Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima wa afya na kuweza kuandika mchango huu kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali chini ya uongozi wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuleta bajeti hii iliyolenga kuwapa matumaini wananchi wa Tanzania kwa kuondoa baadhi ya changamoto zinazoendelea kuwakabili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba bila makusanyo ya kodi hatuwezi kufika mbali kimaendeleo wala hatuwezi kutekeleza miradi ya maendeleo tunayopanga. Lazima wananchi wa Tanzania waweze kuwa na uelewa mpana kuhusu uwajibikaji na wigo wa kukubali kukusanya kodi kupitia wafanya biashara wakubwa na wadogo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa sio waaminifu katika kutumia mashine za kielektroniki. Wamekuwa wakisingizia kuwa ni mbovu au kukusanywa na TRA. Jambo hili limekuwa likidhoofisha sana ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Tumekuwa na juhudi kubwa kama wananchi wa Tanzania tunaponunua bidhaa madukani kudai risiti, lakini kwa muda mrefu sasa wafanyabiashara walio wengi wamekuwa hawatoi risiti wanapofanya mauzo. Niiombe sana Serikali, usimamizi iliyoueleza kupitia hotuba hii ya bajeti iwahusishe wafanyabiashara wote waliostahili kutumia mashine za EFD.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yetu kwamba wale wote wanaopaswa kutumia mashine za kielektroniki watatekeleza wajibu wao lakini pia wanaopaswa kusimamia ukwepaji kodi kwa wafanyabiashara hawa wataweza kusimamia ipasavyo. Pia ni mategemeo ya wananchi kwamba vyanzo vipya vilivyoainishwa kukusanywa kupitia mafuta na miamala ya simu itaweza kukusanya ipasavyo na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopangwa. Wananchi hawana maswali mengi pale wanapoona fedha yao inayochangwa na kukusanywa na kuona kwa uhalisia utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo lililokuwa changamoto kubwa kwa wananchi ni suala la tozo kwa bidhaa hata za nyumbani kuendelea kutozwa kodi. Ni furaha ilioje kwa wananchi wa Tanzania kuona bajeti hii imekuja kuondoa kabisa changamoto hii. Ni imani ya wananchi kwamba zile changamoto nyingine zilizobaki zitaweza kufanyiwa kazi hatua kwa hatua. La msingi wananchi tujitahidi kuchangia makusanyo ya kodi ili fedha itayopatikana iwe mfano wa kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopangwa ili bajeti ijayo iweze kutatua changamoto nyingine zilizobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi wananchi wamekuwa wakihoji kuhusu fedha za Jamhuri ya Muungano kupitia Mfuko wa Pamoja wa Fedha. Niwaombe tu wananchi wa Zanzibar kuangalia miradi inayoendelea kutekelezwa kwa upande wa Zanzibar kupitia Mfuko wa Jamhuri ya Muungano na kufuatilia gharama ya fedha zilizotumika kupitia miradi hiyo. Hii nchi ni moja na utekelezaii wa miradi unaendelea vizuri, muhimu tuendelee kulipa kodi kwa manufaa ya Watanzania wote. Tuendelee kusimamia mapato yanayotokana na kodi kwa manufaa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo machache naunga mkono hoja.