Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa muda huu niliopewa kuchangia hoja hii kuu ya Wizara ya Fedha. Kabla sijasema yangu machache nami niseme nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kazi nyingi, kwa muda mfupi usiozidi siku 100 ambao tumeshuhudia. Tumeshuhudia maelekezo, tumeshuhudia kazi, tumeshuhudia na mfumo mpya wa utendaji wa kazi na tumeshuhudia na kasi mpya ya utendaji wa kazi. Kwa hiyo, nami nampongeza sana, angalau katika siku hizi ambazo hazizidi 100 ambazo amekaa madarakani wananchi tumepata matumaini makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata matumaini na mengi Waheshimiwa Wabunge mnayaona hata humu kupitia Bungeni. Yapo mambo mapya ambayo tulikuwa hatujashuhudia, mnayaona. Haya makofi mengi ya Mheshimiwa Waziri Ummy ni matumaini mapya ambayo yamekuja na utaratibu mpya. Bajeti ni ile ile, pesa ni zile zile, lakini huu ni ubunifu mpya wa namna ya kusimamia na matumizi mazuri. Kwa hiyo, haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita katika siku zisizozidi 100. Sasa fikiria tukifika mpaka 2025, Mheshimiwa Ummy atasema maneno mangapi huyu? Tunajua yako mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunampongeza. Kwetu sisi tulioko wote, maana ni Wabunge wote tuna matumaini makubwa kutokana na mageuzi makubwa anayoyafanya. Nami nimepewa shilingi milioni 500 zile barabara, nimeelekeza zitumike kwenye barabara zangu. Haya ni mapinduzi makubwa kwamba sasa na Wabunge tunashiriki katika kupanga miradi ya maendeleo. Yaani tunashiriki kupeleka pesa na kusimamia pesa tuliyopeleka wenyewe kwa maelekezo ya barabara na miradi tunayoitaka. Tumeulizwa hapa habari ya shule tunazotaka zipelekewe pesa, Wabunge wote tumechagua shule. Ni mapinduzi makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda sana kupongeza haya, yatatupa ule usimamizi wa karibu ambao tulikuwa tumepewa kwenye Katiba, sasa tunapewa kiuhalisia kwamba kuna upangaji wa bajeti unaokwenda kwenye milango ya Serikali na mwingine upande wa jimbo tunakwenda kusimamia. Kwa hiyo, napongeza sana juhudi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wizara ya Ardhi ni Sekta wezeshi. Katika miradi yote inayopangwa humu ndani, yote inatekelezwa kwenye ardhi. Kazi kubwa na maelekezo makubwa tuliyopewa na Mheshimiwa Rais ni kupunguza urasimu katika upatikanaji wa ardhi katika kutekeleza yote yanayopangwa hapa hasa ya uwekezaji. Tumeshuhudia katika kipindi hiki cha siku zisizopungua 100 Mheshimiwa Rais kwa kutumia madaraka ya kisheria aliyopewa ameweza kufuta mashamba yasiyopungua 11 yenye ekari ya zaidi ya 24,119. Mashamba haya yamefutwa kwa sababu yalikuwa hayaendelezwi vizuri. Haya mashamba yako kila mahali, hata Waheshimiwa Wabunge mlipokuwa mnachangia sehemu nyingine, mnayaita mashamba pori. Kwa hiyo, ni fursa Waheshimiwa Wabunge, kama kuna mashamba kama haya watu wanamiliki sehemu mbalimbali lakini mnayaona kwa macho hayaendelezwi, tuambizane kutoka huko huko ili tuchukue hatua za kisheria tuyafute ili waweze kupewa watu wengine wenye uwezo wa kuyaendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mashamba haya ameelekeza sehemu wagawiwe wananchi ambao hawana ardhi ya kutosha na sehemu tumehifadhi kwa ajili ya uwekezaji. Pia tulikuwa na mashamba yenye ekari 45,788 ambayo yalifutwa siku nyingi lakini maelekezo ya namna ya kutumia yalikuwa yatoke kwa Mheshimiwa Rais na yalikuwa hayajatolewa. Mama ametoa maamuzi kwamba mashamba haya angalau ekari 33,672 kati ya ekari 45,000 wagawiwe wananchi wayatumie na sehemu iliyobaki ya ekari 15,000 ziwekwe kwa ajili ya uwekezaji kupitia taasisi ambazo zinasimamia uwekezaji za EPZA na TIC, kulima mashamba ya katani, kujenga viwanda na vitu vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeshuhudia katika kipindi hiki cha siku zisizozidi 100 uwekezaji maombi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji yamekuwa makubwa sana. mpaka tarehe 01 mwezi wa sita ofisi yangu imeshapokea maombi 305 ya watu wawekezaji mbalimbali wanaokuja kutaka ardhi kwa ajili ya uwekezaji mbalimbali. Na kati ya hayo, kama nilivyosema juzi, sasa tumeanza kukaa Kamati ya Kitaifa ya Ugawaji wa Ardhi inakutana kila wiki kwa hiyo, katika maombi 305, mia tatu na tatu yameshapewa majibu na wawekezaji wameshapewa ardhi ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji huu tunakwenda kushuhudia Morogoro kuna uwekezaji mkubwa wa kiwanda cha sukari. Kigoma kuna watu wameomba kwa ajili ya viwanda vya sukari, lakini Kilwa kule kuna kampuni kubwa zinakuja kulima mihogo, lakini yanaweka viwanda vya kuchakata mihogo kwa soko la China kwa ajili ya kununua vilevile mihogo inayolimwa katika Mikoa ya Kusini, lakini hapa Kibaha tumeshuhudia kampuni zimeanza kuomba sasa maeneo ya industrial park. Iko kampuni moja ambayo imepewa ekari 1,000 na imeahidi itawekeza viwanda 73 katika hiyo industrial park. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hayani mambo yanayotokea ndani ya siku zisizozidi 100 kwa hiyo, uwekezaji nao unaenda kwa kasi. Na sisi kama sekta wezeshi tunaahidi mbele yenu Bungeni hapa, tunamuahidi Mheshimiwa Rais kwamba, tutatimiza wajibu wetu, tutaondoa urasimu na kuhakikisha uwekezaji unakuwa wa tija katika nchi hii, hasa katika matumizi ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ardhi hii imetengwa mikoa yote. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wakuu wa Miko ana Wakuu wa Wilaya wametenga ardhi za kutosha na halmashauri, kama mamlaka za upangaji ziko huko. Kwa hiyo, nataka kuwahakikishia wawekezaji wote Tanzania ni salama kwa uwekezaji na ardhi ya kuwekeza ipo. Mtu yeyote ambaye anafikiri nataka kuwekeza, kujenga majengo, kujenga viwanda, ardhi ipo; kokote kule kama wakikusumbua tuonane huko wizarani sisi tunajua ardhi ilipo mahali popote katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, ndani ya Bunge hili tumeshuhudia Waheshimiwa Wabunge mkisema gharama za umilikishaji ni kubwa na wengi mlikuwa mnaitaja tozo ya premium. Kama walivyosema Wabunge wengine, inaelekea Mheshimiwa Rais huwa anasikiliza kule, leo tumemsikia Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametangaza hapa kwamba toso ya asilimia mbili na nusu kwa kila anayemiliki ardhi kwa mara ya kwanza ya thamani ya ardhi sasa imepunguzwa na inakuwa 0.5. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake nini? Hawa wote wawekezaji ambao tumewapa ardhi zaidi ya 303 wangepaswa kulipa asilimia 2.5 ya thamani ya ardhi na hii si kodi ni tozo. Na wote hawa kila anayemiliki kiwanja, hata urasimishaji wakipata invoice wanamfuata Waziri awapunguzie, nilikuwa nawapunguzia, lakini je, mtu wa Kigoma atamuona Waziri? Je, mtu wa Kilosa kule atakuja kwa waziri?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo Mheshimiwa Rais ameleta tiba kwamba, wote wanaomiliki ardhi kwa mara ya kwanza wamilikishwe kwa tozo ya 0.5 yaani nusu ya asilimia moja. Kwa hiyo, hii itaongeza ari ya uwekezaji, lakini na wananchi masikini ambao wanataka kumiliki ardhi zao kwa kupata hati, hasa katika zoezi la urasimishaji. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini nampongeza sana rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa hotuba yake nzuri sana ambayo ameisoma hapa ambayo imewezesha tozo hii kupunguzwa kutoka asilimia 2.5. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi nilivyosikia mazungumzo ya Waheshimiwa Wabunge wengi naona tozo hii mmeikubali kwamba, ipungue. Na pengine tunavyoendelea inaweza ikafutwa kabisa kwa sababu, hii sio kodi ni tozo. Kodi za msingi za umilikaji zipo na mtu akimiliki ardhi kwa mara ya kwanza maana yake anakuwa mlipa kodi wa kila mwaka kwa miaka 99. Kwa hiyo, ni vizuri mtu amiliki kwa gharama ndogo kwa sababu bado anatupa japo kidogo kidogo, lakini kwa miaka 99. Hawa ni walipa kodi wa kudumu wa uhakika, yaani akinunua shati maana yake atalilipia kodi kwa miaka 99, akipewa hati miliki maana yake huyo anaingia kwenye daftari la ulipa kodi la Serikali kwa miaka 99. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huu ni mwanzo mzuri. Nafikiri tukiona inaenda vizuri mwaka huu tunaamini hata mapato yatokanayo na kodi ya ardhi yataongezeka kwa sababu, leo tuna viwanja laki tisa ambavyo tumevipima, lakini watu hawajachukua hati kutokana na tozo hiyo. Kwa michoro ya survey ambayo inaonesha viwanja mbalimbali vilivyopimwa nchi hii kwa urasimishaji na viwanja na mashamba tunayo michoro ya viwanja elfu tisa ambavyo vimepimwa, lakini hatujatoa hati. Watu wanasita kuchukua hati kwa sababu tozo hii ilikuwa kubwa kuliko kodi ya asili ambayo imetungwa na Sheria ya Bunge. Kwa hiyo, tunahisi baada ya kuondoshwa hii premium then tunaamini kwamba, wananchi watamiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi Waheshimiwa Wabunge wamewasemea na Mheshimiwa Rais amesikia ameondoa hii kodi. Kwa hiyo, hakuna kizuizi chochote sasa kisingizio cha kuweza kumilikishwa kwa sababu, gharama kubwa ya umilikishaji imeondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaelekea na sisi kama Wizara, kama ambavyo wameanza kodi ya majengo kwenda ki-electronic, na sisi tumejipanga kuja ki-electronic vilevile. Tunaangalia uwezekano pengine mwakani tutakuja na bajeti tofauti, tunaangalia namna nzuri zaidi ya ukusanyaji wa kodi ya ardhi pengine kwa kuunganisha na majengo, lakini tutajipanga vizuri. Na sisi tunaunga mkono hili la ukusanyaji tujaribu ukusanyaji huu wa kutumia bili za umeme, lakini na sisi kwenye kodi ya ardhi kwa sababu, majengo yako kwenye ardhi na taariza zote tunazo kwa hiyo, na sisi tunajipanga ki-electronic.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tumefunga mfumo mpya ambao umetengenezwa na vijana wa kitanzania. Mwezi ujao tutaanza kutoa Hati za Electronic hapa Dodoma. Mfumo huo utatuwezesha sisi kutokutumia mabavu sana kufuatilia kodi ya kila mwaka kwa sababu, ndani ya mfumo ule tuna namba za simu, tuna taarifa za kila mmiliki wa ardhi. Ikifika siku ya kulipa kodi message itakujia kwenye sim una kukuomba ulipe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mfumo ambao umetengenezwa na wataalamu wa Wizara na utaanza kutumika. Wale wote ambao watachukua hapa Dodoma hati kuanzia tarehe 01 mwezi wa saba wataanza kupata hati za electronic. Na pengine tutaachana na hii tabia ya kufukuzana kwa sababu, kila mwananchi atakumbushwa siku ya kulipa kodi. Tunataka tufanye jambo hili nchi nzima, ili tupunguze kasi ya kukamatana na kufukuzana kwa ajili ya ukusanyaji wa kodi, turahisishe, lakini tupate mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakushukuru sana kwa muda ulionipa, lakini nataka nirudie kuunga mkono kwa nguvu zangu zote hotuba hii ya Wizara ya Fedha kama walivyofanya wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini kuwapongeza sana wenzetu Mawaziri wa Wizara ya Fedha na watendaji wote wa Wizara ya Fedha. Naunga mkono hoja. (Makofi)