Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi walau nami nichangie kidogo kwenye mwongozo huu wa Mpango. Kwanza kabisa nichukue fursa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema ambaye amekuwa akitujalia afya njema na uhai na tumekuwa tukikutana hapa mara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Nina hakika kwamba Watanzania wote sasa wana matumaini makubwa, kazi inaendela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwongozo wa Mpango huu nataka nichangie katika sehemu mbili muhimu; sehemu ya kwanza ni kilimo na pia sehemu ya pili ni barabara. Kabla sijachangia nichukue fursa hii pia kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. Mwongozo wa Mpango unatupa sisi fursa ya kuwaeleza nini kiwepo kwenye Mpango unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa kwenye kilimo ni utekelezaji wa mipango ambayo ipo.

Nimejaribu kusoma Mpango wa mwaka 2019/2020 mambo mengi yameandikwa, lakini sisi wakulima kiukweli kabisa Serikali haijawekeza vya kutosha. Maneno haya yamesemwa na kila Mbunge, lakini mimi najaribu kuangalia tu kwa takwimu. Kwa mfano, ukiangalia kwenye zana za kilimo, mpaka sasa hivi sisi tuna asilimia 20. Hiyo asilimia 20 yenyewe ni kwenye maandalizi tu, yaani ile hatua ya kwanza kabisa ya kuchambua ardhi ndiyo tunatumia labda matrekta na zana nyingine, lakini kwa mantiki kamili ya kutumia zana za kilimo bado tupo chini ya asilimia nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira hayo, hakuna namna ambayo tunaweza tukaisaidia nchi hii ambayo asilimia kubwa ya Watanzania wapo kwenye sekta hii ya kilimo. Ni changamoto kubwa kweli kweli. Sasa hivi tunapoongea, ukifanya ziara kwenye maeneo yote ya Tanzania au hasa Majimboni, mbegu zenyewe hazijafika. Sasa unaanza kujiuliza maswali mengi sana, kwamba kwenye Mpango tumeweka tayari, maana yake hata tukija kusema sasa tuwekeze shilingi trilioni moja, bado changamoto hii itakuwepo pale pale. Kwa maana tumeweka kwenye Mpango, tumepitisha kwenye bajeti, lakini mbegu hiyo bado mpaka sasa hivi haijafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ambalo naliona, ni lazima tuhakikishe tumewekeza vya kutosha kwenye kilimo. Kama hatutafanya hivyo hakuna namna ambavyo tutakwepa watu wengi kuhamia mjini. Ukiangalia population kubwa ya Dar es Salaam ya vijana wengi wanaoitwa Wamachinga ni kwa sababu hakuna kazi kwenye kilimo hicho. Hatujawekeza vya kutosha kwenye kilimo. Tukiwekeza vya kutosha tutapunguza gharama hizo ambazo zimewekezwa kwa ajili ya Wamachinga; majengo yanayojengwa, fedha zile tungewekeza kwenye kilimo, vijana wale wasingekuwa na sababu ya kukimbilia mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu mimi naiona katika mwono huo. Mimi pia nalima, lakini najaribu kuangalia mazingira ya kilimo kile, anaweza akaja kijana akalima mwaka mmoja akaamua bora aende mjini akauze bidhaa mkononi kwa sababu ya mazingira yenyewe yalivyotengenezwa. Nataka niwaombe sana Wizara ya Fedha iangalie namna ambayo itatenga fedha za kutosha waingize kwenye kilimo. Tutaweka Mpango leo, lakini kama fedha hazitaenda huko nina hakika kabisa vijana wengi watakimbilia mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka pia niongelee kuhusu barabara. Tuna barabara yetu; halafu unaweza kujiuliza maswali mengi sana, kwamba tuna barabara ambayo inaunganisha mikoa minne. Mwenzangu Mheshimiwa Mtaturu alikuwa ameiongolea pale kwamba barabara inaunganisha mikoa minne, eti imetengewa kilometa 20 kati ya kilometa 420 na kitu. Sasa sijui wataalamu huwa wanachambua kwa kuangalia vigezo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia barabara hii, ndiyo barabara kubwa iliyobaki, lakini barabara hii ukiangalia faida, niliwahi kumwambia Waziri; hivi nyie mnavyoweka mipango na kujenga hizi barabara mnatumia vigezo gani? Unawezaje kuacha barabara inayounganisha mikoa minne, unaenda kujenga barabara ya kuunganisha wilaya na wilaya halafu umetenga kilometa 70?

Mimi nafikiri kama walivyoshauri Kamati ya Bajeti, wameandika maneno mazuri sana pale, kwamba tukajenge kwanza barabara zile ambazo tayari zipo kwenye mpango zimalizike then ndiyo tuingie kwenye barabara nyingine. Pengine hii itaweza kutibu lile tatizo ambalo wewe unaliona, kwamba wanakuja na Mpango, Wabunge wanasema, lakini mwisho wa siku hakuna ambacho kinafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha sana kwamba una barabara muhimu kuliko zote halafu hiyo ndiyo inatengewa fedha kidogo sana. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kama yupo hapa, Waziri wa Ujenzi wakati ujao, sisi tupo Wabunge wanane ambao tunaguswa na barabara hiyo; nataka nimwambie, ukileta tena kilometa 20 sisi hatutakuwepo tena hapa Bungeni. Kwa sababu ni barabara ambayo ukiangalia faida zake ni kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaenda kupanua Bandari ya Tanga, mizigo yote ambayo inatakiwa kwenda Rwanda na Burundi, lazima ipite kwenye barabara hiyo. Ni kwa namna gani unaenda kujenga barabara nyingine huko kilometa 70, kilometa 80 ya kiwango cha lami…

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa nimekuona.

T A A R I F A

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wasiofahamu, barabara inayozungumziwa hapa ni ya Handeni – Kibilashi – Kiteto – Kondoa – Singida kilometa 460. (Makofi)

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimeipokea taarifa bila wewe kuniuliza, lakini ni ukweli, najaribu kueleza namna ambavyo barabara ile inaweza kusaidia. Najaribu kuangalia, hivi barabara zinajengwa kama unaongeaongea Bungeni au ni Serikali? Ina maana kama haitakuwa Mbunge, barabara hiyo haitajengwa? Kuna vitu vingi vinachanganya sana, kwa namna ambavyo umuhimu wa hii barabara ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana kwamba nimesoma vizuri ushauri ambao umetolewa na Kamati ya Bajeti na ninaomba wauzingatie, wasituweke kwenye mtihani wa kuja kupambana na mipango yao waliyotupangia. Nashauri kama walivyoshauri Kamati ya Bajeti kwamba barabara zile ambazo zipo kwenye Mpango, ambazo zimepangwa muda mrefu sana, zijengwe zimalizwe ndiyo mlete tena mipango mingine ya kujenga barabara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)