Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Mariam Madalu Nyoka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama na kuchangia bajeti ya Serikali leo hii. Pili nimpongeze Mheshimiwa Rais Mpendwa, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo anaendelea kuzifanya. Pia, niipongeze Wizara ya Fedha ikiongozwa na Waziri wake Mheshimiwa Mwigulu Nchemba pamoja na timu yake kwa bajeti nzuri ya Serikali na bila kusahau Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Daniel Sillo kwa bajeti yao nzuri ambayo imeendelea kutekelezeka na hatimaye kufikia muafaka hapo itakapopitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni bajeti ambayo itaondoa changamoto nyingi za wananchi wetu wakiwemo wananchi wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wachimba madini na makundi mengineyo. Pamoja na haya ninaomba nieleze kwamba, wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo Serikali hii haiwezi kutekeleza miradi yake bila wananchi hawa kulipa kodi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni eneo la miradi ya maendeleo viporo, eneo la pili miradi ya kimkakati na eneo la tatu ni eneo la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye eneo hili la miradi ya kimkakati. Miradi hii lengo la Serikali kuleta miradi ni zuri sana ambalo litaiwezesha kila Halmashauri kutekeleza miradi yake yenyewe wakati huo wakiwa wanajielekeza katika kukuza uchumi wa kila Halmashauri yake. Pamoja na lengo hili, dhamira ya Serikali ni nzuri, lakini utekelezaji wa miradi hii kule kwenye Halmashauri imekuwa ni kinyume na matarajio ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali wakati wa kufanya upembuzi yakinifu wa miradi hii ni vema tukawashirikisha wanancbhi wetu wa maeneo yale pamoja na wadau wa maendeleo wa kila eneo husika. Eneo hili la miradi ya kimkakati lina changamoto zake nyingi sana, changamoto hizo tumeona wakati miradi hiyo imeshakamilika na kuanza kutumika. Tukija mfano wa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Songea Mjini, Mheshimiwa pale kuna changamoto kubwa sana. Mradi mkubwa wa kituo cha mabasi umejengwa lakini mradi huu unashindwa kufanya kazi vizuri kulingana na ushirikishwaji wa wananchi wa maeneo yale pamoja na wadau wake wa maendeleo wa Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini ya kwamba, kama tungewashirikisha wananchi katika utekelezaji wa mradi ule, eneo lile la mradi uliojengwa kilometa 21 kutoka Songea Mjini usingejengwa mradi ule kule, badala yake mradi huu ungejengwa kwenye eneo rafiki na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma. Kwa kweli, wakati wa utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo ni vema dhana ya ushirikishwaji wa jamii iwe ni nyenzo muhimu katika dhana nzima ya utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye eneo la miradi viporo. Kwanza niipongeze Serikali kwa dhamira yake nzuri ya kuweza kubadilisha eneo la Kanuni ya 21, Fungu Namba 439, ambalo changamoto hizo zitaondolewa kwa kutorejeshwa fedha katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na badala yake fedha hizi zitatumika kuendeleza miradi ya maendeleo kama ilivyopangwa. Changamoto hii tumekuwa tukiipata kila mwaka kwenye kila Halmashauri, inapofika tarehe 30 ya Juni ya kila mwaka fedha hizi hurejeshwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na badala yake miradi ile husimama au kutoendelezwa kabisa kwa changamoto ya kuwa hii imekuwa ni miradi viporo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuondoa changamoto hiyo na sasa miradi yote ya maendeleo itakuwa inatekelezwa kama ilivyopangwa. Niiombe Serikali sasa kuhakikisha ya kwamba, miradi yote ambayo imeanza kutekelezwa ikamilishwe kama ilivyopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye eneo la ajira. Ajira ni changamoto hapa nchini. Kwa kipindi hiki chote ambacho tuko hapa Bungeni ninaamini ya kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Wabunge wamepigiwa simu na wananchi wao wakiomba kupata msaada wa kupata ajira. Wakati huo changamoto hii tunaweza kuitatua tu kama Serikali yetu itaweka uwiano wa ajira kwa kila Mkoa kwa kuzingatia sifa au vigezo vya muombaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu nchi yetu hii ni kubwa sana, lakini wananchi wake wengi wapo maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi. Hivyo, basi niiombe Serikali hii iweze kuhakikisha kwamba, wananchi walioko vijijini na maeneo ya pembezoni wanapatiwa ajira badala ya wananchi wale kuona usumbufu kubakia kule vijijini na kuona ni vyema waje mjini kwa ajili ya kutafuta ajira hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)