Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza kwa kuunga mkono hoja. Ningependa kumpongeza Mheshimwa Raisi kwa kupata billion 32 za kwenda kujenga upya soko la Kariakoo. Kimsingi soko lile linakwenda kutumiwa na wafanyabiashara ambao wanafanya kazi kwenye minyororo ya thamani ya sekta za uzalishaji kwa maana ya kilimo, mifugo na uvuvi. Hiyo inaendeleza azma ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ya kwamba tunaimarisha hizi sekta za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kunufaika na hizi sekta za uzalishaji, napenda kuishauri Serikali lazima tuwekeze kwenye mbegu kwa maana ya mbegu bora, hususani zitakazoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Lazima tuwekeze pia katika afya ya udongo wetu, lakini tatu lazima pia tuwekeze katika utafiti na huduma za ugani. Ili tuweze kufanya matatu yote haya lazima tuwekeze kwenye teknolojia na masuala ya TEHAMA, matumizi ya teknolojia kwa ajili ya kukuza kilimo na uzalishaji wetu na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hapa nirejee, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, mapema mwaka huu alisema kwamba tunakwenda kujenga kituo kikubwa cha TEHAMA hapa nchini. Kwa hiyo, hiyo inaonyesha dhamira yake kwenye masuala ya TEHAMA na kwenye Mpango huu ningependekeza Serikali ioneshe jitihada za makusudi kabisa, inakwenda kuinuaje sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kwenye mwezi wa Nane aliyekuwa Waziri wa Wizara inayosimamia masuala ya TEHAMA alisema kwamba Tanzania imepata dola miloni 150 kwenye mradi ambao unaitwa Tanzania Digital Project. Kwa hiyo ningependa kupendekeza baadhi ya zile fedha kama mgao ulivyofanyika kwenye hizi pesa za Covid, basi hata katika zile baadhi zielekezwe katika kufanya tafiti na kuja na ubunifu wa kiteknolojia ambao utatuwezesha kuwa na mbegu bora, kufahamu afya ya udongo wetu, lakini pia kutoa huduma za ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hivi karibuni tumetangaziwa kwamba Benki ya CRDB imepata dola milioni moja kutoka kwenye Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi ili kutoa mikopo kwa wakulima wadogo. Niiombe sana Serikali ihakikishe kwamba fedha zile zinakwenda kweli kwa wakulima wadogo na sio kunufaisha wafanyabiashara wakubwa, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya zile fedha pia zinaweza zikaelekezwa katika kutafuta mbinu kwa kutumia teknolojia za kupambana na haya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo narudia tena mbegu bora, kufahamu afya ya udongo wetu na kutoa huduma za ugani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeshasema kwamba ungependa kuona Bunge lako la Kumi na Mbili linaacha historia na legacy yake kwenye sekta ya kilimo. Wengi tumeongea kwamba tunahitaji bajeti iongezeke kwenye sekta ya kilimo, lakini tunayo fursa ambayo naiona ni low- hanging fruits. Kwenye sheria ambazo zipo chini ya TAMISEMI, kila halmashauri inatakiwa ifanye reinvestment kwa maana kwamba kama kwenye mapato ya council ilipatikana shilingi milioni moja kutokea kwenye sekta ya kilimo, wanatakiwa wafanye reinvestment asilimia 20 kwenda kukuza ile sekta ya kilimo. Asilimia 15 wafanye reinvestment kwenye sekta ya mifugo, asilimia tano kwenye sekta ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la reinvestment halifanyiki. Kwa hiyo ni low-hanging fruits ambao sisi kama Bunge tunaweza tukahakikisha kwamba TAMISEMI watekeleze sheria hiyo, TAMISEMI watekeleza takwa hilo la kisheria, kwa sababu moja kwa moja hapo sekta ya kilimo itaweza kupata fedha nyongeza zinazotokana na uzalishaji kutokana na sekta hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuipongeza Serikali kwamba wamekuja na mpango wa e-commerce yaani biashara ya mtandao. Wanufaika wakubwa na biashara wa mtandao ni watu ambao wapo kwenye sekta za uzalishaji, kilimo, mifugo na uvuvi, lakini mpaka hivi sasa kwa mujibu wa taarifa za Shirikisho la Watoa Huduma za Simu - GSMA wanasema bado mpaka sasa asilimia 48 ya Watanzania hawatumii mobile internet. Sasa ikiwa bado hatutumii mobile internet ina maana hata matumizi yale ya e-commerce hatutaweza kufikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda nipendekeze kwa Serikali iwekeze jitihada kubwa kwa kushirikiana na wadau kuja na mfumo wa kuhakikisha kwamba wanatoa elimu ya digital literacy na digital skills, kwa sababu bila ya kufanya hivyo hata huu mpango wa biashara mtandao hatutaweza kunufaika nao kutoka na kwamba watu tunazo simu lakini hatutumii simu zetu kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia nielezee suala zima la vyanzo vipya vya mapato. Nakumbuka Mheshimiwa Raisi alivyokuja hapa kuhutubia kwenye Bunge lako Tukufu mwezi Aprili alisema kwamba tutanue wigo wa walipakodi. Hapa narudia tena kusema, lipo kundi kubwa la wafanyabiashara walio kwenye sekta isiyo rasmi. Katika kila shilingi kumi ambayo inazunguka kwenye uchumi wetu shilingi sita ipo kwenye sekta isiyo rasmi. Kwa hiyo, ni lazima Serikali ije na mpango mkakati wa namna gani tutarasimisha biashara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ningependa kupendekeza, ikiwa kama Serikali inaweze ikaweka mazingira wezeshi ya kuvutia wawekezaji, inaweza ikatoa misamaha ya kodi kwa ajili ya wawekezaji, kwa nini isifanye hivyo kuhakikisha kwamba inawavutia wale wajasiriamali ambao biashara zao hazijarasimishwa waweze kuzirasimisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna swali liliulizwa kwamba tuna mabilionea wangapi? Kwa hivyo, ninachopenda kupendekeza ni Serikali ije na mpango wa kuweka angalau miaka miwili ya tax holiday, misamaha ya kodi kwa wazalishaji…

MWENYEKITI: Hivi tulijibiwa tuna mabillionea wangapi?

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulijibiwa kwamba tuna mabillionea takriban 5000 na wote ni kwa hisani ya Chama cha Mapinduzi, kama nipo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwamba, tunahitaji kuja na mpango ambao utawavutia wale walio kwenye sekta isiyo rasmi kurasimisha biashara zao. Mpango ambao utawavutia vijana, wanawake na wenye ulemavu kuingia kwenye biashara rasmi. Kwa hiyo ningependa kuiomba Serikali ije na angalau miaka miwili ya msamaha wa kodi kwa biashara mpya ambazo zinaanzishwa na makundi haya na kama inafanya hivyo kwa wawekezaji naamini kabisa inaweza pia ikafanya hivyo kwa kundi hili la vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na hapo ndio tutakuwa tunafanyia kazi ile dhana nzima ya kuongeza wigo wa walipakodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote hapa tunafurahia na tunamshukuru sana Mheshimiwa Raisi Samia Suluhu Hassan kwa pesa za Covid-19 ambazo zimeingia nchini. Pia ningependa kutumia fursa hii nipendekeze kwa Serikali iko haja ya kutumia makundi yenye ushawishi mkubwa kwenye jamii kumuunga mkono Mheshimiwa Raisi katika vita hii ya Covid-19 na kutoa elimu kwenye jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka siku ya Mkutano Mkuu wa NGOs, binafsi nilimwomba Raisi Samia Suluhu Hassan kwamba NGOs ziweze kushiriki kwenye kutoa elimu kwa jamii, wasanii washiriki kwenye kutoa elimu kwa jamii, vyombo vya habari vishiriki kwenye kutoa elimu kwa jamii, watu mashuhuri washiriki kwenye kutoa elimu kwa jamii kuhusu Covid-19, hata na sisi Wabunge tushiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningependa kuishauri sana Serikali, kama ambavyo Ofisi ya Rais, TAMISEMI wameweka wazi mgao basi na Wizara ya Afya pia iweke wazi mgao wa kile kipande cha elimu ya jamii kwenye upande mzima wa Covid-19, kwa sababu mpaka sasa hauelewi kipande kile kinatumikaje na nani ambaye anafanya au anatoa elimu hiyo ngazi ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kusisitiza sana iko haja kubwa ya kuweka kipaumbele kama ambavyo Wabunge wamesema katika Sekta ya Kilimo, Sekta ya Mifugo na Sekta ya Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga tena mkono hoja. (Makofi)