Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mungu kwa kunijalia kuchangia siku ya leo katika Wizara ya Afya. Namshukuru kwa nafasi ya kipekee Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya yeye na Serikali nzima, kwa kuonesha kwamba anaweza na kwa kuonesha kwamba sasa Tanzania mpya yenye matumaini inawezekana.
Meshimiwa Mwenyekiti, Mkoani kwangu Mara kuna matatizo makubwa sana ya vituo vya afya, ukizingatia kwamba Mkoa wa Mara umepakana na mipaka mingi ambayo wenzetu wa nchi za jirani pia wanategemea huduma za afya kutokana na Mkoa wetu wa Mara. Kwa mfano, Wilaya ya Tarime kwa sasa imegawanyika katika sehemu mbili; tuna Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya. Hospitali tuliyonayo ni moja tu, ambayo haikidhi mahitaji kutokana na wingi wa watu waliopo Wilayani hapo Tarime. Kutokana na hali halisi ya matatizo hayo ya hospitali, Mgodi wa Acacia uliopo Wilayani Tarime, ambao uko chini ya North Mara wameamua kutujengea Kituo cha Afya katika Kijiji cha Nyamwaga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Tarime, kaka yangu Mheshimiwa Luoga, alikaa nao chini wakafanya maongezi, pamoja na Halmashauri ya Tarime. Wakaongea wakakubaliana kwamba badala ya kutengeneza au kujenga Kituo cha Afya, wakakubaliana kwa majengo yale yale na kwa gharama zile zile, tuiombe Serikali ikubali majengo yale baadaye yawe Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa dada yangu Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla bahati nzuri mpo hapa, nawaomba watukubalie Wilaya ya Tarime, yale majengo yatakayojengwa na Kampuni ya Acacia yawe ni Hospitali ya Wilaya kwa sababu wamejitolea wao wenyewe. Kwa hiyo, pia yanakuwa yametusaidia sisi kupunguza gharama ambazo tungezipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya kipekee zaidi, kama mnakumbuka, naamini hata Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliopita wameiongelea sana Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kwangwa. Hospitali ya Kwangwa ilikuwepo hata kabla hatujazaliwa, tunasikia historia yake. Kama mnavyojua, Mkoa wa Mara kuna matatizo mengi sana, ukizingatia kule kwetu kulikuwa na mfumo dume ambao hadi sasa haujakwisha, kwa hiyo, kuna matukio mengi sana ambayo yanategemeana na Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma Hospitali ya Kwangwa, wanawake, watoto na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kwa ujumla wanapata shida sana. Tangu mwaka 2012, mkoa ulikuwa unaomba shilingi bilioni mbili na point, lakini hizo fedha zilikuwa hazifiki kama zilivyokuwa zinaombwa. Toka kipindi cha mwaka 2012, mwisho imekuwa 2013; na mwaka 2014, Serikali imejitahidi kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mara, wamejenga hospitali, imefikia ilipofikia, lakini mpaka sasa imekuwa kitendawili; na fedha ambayo imeshatoka ilikuwa ni sh. 3,334,967,000/= na fedha nyingine za kipindi hicho bado hazijatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu zaidi, wananchi wa Mkoa wa Mara, kwa kuiona Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina umuhimu, pamoja na kuwa baadhi ya Majimbo wamewachagua Wabunge wa Upinzani, lakini Rais wetu aliongoza kwa kura za kishindo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Rais aiangalie sasa hospitali ya Mkoa wa Mara ili sasa ifikie mwisho kwa sababu ni hospitali ambayo inaweza kutoa msaada mkubwa sana, lakini pia ikapunguza matatizo ya wananchi wa Mkoa wa Mara kutoka Mkoa wa Mara kwenda Mkoa wa Mwanza, wakati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza pia inazidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, wananchi wa Mkoa wa Mara wengi wao akinamama ndiyo wanaotunza familia zao na akinamama hao hawana vipato vya kutosha; wanakosa hata nauli ya kuwatoa kutoka Mkoa wa Mara kwenda Mwanza. Kwa nini hili suala Serikali isiliangalie kwa nafasi ya kipekee zaidi ili hospitali hiyo itengewe sasa kiwango cha kutosha ili kuisaidia japo ianze kufanya kazi, hata kama majengo mengine yatakuwa bado, basi yatamaliziwa baadaye, lakini ianze kazi, iitwe Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy, baada ya Bunge, kama inawezekana twende wote Wilayani Tarime, aende akaangalie yale majengo ambayo Acacia imeshakubali kujenga ili muipe hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kwa nafasi ya kipekee sana, kuna wanawake wenzetu ambao ni ma-nurse mishahara yao ni midogo sana, haitoshi. Mwaangalie na mwaongezee mishahara. Pia Wizara ya Afya kwa ujumla muiangalie bajeti yake iongezwe kwani bajeti iliyopo ni ndogo sana, haitoshi kukidhi mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi nyingine tena ya ziada, nasema MSD ni jipu kwa sababu, ni kweli kuna baadhi ya maeneo wanakosa pesa ya kuwalipa, lakini kwa mfano Wilayani Serengeti wametenga bajeti ya kuwalipa lakini wao madawa ndiyo hawana. Kwa hiyo, naomba kama inawezekana, urudishwe utaratibu wa zamani, twende tukanunue madawa au hospitali ziruhusiwe kununua madawa kwenye maduka makubwa ya wengine, ambapo madawa yanapatikana, kuliko wananchi wetu wanakufa wakati madawa hakuna MSD. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusiana na Bima ya Afya, wananchi wangu wa Mkoa wa Mara wanapata shida sana na wamekuwa mstari wa mbele kujiunga na Bima ya Afya. Katika mazingira ya kawaida, unapojiandikisha, kwa mfano umejiandikishia hapa hapa Bungeni, ukienda kituo kingine huwezi kutibiwa. Kwa hiyo, wananchi wangu wa Mkoa wa Mara wanapata shida. Mwanamke akijiandikishia Nyamongo mgodini au akijiandikishia Mtaa wa Mkendo, hawezi kwenda kutibiwa Mtaa wa Ilingo, kwa sababu Bima yake inaishia kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.