Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru sana na mimi nipate nafasi ya kuchangia katika Mapendekezo haya ya mpango ambayo yameletwa na mwananchi Mheshimiwa Mwigulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipende kuunga mkono hatua iliyofikiwa hadi sasa naunga mkono mapendekezo haya. Vilevile niipongeze Kamati ya Bajeti tulifanya kazi nzuri sana ambayo hata Waheshimiwa Wabunge humu wameikubali na kwa hali hiyo ningeomba Mheshimiwa Waziri ayachukulie kwa uzito stahiki kabisa mapendekezo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitazungumzia katika vile vipaumbele na ningeanza na maendeleo ya watu. Kwenye Jimbo langu la Kinondoni sisi hatulimi, hatuna bahari hatuvui, sisi ni watu wenye shughuli ndogo ndogo na tunawamachinga wengi sana na mimi sitaki nizungumzie eneo la wamachinga kama lilivyozungumziwa ile timua timua, upangaji, hapana mimi nakubaliana na Serikali hatua walizochukua. Nataka niliangalie eneo hili hasa pale ninapolinganisha na mpango kwamba mpango wenyewe huu haujabainisha hali ya umaskini kiwazi kabisa na jinsi gani mpango unakwenda kuhangaika na taratibu za kuondoa umaskini, hii inaunganisha na wamachinga kwa sababu hili kundi limejitokeza miongoni mwetu na ni kundi ambalo yawezekana kabisa na naamini Serikali haijawahi kufanya utafiti kulijua kundi la wamachinga lina nguvu kiasi gani katika uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana tunawaona tu barabarani wakitembea ama wakijenga mabanda yale ya plastiki, lakini nataka nikwambie kwamba hawa watu kwanza wamewaondolea mzigo Serikali ya kuwatafutia kazi ni watu ambao wameamua kujiajiri wao wenyewe, lakini kama itafanyika tafiti ili kuonekana kwamba hawa wamachinga ni kwa jinsi gani wana-support baadhi ya viwanda vidogo vidogo nchini, baadhi ya wakulima wanaouza matikiti utakuta kwamba sasa hivi biashara imeshuka kidogo kwa sababu hawajakaa vizuri zaidi maana yake nini maana yake wanamkono katika uchumi, wana mkono katika biashara katika Taifa letu kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri mpango huu ujaribu kuunda utaratibu wa kwenda kufanya utafiti wa kina very independent ili kuliangalia hili kundi hili la wamachinga ni kundi la aina gani lina nguvu kiasi gani katika uchumi ili kama ikiwezekana waliingize katika utaratibu wa kulipia hata kodi wajulikane wanafanya shughuli gani na wapo wapi na akina nani ili nao waweze kuchangia katika Pato la Taifa la nchi yetu, lakini vilevile katika kodi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nizungumzie ukurasa 25 na 26 za Mheshimiwa Waziri wakati alivyokuwa akitoa hotuba yake juu ya kuwasilisha kwa mapendekezo haya na hii inagusa vipaumbele vifuatavyo: -

Kuchochea uchumi shindani, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani, utoaji huduma na kukuza biashara na uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote haya ukiyaangalia yanagusa mwenendo wa kibiashara na hasa private sector na kwa kuwa private sector ni tegemeo kubwa sana katika kodi za Taifa hili kiasi kwamba zaidi ya trilioni 22 zinatarajiwa kutoka kwao. Kwa hali hii nilikuwa naangalia ni kwa jinsi gani basi hivi vipaumbele vitatu vinaweza vikaleta mafanikio bila ya kuangalia ni kwa jinsi gani private sector inakwenda kusaidiwa. Hebu tuangalie nijaribu kukumbusha huko nyuma kulikuwa na kitu kinaitwa road map for improvement of business and investment climate baadaye ikaja big results now sasa tuna blue print.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zote hizi ni documents ambazo zilikuwa zinajaribu kutatua na kuleta hali bora ya uendeshaji wa biashara katika Taifa hili. Nimeangalia katika huu mpango sijaona vizuri ni kwa kiasi gani blue print imefyonzwa katika Mpango huu sijaiona yaani ikaja wazi wazi kabisa, kwa sababu blue print yenyewe ni majibu ya matatizo tuliyonayo katika kuifanya private sector ikawa vibrant na ikaendelea kuchangia kiasi kikubwa, trilioni 22, kwa Tanzania ya leo ilivyo ni fedha ndogo mimi ninaamini kabisa, laiti kama tungeshika certain buttons tukaminya vitufe ambayo pengine hatuvijui au tunavijua kupitia kwenye blue print utakuta kwamba uchumi wa Tanzania utafunguka hasa katika kipindi sasa Tanzania tumejenga imani huko nje, tumejenga imani ndani, kwamba sasa Tanzania unaweza ukafanya biashara vizuri. Ingawa Tanzania kufanya biashara ni kugumu kidogo kwa sababu hata kwenye index ile ya easier of doing business bado hatujafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba mpango huu uje na hatua za kutunasua kule kufanya vibaya katika ufanyaji wa biashara tuondoke katika ile nafasi ya 141, tupande juu ili tuweze kuwavutia watu wengi sana. Kutokana ninaomba mpango uje kiwaziwazi uonyeshe ni kwa jinsi gani tutakwenda kuondoa urasimu wa ufanyaji na mifumo ya usimamizi wa biashara katika nchi yetu, regulator reforms lazima zifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tusaidie Mpango uweze kuja wazi wazi utuondolee gharama nzito za kufanya biashara, leo hii ukifanya biashara regulators walio wengi watakufuata, wewe ukisoma ile sheria ya OSHA peke yake kuna kodi ya kucheka, kuna kodi ya kuchukia yaani ni hatari ni hatari kabisa, ukitoka hapo ukienda kwenye fire nao wana mambo yao yaani ni balaa balaa, hebu tufanye ufanyaji wa biashara katika nchi hii usiwe na gharama kubwa ili tuweze kuwavutia watu wetu wengi wafanye biashara, Watanzania na hata wale wa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la reduction...

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Waziri wa Nchi.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamheshimu sana Kaka yangu Tarimba Mheshimiwa Mbunge, lakini naomba tu tuwe realistic katika sheria zote ambazo zimetungwa na sheria hii, hamna tozo yoyote iliyowekwa na Serikali ambayo inamtoza mtu kwa kucheka, inamtoza mtu kwa kukasirika ama kuchukia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tukiacha hivi records zetu zitakuwa zimerekodi kitu ambacho hakina uhalisia kwa hiyo nilikuwa naomba nimpe taarifa kodi hizo ndani ya Serikali hatuna. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Unajua Yanga hawa wana shida sana, Mheshimiwa Tarimba unapokea taarifa. (Kicheko)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naipokea. Unajua alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Michezo, tulikuwa pamoja sina haja ya kushinda naye ni kweli hakuna kodi hiyo lakini inaonesha vile vikodi vidogo vidogo vya kuangalia ngoja kuna kodi ya vision sijui kufanya nini wanakupima macho, kama kampuni kama mtu, kuna vikodi vingi vingi hata Mheshimiwa akitaka nimkumbushe, nimuoneshe, nitamuonesha, lakini zipo kodi zinazoudhi ninachojaribu kusema ni kodi zinavyoudhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa nione huu mpango unakuja na ile dhana ya kuongeza confidence kwa investors wa ndani na wa nje, watu waliumiaumia hapa katikati hivyo, ningeomba mpango huu uweze ukasaidia.

Kwa hali hiyo, kwa kuwa nimeyazungumza yale ambayo nilikuwa nataka kuzungumza niseme naunga mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)