa Mama yetu Mpendwa Samia Hassan Suluhu, kwa hizi fedha ambazo kwa kweli zimekuja kukomboa majengo yetu katika Majimbo yetu. Mimi binafsi nilikuwa na majengo zaidi ya 150 kati ya miaka sita au miaka saba ilifika mahali sijui nifanye nini. Lakini sasa hivi kwa kweli naishukuru sana Serikali chini ya Mheshimiwa Mama Samia, tunakwenda kumaliza matatizo haya ya maboma yetu vizuri na watoto watakwenda kusoma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia sana Mheshimiwa Kigwangalla na Mheshimiwa Abbas Tarimba, suala zima hapa ukitazama kwa upana wake matatizo yote haya ili kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji katika mpango huu, ninashauri sana blue print ifanyiwe kazi. Blue print leo inaongelewa zaidi ya miaka mitatu, mambo yote ambayo yapo kwenye blue print yakifanyiwa kazi, wawekezaji siyo tu wa nje hata wa ndani watapitia humo humo na wataweza kuwekeza vizuri na kuweza kurudi kwenye ile hali ambayo wanaitaka wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongelea hapa Mheshimiwa Kigwangalla katika suala hili la Covid-19 limeathiri sana uwekezaji, biashara na kadhalika. Ukija kwenye hii blue print ni mambo mengi mno ambayo ukiipiga overall, kwa ujumla wake na nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha itizame hii. Leo watu wanatoa viwanda vyao hapa wanapelekea Uganda kuna watu wanapeleka Uganda ili azalishe a-export bidhaa tena Tanzania au Congo! Yote hiyo moja katika sababu kubwa sana bado sisi hatupo vizuri sana ku-refund VAT on export product. Tunauza bidhaa nje lakini ku-refund zile VAT tunachelewa mno kuliko Uganda na Rwanda wanavyofanya. Leo Uganda na Rwanda wanafanya vizuri sana kwenye suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Rwanda wanapata wawekezaji wengi siyo kwa sababu ya population waliyokuwa nayo Rwanda. Rwanda wana population ndogo mno lakini uwekezaji unaofanyika katika nchi ya Rwanda wana-target nchi kama ya Congo, wana-target nchi za jirani na hata juzi kuna malori yamekwenda kupakia hivi vifaa tiba tu Rwanda wanakuja kuleta Tanzania, hivi ni kweli? Yote haya ni kwa sababu ya blue print hatuifanyii kazi haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la muhimu sana siyo la kufanyia mzaha tu hivi. Pitia hii Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe mwenyewe na Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri Mkuu uko hapa, angalieni namna ya kufanya yale ambayo hayana madhara kwenye nchi, toeni watu waje wafanye kazi wawekeze mambo yaende na nchi iweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu uwekezaji kwenye viwanda. Ni jambo jema sana kupata wawekezaji kutoka ndani ya nchi ni zuri tu. Lakini ni hatari sana kama hatutakuwa na mpango maalum wa kuwawezesha watanzania wakaingia moja kwa moja kwenye uwekezaji hasa wazalishaji wa viwanda. Itaweza kufika mahali huko mbele ya safari mkawa na wawekezaji wageni zaidi ya asilimia 80, halafu Watanzania wakawa kama wasindikizaji asilimia 10 au asilimia 15 tu, by then huko wakija kuungana tu wanaweza wakaiyumbisha Serikali itakayokuwepo huko mbele ya safari. Kwa hiyo, ni jambo la muhimu sasa sana tena, Serikali ione namna ya kufanya kuwawezesha watanzania waliopo katika biashara na watakaotaka kufanya kazi hiyo ni namna bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama Benki ya Afrika ya Kusini (South African Bank) mtu anakwenda na proposal yake, proposal yake kama ni nzuri wameipenda na haikukamilika, wanaibeba ile proposal wanaifanyia kazi wanakuchukua wewe mwenyewe kuna wataalam pale mpaka wanahakikisha ile proposal imekaa vizuri na fedha wanakupa na kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hii tusipofanya hivyo, hivi ukitenga hizi Shilingi Bilioni 500 ukapeleka kwenye hizi Developments Bank kama TIB ukasema sasa Watanzania waende pale, mkapunguza riba hata asilimia 10. Fedha kama ni za Serikali wana haja gani wao Benki kutoza asilimia 18 wakati fedha ni za Serikali. Malengo makubwa ni kuwawezesha Watanzania wawe na viwanda wengi waingie kwenye ushindani huo huo ambao wawekezaji wa nje wanatoka kuja kuwekeza ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo mangapi tunayahitaji na unaweza ukaweka strategy tu kwamba, tunatoa hizi fedha katika Benki zetu za Maendeleo lakini tunataka wawekezaji wa aina hii. Wawekezaji wa viwanda vya pamba, wawekezaji wa mafuta, uwekezaji ambao una manufaa kwa nchi na kwenda kujibu masuala majibu ya masoko ya kilimo ambayo wakulima wanazalisha. Kwa mfano, katika Kanda ya Ziwa zao la pamba linaajiri zaidi watu milioni 20 lakini kuna kiwanda gani Shinyanga? Hakuna viwanda vya pamba Shinyanga, hakuna kiwanda cha pamba labda Mwanza. Kuna kiwanda cha Urafiki hapa kimekufa tu, kiwanda cha Urafiki kwa historia yake ni ushirika baina ya Tanzania na China, lakini tunashindwaje kwenda kuongea na Serikali ya China kuwaomba tu bwana hiki kiwanda, naomba mkiache tupeni sisi kirudi kwenye mkono wa Serikali mkitangaze ili watu waje wawekeze.

Mheshimiwa Spika, leo pale kiwanda cha Urafiki imekuwa magofu, yule Mchina anakodisha kodisha tu maduka yale imekuwa ukiingia pale mpaka roho inakuuma, kiwanda kiko vizuri mno yaani pale lakini kimekaa tu. Hatuoni strategy, hatuoni Serikali kufanya intervention kuongea na Serikali ya China watuachie ili tuitangaze aje mwekezaji mkubwa pale na ikiwezekana aje Mtanzania afanye kazi pale. Kwa hiyo ni suala tu… (Makofi)

MWENYEKITI: Pokea taarifa Mheshimiwa Ahmed Salum.

T A A R I F A

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa kwanza tu kuweka sawa maneno nafikiri alipokuwa anasema viwanda vya pamba Shinyanga, Mwanza kwamba havipo, vipo. Hata mimi mwenyewe tu nimpe taarifa ni Mwekezaji kwenye sekta ya pamba na nina kiwanda cha pamba kipo Mwanza. Tatizo tulilonalo siyo kukosekana kwa viwanda vya pamba, tatizo tulilonalo ni kwenye kilimo. Kulizuka mjadala mzito sana hapa jana kuhusu kilimo ni kweli shida tuliyonayo hatuna uwekezaji wa kutosha kwenye kilimo kwa sababu, viwanda vya pamba vyote vilivyopo hapa nchini vinagombania raw material, vinagombania pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kwamba kuna shida ya pamba na kuhusu kiwanda anachokizungumzia cha textile, changamoto kubwa hapa kwenye nchi yetu ukitaka kufilisika wekeza kwenye kiwanda. Changamoto kubwa umeme, kodi, utitiri wa tozo na involvement ya Serikali kwenye kila hatua ya uwekezaji wako. Ndiyo maana hakuna mtu atawekeza kwenye kiwanda ambacho ni capital intensive kama cha textile hapa nchini na akafaidika. Kila atakayejaribu atafeli kwa sababu, riba za benki ni kubwa na mahali pa kuuza finished goods za kutoka kwenye kiwanda chake ni padogo. (Makofi)

MWENYEKITI: Kwa kuwa unajua hilo kwa nini Mheshimiwa Kigwangalla wewe umewekeza? Mheshimiwa Ahmed Salum unapokea taarifa hiyo? (Kicheko)

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Mheshimiwa Kigwangalla namheshimu sana lakini tukisema viwanda vya pamba ni viwanda vya pamba. Kiwanda cha pamba kimoja cha India kinanunua pamba yote ya Tanzania. Viwanda tulivyokuwa navyo hapa Mheshimiwa Kigwangalla ni vya nyuzi tu na ginnery. Kiwanda kama kiwanda ina maana kuna kiwanda ginnery inaunganishwa nyuzi, inakuja inazalisha nguo, hicho ndicho kiwanda. Magari 500 kwa mpigo zikishusha zinaingia pale mashine zinachukua zile pamba zinachakata. Kiwanda kimoja ukitembelea India au China kimoja kinanunua pamba yote ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka viwanda vya aina hiyo ambayo vinakwenda kujibu masoko ya wakulima wa pamba, vinakwenda kujibu masoko ya walimaji labda korosho na kadhalika na kadhalika. Yaani unaweka viwanda 10 vya kimkakati ndani ya nchi hii, 10 tu vinatosha kubwa kiwanda kimoja labda Dola Milioni 50, hivyo ndiyo unaongelea viwanda, ambavyo vinakwenda kujibu masuala mazima na maslahi ya wakulima wetu watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo kuhusu Irrigation (skimu ya umwagiliaji) hapa wewe mwenyewe umesema na watu wote wanajua baada ya muda siyo mrefu, au tuseme sijui mwaka huu sijui mwakani watu wa hali ya hewa wanasema kutakuwa kuna shida kubwa sana ya hali ya hewa. Njaa inaweza ikatokea jua kali sana hakuna, lakini majibu makubwa hapa ni kwenye skimu ya umwagiliaji tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika Jimbo la Msolwa kwa mfano na hii uchukue kama mpango Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wenzako, tukijikita sana kwenye kilimo cha umwagiliaji, mimi nina skimu za umwagiliaji saba lakini nimshukuru hata Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara yote ya Kilimo. Wamepita pale kwenye skimu moja ya umwagiliaji pale Nyida wamechukua na ninaamini kabisa katika mpango huu na fedha wa mwaka huu, Mheshimiwa Bashe alikuja Naibu Waziri namshukuru sana amejitahidi.

Mheshimiwa Mwenyikiti, imagine tukiwa na mpango mzima wa skimu ya umwagiliaji ndani ya Jimbo la Solwa na maeneo yote yenye advantage kubwa ya kilimo, maana yake nini, tunaweza tukalima hata kwenye wakati ambapo msimu siyo mzuri jua kali wewe pale skimu ya umwagiliaji ipo, bwawa lipo, mnafungulia watu wanalima. Angalau tunaweza tukawa na wakulima wanaweza wakalima kwa wakati wowote ule bila kujali kuna jua ama mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende kwenye wakati huo na kwenye eneo hili la skimu ya umwagiliaji ndiyo tunakwenda kuwasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)