Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie Mapendekezo hayo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa ajili ya Mwaka 2021/2022 - 2025/2026. Kwanza nitoe shukrani, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha nyingi sana jimboni kwetu za madarasa, barabara lakini pia za hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mpango sasa, ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage amesema vizuri na Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Kilimo, sisi tunachangia kilimo. Sekta ya Kilimo ndiyo inayofanya tuseme, tuongee hapa. Kilimo kimekuwa na kauli nyingi sana; Kilimo cha Kufa na Kupona, Siasa ni Kilimo na Kilimo ni Uti wa Mgongo, lakini leo naona uti wa mgongo hauna mfupa, huu kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisemee mambo machache ambayo ni muhimu sana. Kilimo cha kwetu kinadumaa na kama kilimo kinadumaa na kinaajiri zaidi ya watu asilimia 75. Kwa hiyo watu wote huko vijijini hali siyo nzuri. Sababu kubwa ni uhaba wa mbegu, ukosefu wa mbolea, lakini vile vile bei kubwa ya mbolea na bajeti ndogo ya Serikali kwenye kilimo. Niwakumbushe tu kwamba bajeti ya mwaka jana ilikuwa asilimia 0.8 ya bejeti ndiyo kilimo, lakini pia tumetekeleza skimu zote za umwagiliaji lakini pia ukosefu wa watalaam wa kilimo, Maafisa Ugani Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kina mchango mkubwa sana kitaifa. Moja, kilimo kinatoa ajira kwa wananchi zaidi ya asilimia 75, lakini kinachangia bajeti asilimia karibu 27, lakini pia malighafi viwandani na chakula kwa Watanzania wote, kilimo ni kitu muhimu sana. Ili niweze kuchangia na niwe mkweli ningependa kupendekeza yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Fedha na Mipango ije na Mpango mzuri wa kujenga Viwanda vya Mbolea. Ili tuweze kupunguza bei kubwa ya mbolea lazima tuwe na Viwanda vya Mbolea hapa nchini, tulikuwa nacho kimoja huko Tanga kimekufa, Kampuni ile TFC haina kazi yoyote. Kwa hiyo, tunahitaji viwanda vya mbolea nchini, sisi tuna malighafi zote za kujenga viwanda vya mbolea hapa, gesi tunayo, lakini pia malighafi nyingine zinapatikana. Ndiyo maana watu kutoka Burundi wanakuja kujenga Kiwanda cha Mbolea hapa na hawaleti malighafi kutoka nje. Malighafi ipo hapa, tujenge Kiwanda cha Mbolea ambacho kitafanya mbolea ipatikane. Kwa wale ambao hawafahamu mbolea iliyopo nchini sasa ni asilimia 35 haizidi 40, lakini pia bei zake wananchi hawawezi kununua mbolea kwa bei ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, umefika wakati ni lazima tupange ardhi ya kilimo. Sasa hivi ardhi haijulikani ipi ni ya kilimo, tumepanga ardhi ya wanyama, National Games, maeneo oevu, lakini kwa kilimo, haiwezekani akaja mkulima mkubwa sana anataka Tanzania tumpe ardhi iko wapi? Haijawa demarcated.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda basi, kama inashindwa kuwa demarcated, Serikali irasimishe mashamba ya wakulima wadogo wadogo kama ardhi ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni kilimo cha umwagiliaji. Hatuwezi kutoka kwenye kilimo cha kutegemea mvua? Sasa hivi tunaambiwa mvua haitoshi, lakini mabwawa yapo yamejaa maji. Tungekuwa na skimu za kumwagilia zinazojulikana, siyo kumwagilia kwa mitaro, mashine kubwa zimwagilie mashamba ya kisasa. Tunaweza tukapanga kiasi gani tutavuna kwa mwaka kwa kutumia umwagiliaji. Siyo mvua hainyeshi, mwaka huu hatupati. Nashauri kilimo cha umwagiliaji ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni kuongeza bajeti. Bajeti ya Serikali ya 0.8 kwa mwaka kusaidia sekta ya kilimo haitoshi kabisa. Napendekeza na watu wote duniani wanasema lile Azimio la Maputo, lilisema Serikali iweke asilimia 10, iwe ndiyo kwa ajili ya kilimo. Sasa mimi napendekeza hata twende 5% siyo 0.8%, hatuwezi kuwa na kilimo bora.

La mwisho ni Benki ya Kilimo. Tunayo Benki ya Kilimo hapa nchini. Hii benki haifanyi kazi yoyote kusaidia kilimo, haionekani popote katika ushiriki wake wa kujenga au kuongeza tija ya kilimo. Inakopesha watu na imekuwa tu ni wakala wa mabenki ya biashara na ili wananchi wachache wajanja wajanja waweze kukopa, lakini wakulima wadogo wadogo ambao benki hii ilikuwa imekusudiwa kwenda kuwasaidia, haionekani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nchi nzima hii ina ofisi moja tu kwenye hii benki ya kilimo. Haionekani mikoani kote wala kwa wakulima. Imekuwa tu Wakala kwamba unataka kwenda kukopa CRDB, unataka kwenda kukopa benki yoyote ile, sijui NMB, wao ndiyo wanakuwa brokers, wanasema wanaweka dhamana. Benki ya Kilimo ichukue jukumu lake na Serikali isaidie kuipa fedha nyingi Benki ya Kilimo ili iwakopeshe wakulima wadogo wadogo kuongeza tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo suala lingine dogo nje ya kilimo ambalo ni REA. Mradi wa REA ni muhimu sana, unaleta maendeleo makubwa vijijini, lakini utekelezaji wake umeanza kuwa na matatizo. Wanajenga halafu vijiji vingine wanaruka. Wale wananchi ambao wanarukwa vijiji vyao wanakuwa wanyonge sana. Wanakosa raha, wanakuwa kama siyo Watanzania. Tumefanya mikutano na watu wa REA, wale Wakandarasi wanasema wao wamepewa BOQ ya nguzo 20 kwa kijiji kimoja. Sasa kuna kijiji cha pili yake labda nusu kilomita wanakiruka, waya za umeme zinapita kwenda kuweka umeme kijiji kingine kinachofuatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imekuwa kasoro kubwa sana ambayo inaleta chuki kwa wananchi wetu na viongozi. Vile vile, suala hili linafanya wananchi wengine wawe na matabaka kati ya wananchi wengine; hapa pana umeme, umeme huo unaruka mahali fulani. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Nishati... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)