Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana ambaye ni Naibu Spika wetu; naomba awali ya yote kabisa nianze kwa niaba ya wananchi wa Sikonge kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuenzi maana halisi ya majina yake, maana Samia maana yake ni Msikivu, Suluhu maana yake ni Mpatanishi na Hassan maana yake ni Mzuri au mtu mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana, ndio maana mwezi uliopita kwa makusudi kabisa akaamua kuwaongezea Watanzania kwenye bajeti yao, zaidi ya Shilingi trilioni 1.3 ili zikapeleke rekodi ya maendeleo ambayo haijawahi kupatikana katika miaka ya hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena kwa kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango ambao Mheshimiwa Waziri aliuwasilisha kwa weledi mkubwa sana. Nimpongeze Waziri na timu yake yote kwamba, wameweza kuwasilisha kwa weledi mzuri sana Mapendekezo ya Mpango. Pia simsahau Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Daniel Sillo aliposimama kuwasilisha maoni ya Kamati aliwasilisha kwa ueledi mkubwa sana. Hongera sana Mheshimiwa Daniel Sillo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Spika Job Ndugai, siku ya Jumanne alitoa maelekezo muhimu sana kwa Serikali akiwa kwenye kiti kile pale. Akaiagiza Serikali kwamba, fanyieni kazi suala la upandaji wa bei ya mbolea kwa haraka iwezekanavyo. Hiyo kweli nampongeza sana Mheshimiwa Ndugai, kwa sababu, ni jukumu ambalo ni muhimu sana kwa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maoni katika maeneo manne tu. Eneo la kwanza, naomba sana katika hatua hii ya mapendekezo ya Mpango naomba Serikali ikasisitize, Mpango utakaoletwa na bajeti yake itakayopendekezwa, ni muhimu sana Serikali itenge bajeti maalum kwa ajili ya vitu viwili; ruzuku ya pembejeo za wakulima na hii ni kwa nchi nzima. Pili, kupanga fedha za buffer stock kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima pale ambapo uzalishaji utakuwa mkubwa ukazidi soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kupendekeza katika maoni yangu, Mfuko wa Jimbo ni wa Sheria ya Mwaka 2009. Kwa sasa hivi una umri wa miaka 12, vigezo ni vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wakati Waziri atakapoleta Mpango azingatie vile vile, Serikali ilete marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Jimbo ili kuboresha zaidi malengo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, nilikuwa naangalia upandaji wa bidhaa muhimu nchini, hasa hasa bidhaa za ujenzi na nimeona kwamba kuna tatizo ambalo Serikali inabidi iweke mkakati maalum. Afrika Kusini mwaka uliopita 2019/2020, kwa sababu ya UVIKO walifunga viwanda 2,000. Mwaka jana na mwaka huu 2020/2021, wamefunga viwanda 1,000 kwa sababu ya mambo ya lock down. Sasa hii imesababisha demand ya bidhaa zinazotengenezwa Tanzania ivuke mipaka ya nchi kwa kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna demand kubwa ya bati, kuna demand kubwa ya cement, kuna demand kubwa ya bidhaa za chuma ikiwemo nondo katika nchi hizo za Kusini mwa Afrika - SADC kwa ujumla. Kwa hiyo, lazima Serikali itengeneze utaratibu/mkakati maalum wa namna ya kukabiliana na hiyo hali ya hiyo demand. Matokeo yake, uzalishaji wa Tanzania sasa umekuwa ni wa export zaidi, kwa hiyo demand ya ndani ya nchi nayo imeathirika matokeo yake bei zimepanda sana. Kwa hiyo, naomba Serikali ije na mkakati maalum wa namna ya kudhibiti hali hiyo ya biashara kuanzia sasa, sio kusubiri mwakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nitatumia muda kidogo hapa, kwa miaka mingi kumekuwa na udhaifu kwenye eneo la ufuatiliaji na tathmini na ndio maana akienda Mkuu wa Mkoa, anagundua matatizo, akienda Mkuu wa Wilaya kwenye miradi, anagundua matatizo, akienda mkimbiza Mwenge wa Kitaifa, anagundua matatizo, akienda CAG, ndio kabisa. Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuimarisha ufuatiliaji na tathmini (monitoring and evaluation). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana Kamati imekuwa inasisitiza mara kwa mara na Serikali imekiri Bungeni humu kwamba, upo umuhimu sasa wa Serikali kuja na sera na sheria maalum itakayo-guide M&E nchini. Nikisema hivi watu wengine watasema mbona sheria zipo tunazo, sawasawa ni kweli. Tuna Sheria 10 zinazo-guide M&E nchini na nitazitaja kwa kifupi kabisa. Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001, inayo-guide utunzaji wa nyaraka, matumizi na ukaguzi wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ni Sheria ya Ununuzi wa Umma ina-guide M&E za mikataba, kukagua miradi na utunzaji wa nyaraka; Sheria ya Tawala za Mikoa, Sheria za Serikali za Mitaa, Sheria ya PCCB kuhusu masuala ya kudhibiti ubadhirifu, Sheria ya Polisi - Police Force Ordinance kuhusu ukaguzi wa sheria zote, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria ya Utumishi wa Umma kuhusu Strategic Plan na OPRAS, Sheria Kuu ya Jinai (Penal Code) kuhusu wajibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Sheria ya Kodi ya Mapato kuhusu kufuatilia ajira, biashara na uwekezaji. Halafu kuna Sheria nne kuhusu tathmini; Sheria ya Ukaguzi wa Umma ambayo anaitumia CAG; kuna Sheria ya Bajeti, halafu kuna Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana za Serikali ambao kwenye Financing Agreement inaweza ikatoa M&E framework, kwa ajili ya miradi na program fulani fulani. Halafu ya mwisho ni Sheria ya NBS – National Bureau of Statistics hii Sheria nayo ina-guide kuhusu evaluation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna Sheria 14 sasa kuna hapa na pale, kuna mambo fulani fulani ambayo inaonyesha kabisa kwamba hii M&E haipo streamlined. Kwa hiyo, ombi langu, Serikali mwaka ujao itunge Sera ya M&E halafu vile vile, ifuatiwe na Sheria ya M&E ambayo sasa hiyo ndio itatumia…

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya kufuatilia na ku-evaluate mambo ya Serikali yote kwa ujumla. Ahsante sana. Kuna taarifa hapa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome, naomba mchangiaji ameshasema ahsante sana. Umemaliza Mheshimiwa Kakunda?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Bado hajamaliza.

MWENYEKITI: Sawa, endelea Mheshimiwa Salome Makamba.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Kakunda kwamba, tulishaleta mapendekezo ya kuunda sera ya monitoring and evaluation na Serikali ilishapokea na ikasema inaenda kulifanyia kazi. Kwa hiyo, labda tuombe Serikali walete kwenye commitment ya Mpango huu, sera hiyo, lakini tulishawapelekea. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome, unasema tulishaleta wewe na nani?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna-Caucus Maalum ya Monitoring and Evaluation, tulileta na Kamati ya Bajeti walileta lile pendekezo na walitoa Azimio la Bunge.

MWENYEKITI: Ngoja kwanza ngoja. Ukisema tulileta, maana yake ulileta kwa Spika, la sivyo useme tuliipelekea Serikali. Kama ukisema tulileta maana yake ulileta kwa Spika, ndio maana nakuuliza wewe na nani mlileta?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hicho Kiswahili chako hicho hicho ndio nachukua na mimi na-adopt, lakini point yangu ni kwamba suala hili Serikali ilishalipokea na ni Azimio rasmi la Bunge. Kwa hiyo, commitment ya Serikali wataleta lini sera hiyo ndio nafikiri alichotaka kukisema Mheshimiwa Kakunda. (Makofi/ Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kakunda unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge Wakereketwa wa ufuatiliaji na tathmini na naipokea taarifa ya Mheshimiwa ya Salome Makamba. Ndio maana mimi sikutaka kuisema hiyo, kwa sababu, ile ilipelekwa katika utaratibu ambao sio wa Bunge kwa maana kwamba, Kamati yetu sisi ya Wakereketwa mambo yetu humu Bungeni yanaletwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yalishaletwa humu na Waziri mwaka jana alisema kwamba suala hilo ni muhimu. Kwa hiyo, kama Serikali ilishakiri kwamba suala hilo ni muhimu ndio maana tunasisitiza kwamba, kwenye Mpango ujao walete sasa mchakato maalum ambao utatunga Sera ya M&E halafu itahitimishwa na utungaji wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie mchango wangu sasa kwamba lengo la pendekezo hili sio kuzifuta Sheria zile 14 nilizotaja, hapana. Lengo ni kunyoosha utaratibu wa usimamizi, ufuatiliaji na tathmini katika nchi yetu, ili uwe wa Kimataifa na kuhakikisha kwamba tunapunguza observations zile ambazo CAG ndio huwa anasubiri akienda anazikuta au mkimbiza mwenge akienda anazikuta, au Mkuu wa Mkoa akienda anazikuta, au Waziri au Waziri Mkuu au Rais akienda anazikuta yapunguzwe hayo kwa kufuatilia. Kuna maeneo 35 ya kufuatilia kwenye mchakato wote wa mradi. Maeneo hayo yakifuatiliwa vizuri, hizo observations za CAG na Wakaguzi wengine zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)