Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Niende moja kwa moja kwenye kuchangia, mimi nitakwenda kwenye kilimo. Sasa kwenye Mpango, wenzetu wamesema kwamba wataimarisha mashamba makubwa yawe kitovu cha teknolojia kwa wakulima wadogo wadogo. Najiuliza haya mashamba makubwa makubwa yapo wapi, mangapi, halafu yapo wapi? Lakini nilifikiri katika Mpango, tunaongea hapa Mheshimiwa Nape amezungumza kuhusu kilimo na wewe mwenyewe umeongea. Hivi kwa nini tusiweke kwenye mpango sasa hivi, mashamba makubwa yaanzishwe na hawa vijana tunaosema hawana ajira nilizungumza, tuna vijana wengi hawana ajira Vyuo Vikuu hebu tuanze hilo kwa nini tunaogopa? Tufanye kama pilot hata katika mikoa miwili au mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya kuna hayo mabailiko ya hali ya hewa, kuna Covid, hivi wakati mwingine nawaza tutapata shida ya chakula na tungekuwa na mashamba haya makubwa je, si yangetusaidia. Kwa nini tusiwekeze huko tunaogopa nini? Iwe kwenye Mpango tuwasaidie hawa vijana, watafanya production wao wenyewe watafanya processing halafu baadaye mambo ya sales. Ni kiasi tu chakuwekeza kuwapa matrekta na pembejeo, hebu tuanze sasa kuwa hizo commercial farms tunazungumza lakini tunazo ngapi? Tunazo ngapi?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Thea huwezi kuwa na commercial farms kama huna mabwawa makubwa, ili pale mvua haijanyesha wewe una supplement kwa kumwagilia, mvua ikinyesha mnakwenda namna hiyo.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo unavyosema.

MWENYEKITI: Nakuunga mkono lakini, endelea tu.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Eheee! Mmmh!

MWENYEKITI: Taarifa, endelea nimekuona Mheshimiwa Tabasam.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba katika hili nataka kumwambia Mheshimiwa Mpango huu upo Misri, wenzetu wa Misri kwa kutumia maji haya haya yanayotoka katika Ziwa Victoria, kule kwao wamechimba bwawa, wanafunzi wanaotoka katika Vyuo Vikuu vya Kilimo wanakopeshwa kila kitu kwenda kufanya kazi hiyo. Nafikiri Tanzania na sisi tunaweza kwenda kujifunza kule tukaleta habari hiyo Tanzania.

MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa Ntara.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani naipokea sana, nafikiri wewe ni Dokta. Tufanye hivyo, nafiriki tusisubiri wakati mwingine tunasubiri tamko lakini hebu tujipange tuone kwamba kila Kanda au kila mkoa. Wakati tupo Kahama tuliwaomba Kahama kwa sababu wale wanadiriki, wanathubutu, hebu waanzishe hilo. Tutamaliza au kupunguza hizi kelele za ajira. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili niende kwenye elimu. Suala lililozungumzwa nyuma kwamba tuboreshe mitaala, mitaala yetu ya elimu haijakaa vizuri, tatizo ni moja kwenye Mpango sijaona sehemu wamesema watawekeza ili hawa watu wa TARI waweze kuboresha. Hawana fedha kabisa hivi watakaaje chini waanze kuboresha mitaala. Serikali iangalie ile mitaala ili iboreshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimeona kuna ujanzi wa Chuo VETA kikubwa Dodoma, sioni wivu lakini nilitegemea kutakuwa na mpango wa kuimarisha ile branch ya SUA iliyoko Tunduru. Hayo ni maneno tu, kule Tunduru wanasema kuna branch ya SUA, siku moja niliongea hapa Naibu Waziri wa Elimu ananiamba tutaongozana, mambo ya kuongozana siyataki, kwa nini tuongozane? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, SUA mmesema mmeanzisha branch Tunduru nilitegemea hapa angesema kwamba, tunaimarisha mpango wa SUA na nikuambie jambo moja wakiimarisha ile branch pale Tunduru itapanda baadaye kinaweza kikawa Chuo chenye program nyingi tu. Kuna korosho kule kwa hiyo, tutakuwa na program ya chemical engineering, tutakuwa na program ya mambo ya crops, tutakuwa na program ya fisheries inatoka kule Lake Nyasa. Lakini ile branch iko pale sijui ni jina tu hakuna kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mpango wahakikishe kwamba watu wa Ruvuma, watu wa Lindi na Mtwara kunakuwa na Chuo. Tunalalamika hapa kwenye Vyuo tukisema Kusini hakuna Vyuo tunaambiwa eti hivi Vyuo vilivyopo ni vya Kitaifa. Kama vya Kitaifa basi vijengwe kwenye Mkoa mmoja vyote vije Dodoma au vyote viende Dar es Salaam. Tunaomba kuwe na Chuo mtusaidie ile SUA pale Tunduru inyanyuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho. Nimeona kuna mpango kama alivyosema mwenzangu mmoja, huu mpango wa reli kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay nimeusikia toka enzi hizo nikiwa Mwalimu nafundisha nasikia mpango, enzi za Mtwara Corridor nilikuwa namsikia Marehemu Profesa Mbilinyi nimeusikia, nimeusikia, nimeusikia! Sasa hivi kule Ruvuma wanangoja wanasema na sisi tutaona treni? kwanza hawaijui! Nafikiri siku itakayopita watafikiri sijui ni bomu linapita sijui ni dudu gani? Sasa huo mpango uwe kweli waanze hata kwa kitu tuone tu wanafukua fukua matuta kule angalau, lakini isiwe mpango kwenye maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)