Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai. Vile vile napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, jemedari wetu, mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi tukiwa kama wanawake nchini Tanzania tunatembea kifua mbele kwa ajili yake na tunamuunga mkono na tutaendelea kumpambania hata kule katika majimbo yetu kwa kuyaeleza yale mazuri yote anayowafanyia wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa yafuatayo: Kwanza kabisa, ameweza kuongea na wazee pale Jijini Dar es Salaam, aliweza kuongea na viongozi wa dini, aliongea na sisi akina mama hapa Dodoma na pia aliongea na vijana pale Mwanza na kukubaliana na maombi ya vijana kwamba wataunda Baraza lao la Vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuja na bajeti nzuri ambayo imekwenda kuwapunguzia kodi wafugaji, wakulima pamoja na wale wenye NGOs zao. Pia ni kodi ambayo imeangalia mpaka yule mtu wa hali ya chini, bodaboda kwamba kipato chake ni cha chini na kuweza kumpunguzia kodi ya adhabu kutoka shilingi 30,000 kwenda shilingi 10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi za Mheshimiwa Rais, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake, Mheshimiwa Engineer Masauni kwa bajeti yao nzuri sana ya mwaka 2021/2022. Nawapongeza sana watendaji wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Katibu Mkuu pamoja na Gavana wa Fedha, Mheshimiwa Luoga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Naibu wake kwa kuja na wazo la kukusanya Property Tax kutoka kwenye Luku. Pia nawapongeza sana kwa sababu area hii ya ukusanyaji wa kodi ilikuwa imeleta shida, Halmashauri zilishindwa kukusanya, lakini TRA pia walivyopewa walishindwa kukusanya. Kwa hiyo, kwa kuja na wazo hilo, nawapongeza sana. Naomba mawazo hayo wayapeleke pia kwenye land rent, waweze kutafuta utaratibu ambao viwanja ambavyo vimepimwa nchini kwetu Tanzania vitaweza kukusanywa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, nawapongeza pia kwa suala la kuja na kodi ya miamala ya kwenye simu na tozo zile kwenye vocha tutakazokuwa tunaweka kwenye simu. Hii inamfanya hata Mtanzania wa hali ya chini aweze kuchangia kodi ya nchi yake. Kuchangia kodi ya nchi, ndiyo utaratibu wa nchi zote duniani. Hii itamwezesha mwananchi kuiuliza Serikali ni kwa nini haijajenga barabara? Ni kwa nini haijaleta maji kwenye eneo? Kwa nini haijajenga kituo cha afya; zahanati pamoja na kuhudumia wananchi kwa ujumla? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuzungumzia Mkoa wangu wa Katavi. Sisi katika bajeti iliyopita tuliahidiwa kujengewa reli kutoka pale Mpanda Mjini kwenda sehemu moja inaitwa Karema ambako kuna bandari ambayo itakuwa inapokea mizigo kutoka Kongo. Naomba tu hili zoezi la ujenzi wa hiyo reli lisiishie kwenye karatasi, litekelezwe ili wananchi wale wa Mkoa wa Katavi waweze kufanya biashara kwenda Kongo na pia Taifa letu la Tanzania liweze kupata kipato kutokana na ushuru utakaotokana na wale wafanyabiashara ambao watapitisha mizigo yao. Maana yake hiyo reli ikiisha, mzigo utakuwa unatoka Dar es Salaam unapita Tabora - Mpanda mpaka kwenye Bandari ya Karema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuliahidiwa barabara ya lami kutoka pale Mpanda Mjini kwenda kwenye hiyo Bandari ya Karema. Naomba pia Waziri wa Fedha asije akatusahau. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii pia kupongeza miradi iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, kama Mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge. Ni umeme ambao utauzwa mpaka nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)