Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukutana leo na mimi nikapata kuwa mchangiaji wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono hotuba ya Kamati ya Bajeti wamechambua vizuri na kutoa ushauri mzuri sana kwa Serikali. Kwa hiyo pamoja na yote ambayo sisi Wabunge tutaendelea kushauri lakini Serikali itulie isome hotuba ya Kamati ya Bajeti kuna mambo mengi ambayo yatasaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba ya Bajeti ukurasa wa 27 wameeleza Serikali imekuwa ikileta vipaumbele vingi. Serikali imekuwa ikileta miradi mingi ya mikakati, lakini ni kama tu inatajwa kwenye mpango, inatajwa kwenye bajeti, lakini haifanyiwi kazi. Kwa mfano, kule kwetu Mikoa ya Kusini kuna ule mradi wa LNG kuna mradi wa Reli ya kutoka Mbamba Bay mpaka Mtwara kila siku inatajwa. Kuna mradi wa Makaa ya Mawe wa Liganga na Mchuchuma kila siku ile miradi imekuwa ikitajwa, lakini haifanyiwi kazi ama haitekelezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo mradi wa Makaa ya Mawe, huo mradi wa reli ungekuwa umetekelezwa leo hii tusingekaa humu ndani Wabunge wa Mikoa ya Kusini kulilia Bandari ya Mtwara haifanyi kazi vizuri, kwa sababu mizigo ingekuwa ina uwezo wa kusafirishwa vizuri kwa njia ya reli, Makaa ya Mawe kila siku yangekuwa yanaingia pale bandarini kwa uwingi wake maana yake meli zingekuwa zinafika na leo tusingekuwa tunahangaika kwamba makasha hakuna, meli hakuna, korosho badala ya kusafirishwa Bandari ya Mtwara ziende zikasafirishwe Bandari ya Dar es Salaam. Haya yote ni kwa sababu kuna miradi ambayo ingetekelezwa ingesaidia ku- boost Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapokuja kuhitimisha atuambie huu mradi wa Reli kutoka Mbamba Bay mpaka Mtwara unakwenda kutekelezwa ama hautekelezwi? Kama hautekelezwi basi auondoe kwenye mpango, siyo kila siku tunauona lakini haufanyiwi kazi. Pia aje atueleze mradi wa Makaa ya Mawe wa Liganga na Mchuchuma unakwenda kutekelezwa ama hautekelezwi kama hautekelezwi asifanye kazi ya kuandika kwenye mpango kila mwaka, mimi huyu leo nipo Bungeni mwaka sita tunauona, lakini haujawahi kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzetu wa Kamati ya Bajeti wameshauri kama anafikiri hawezi kutekeleza aandike vipaumbele vichache ambavyo vitatekelezeka akishamaliza basi ahamie kwingine si kila siku anaandika halafu hatekelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na bandari naomba mtuangalie watu wa Mikoa ya Kusini hususani Mtwara kwa jicho la huruma, kuhusu pembejeo za kilimo ya zao la korosho, unakumbuka kulikuwa na mjadala mkubwa hapa wa export levy na nini na nini, mwaka huu watu wamelima hivyo hivyo ingawa pembejeo zimechelewa korosho zimepatikana korosho tulitegemea zitasafiri kwa Bandari ya Mtwara, lakini pana changamoto haya zinaenda huko Dar es Salaam lakini tunaomba kwenye msimu ujao mpango huu uende ukatueleze unakwenda kuhakikisha vipi pembejeo za wakulima iwe wa korosho, iwe wa mahindi kwa sababu wenzetu huko Mikoa mingine nao pia wanalia mbolea imepanda bei na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ukaeleze unakwenda kujipanga kwa namna gani kuhakikisha wakulima wa Tanzania ambao ni wengi wanachangia Pato kubwa la Taifa ingawa wanafanyakazi katika mazingira magumu na hatarishi wanakwenda kuwawezesha namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu nyingine kuhusu madeni ya Wakandarasi. Ukisoma kwenye mpango, ukisoma hotuba mbalimbali unakuta kwamba nchi yetu hii inapoteza pesa nyingi sana kwa sababu ya kuchelewa kuwalipa Wakandarasi. Wakandarasi wanakuwa wamefanya kazi wamemaliza wamepeleka certificate kule, lakini Wizara ya Fedha inachelewa kutoa pesa. Inapochelewa kutoa pesa kinachotokea ni nini, kunakuwa na riba, kunakuwa na tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti ya CAG amekagua miradi saba tu, karibia Shilingi Bilioni 14 zinapotea kwa sababu ya Wizara ya Fedha kuchelewa kuwalipa Wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano tu, ujenzi huu wa reli ya kisasa umetoa riba na tozo kama hasara karibia Bilioni Mbili na point fedha hizi Wizara ya Fedha ingekuwa inalipa kwa wakati maana yake hizi fedha zingekwenda kufanya mambo mengine ya maendeleo. Kwa hiyo, katika huo mpango tunamuomba Mheshimiwa Waziri atueleze anakwenda kuhakikisha vipi certificate za Wakandarasi zikifika anawalipa kwa wakati na pia asizalishe madeni mengine. Wakandarasi waliowengi ni wafanyabiashara wadogo wadogo, wanakopa benki wakitegemea wafanyekazi warudishe zile pesa, usipowalipa kwa wakati unawakwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee mambo mawili ya mwisho, la kwanza sisi watu wa Kusini tuna Mto unaitwa Mto Ruvuma una maji safi na mengi kweli kweli, lakini nikikuambia jambo la kusikitisha katika Mikoa yetu ya Kusini hususani Mkoa wa Mtwara ndiyo Mikoa ambayo inaongoza kwa ukosefu wa maji kwa kiasi kikubwa. Huu mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma kuja Mkoa wa Mtwara umekuwa ukizungumzwa siku nyingi unaandikwa lakini hautekelezeki. Naomba kwenye Mpango aende akatueleze ana mkakati gani wa makusudi wa kuhakikisha mradi huu wa maji kuyatoa Mto Ruvuma kuleta katika Miji ya Mtwara, Mtwara Mjini, Nanyamba, Tandahimba na kwingine unakwenda kutekelezeka kwa namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ile barabara yetu kila siku tunaiongelea ya kutoka Mtwara Mjini inapita Tandahimba, Newala mpaka Masasi ya kilometa 210, wamejenga kilometa 50 tu hizo zingine wanakwenda kuzimaliza lini. Tunaomba mpango uje ueleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la mwisho kabisa, sasa hivi Serikali imekuwa ikikusanya mapato yake mengi kupitia mifumo, unapokwenda ardhi utapewa control number, unapokwenda TRA utapewa control number na kokote kule, lakini suala hili nimekuwa nikiliongea Serikali inapoteza mapato mengi kwa siku kwa sababu ya mifumo mibovu ukienda utaambiwa network ipo chini hatuwezi kupokea pesa, mwananchi anarudi na pesa yake. Mpango uje utueleze umejipanga vipi kwenda kuhakikisha wanaboresha hii mifumo ikiwezekana kuwe na utaratibu wa kukusanya off line mfumo ukirudi vizuri basi pesa iingie kwenye mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Huo ni mchango wangu kwa leo. (Makofi)