Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. CASATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami nianze mchango wangu kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais. Niliwahi kusema hapa wakati wa Bunge la Bajeti kwamba Mheshimiwa Rais kama Mkuu wa Nchi na Mkuu wa Dola, ndiye Diplomat namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ametendea haki ile kuwa Diplomat namba moja, kwanza ambavyo mmemwona anashiriki katika shughuli mbalimbali Kimataifa na matunda yake tumeyaona ikiwemo pamoja na huu mkopo ambao tumetoka kuzungumza na mchangiaji aliyepita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi kwa Mheshimiwa Rais kama Diplomat namba moja, nilikuwa napenda kutoa changamoto au wito kwa wataalamu wetu; kwa mfano nitanukuu hapa, wakati Mheshimiwa Rais akiwa kwenye Mkutano wa Mazingira kule Scotland, amesema kwamba tunapimwa kwa vitendo vyetu na siyo kwa ahadi kubwa kubwa. Mheshimiwa Rais alikuwa na uthubutu wa kuyaambia Mataifa makubwa ambayo yamekuwa yaki- pledge katika kuchangia masuala mazima ya madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi; na amesema, naomba kunukuu.

“Mabadiliko ya tabia nchi ni suala la dunia nzima na hivyo majawabu yake ni lazima yawe ya Kimataifa na hivyo tunatoa wito kwa nchi zilizoendelea ambazo ndiyo zinazoongoza kwa uchafuzi, zitekeleze kwa vitendo ahadi zao za kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa fedha za kutosha kutuwezesha sisi nchi za kipato cha chini kufanikisha malengo yetu kwenye michango ya Kitaifa ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa uendelevu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa nilikuwa napenda kushauri wataalam, kuna fedha ambazo pamoja na kuwa nchi zilizoendelea hazitoi kwa kiwango kinachotakiwa, lakini kuna fedha zinazotolewa katika mifuko mbalimbali, nitaitaja baadhi kama vile Climate Investment Funds, Green Climate Funds, Adaptation Fund na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mifuko hii ili uweze kupata zile fedha ambazo kwa namna moja au nyingine zitawezesha Taifa lako kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, zitawezesha nchi kama Tanzania, watu kama wa Iringa, watu kama wa Mufindi na Njombe ambao wanapanda miti kwa wingi na hivyo kusaidia dunia kupunguza hewa ya ukaa ili uweze ku-access zile funds, lazima kuna vigezo kama Taifa uwe umepitia na umefikia. Baadhi ya vigezo lazima uwe na taasisi ambazo zimekuwa accredited au zimepata ithibati ambapo ndani ya ule utaratibu utaeleza zile fedha utatumiaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Rais ameshafungua mlango. Kwa hiyo, pamoja na kwamba nchi hazijatoa fedha kwa kiwango kikubwa, lakini kile kiwango ambacho kipo kwa Taifa letu mpaka ninapozungumza sasa, ni taasisi mbili tu; ni NEMC na CRDB ambao wamekidhi hivyo vigezo, wanaweza ku-access hizo Fund. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Mpango kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira) tuwezeshe taasisi nyingi ziweze kujengewa uwezo. Sisi watu wa Mafinga na Mufindi ambao tunachangia kupunguza shida katika mabadiliko ya tabianchi tuweze ku-access zile funds ili kusudi ziweze kutusaidia katika kukabiliana na madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nchi kama Kenya, Rwanda na Morocco, wanapata mabilioni ya pesa kila mwaka, kwa sababu tu wameweza kukidhi vigezo ambalo ni jambo la kawaida. Hapa nitoe wito kwa wenzetu wa Vyuo Vikuu, Taasisi za Elimu ya Juu, hebu zitusaidie katika kuona zinaweza kujengeaje uwezo taasisi mbalimbali; za Serikali na za binafsi ili tuweze ku-access hizo funds kusudi siyo tu watu wa Mufindi, Mafinga, Iringa na Njombe wanufaike, lakini Taifa zima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ambalo napenda kushauri kwenye Mpango, tunatumia pesa nyingi sana kuagiza sukari na mafuta ya kula. Kwa mfano, katika mafuta ya kula, tunatumia karibu shilingi bilioni 500 kuagiza mafuta kula. Kwenye sukari vivyo hivyo; kila mwaka tunakuwa na uhaba wa sukari na sukari inapanda bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuwaandikia Mawaziri kadhaa kuhusiana na ushauri kwamba pamoja na ule mradi mkubwa wa Mkulazi, bado kama Taifa tuna maeneo ambayo tunaweza tukawekeza katika small scale industry na Taifa likajitosheleza kwa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala zima la mafuta ya kula, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, namwona kila mara anaenda Kigoma kwa ajili ya masuala mazima ya Mchikichi. Yaani kama Taifa, ninashauri sana Mpango kama ulivyosema katika kilimo, hebu tujielekeze katika kupunguza kutumia fedha za kigeni kuagiza bidhaa ambazo hapa hapa nchini tunaweza tukazizalisha ikiwemo sukari na mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 126 wa Mpango, umesema mambo mbalimbali ikiwemo kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuboresha uwezeshaji wananchi kiuchumi, kukuza sekta binafsi na mwisho wa yote ni kuchochea maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa napenda kuishauri Serikali na Mpango kwa ujumla, wakati tunatengeneza mazingira ya uwekezaji kuvutia wawekezaji, ninashauri pia wawekezaji hawa tunaowavutia katika kule kuwekeza kwao kuwe na mantiki na kusaidie kunyanyua maisha ya wananchi. Kwa nini nasema hivi? Ukija pale Mafinga tuna wawekezaji wengi sana kutoka China wamewekeza kwenye mazao ya misitu, lakini ile biashara namna wanavyofanya, pamoja na kuwa tunasema tupo kwenye soko huria, lakini soko huria ambalo haliwi regulated litakuwa soko holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninapozungumza, pamoja na Serikali ya Mkoa naya Wilaya kuwasaidia watu wanaouza magogo kwa Wachina, kuna kitu kinaitwa betting; yaani unaenda pale na gari lako, umepakia magogo, unamuuzia Mchina mwenye kiwanda, mnaanza kubishana. Anakwambia hii ni shilingi 700,000/=, wewe unamwambia hapana ni shilingi 900,000, laki saba na nusu, laki nane na nusu, inaitwa betting.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naishauri Serikali watusaidie kuweka bei elekezi ili wale watu wanaouza magogo kwa wale wawekezaji waweze kuuza kwa bei ambayo itarejesha gharama zao na pia watapata faida ili kwenye ule ukurasa wa 26 tunaposema kuchochea maendeleo ya watu, basi tuweze kuwa tumechochea maendeleo ya haya watu kesho waweze ku-afford huduma za afya, waweze ku-afford huduma za elimu na kadhilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, nimalizie na suala la mbolea. Mimi nilifanya ziara katika baadhi ya maeneo, mwananchi mmoja alinishika hivi ananitingisha, ananiuliza, nijibu Mbunge; niuze madebe mangapi nipate mfuko mmoja wa mbolea? Kwamba debe la mahindi ni shilingi 5,000/=; mfuko wa mbolea shilingi 100,000/=. Yaani auze madebe 20 apate mfuko mmoja wa mbolea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nami naungana na wewe na Mheshimiwa Nape, lazima Mpango ujielekeze kwenye suala zima la kilimo ambacho kinachangia pato la Taifa kwa asilimia 26.6; bidhaa zote zinazouzwa nje kilimo kinachangia asilimia 26; lakini zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wamejiajiri kwenye kilimo; lakini leo hii mfuko wa mbolea ni shilingi 100,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali na kwa Mpango kwa ujumla, pamoja na kujenga viwanda, lakini pawe na uwezekano wa kuweka ruzuku kwenye mbolea.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru na ninasema, Bwana asipoulinda Mji, waulindao wakesha bure. Mungu ailinde nchi yetu. (Makofi/Kicheko)