Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon Toufiq Salim Turky

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpendae

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujaalia uzima tukafika katika Bunge hili. Halikadhalika naomba tumwombee dua Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Ghati amepata ajali na yuko mahututi, lakini tumwombe Mungu amjaalie shufaa aweze kurudi katika Bunge hili tuwe nae pamoja. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Turky, ngoja tuelewane vizuri. Taarifa kuhusu wagonjwa na vifo hutolewa na Kiti. Kabla Kiti hakijatoa maelezo usije ukasema hapa mgonjwa yuko mahututi kumbe sio mgonjwa. Kwa hiyo tafadhali, hayo maneno yaondoke, madam Kiti hakijatoa bado Taarifa.

MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, nafuta hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii tumuombee mzee wetu Hayati Kenneth Kaunda alikuwa katika waasisi wa Bara letu hili la Afrika. Alikuwa pamoja na mzee wetu Mwalimu Nyerere katika kuwakomboa Waafrika wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuja na bajeti ya namna yake. Kwa kweli bajeti hii imewagusa karibu Watanzania wote, tukisema wote pamoja na wa visiwani. Kwa kweli, mwenyewe nimeshaenda kwenye vikao tofauti katika Baraza la Biashara Zanzibar, Baraza la Biashara la Taifa la Bara na katika kilio kikubwa sana kilikuwa ni kilio cha VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Fedha kwa kuona kilio cha Watanzania. Watanzania sisi ni ndugu tuna ushemeji kila mkoa kutokana na kwamba, kuna Wasukuma wako Zanzibar, wako Wagogo Zanzibar, wanakuja kule kutembelea kwetu, wanaona TV, wanaona blender, wakichukua wanalipishwa VAT, wakija zao bara wanalipishwa VAT Bara, lakini hiki kilio cha Watanzania kimeonekana. Hongereni mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika tunafahamu Watanzania wengi waliokuwepo ni wajasirimali na wafanyabiashara wadogo wadogo. Kama hatujabuni miradi tofauti basi Watanzania tutabakia kuwa na vibaka au wakawa waporaji. Leo kwa kupitia punguzo la bodaboda hizi faini peke yake, basi imeleta hamasa ndani ya nchi watu wameweza kufanya kazi zao ipasavyo. Ilikuwa ni juzi wakati inasomwa bajeti nilikuwa na Mheshimiwa Shabiby wakati linaongelewa suala la kupandisha mafuta bei, akasema sasa haya mafuta yameshapandishwa, nikamwambia kwani unadhani zile pesa za TARURA za 500 zingetoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Wizara ya Fedha na Mipango kuja na ubunifu wa kutafuta vyanzo tofauti vya kuleta maendeleo ndani ya Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda sana kuongelea suala zima la forodha ndani ya Afrika Mashariki. Hivi karibuni nilimwona rafiki yangu, Mheshimiwa Bashe akienda zake Namanga kwenda kupigania masuala ya mahindi. Tukajiuliza, kwani hii kazi ya Waziri au ya Wizara? Kulikuwa kuna itifaki ya Forodha ya Afrika Mashariki. Katika itifaki hii ilipaswa kila mwanachama atoe wajumbe watatu. Mjumbe mmoja ni Mwanasheria, anatakiwa Afisa wa Forodha halafu pia anatakiwa na Afisa wa Biashara. Toka 2005 itifaki hii kupitia Ibara ya 24 ya Biashara inatakiwa kuwe na Kamati ya Biashara ambayo inatatua changamoto hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya au nzuri wakaongezeka wanachama wawili wengine Burundi na Rwanda, ikabidi ifanyike amendment. Miaka 15 imechukua kubadilisha amendment. Kwa bahati nzuri amendment imekamilika, kinachohitajika sasahivi ni kupitisha katika Mabunge yetu kuhakikisha hii Itifaki ya Forodha inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo naomba sana kupitia Bunge hili la Kumi na Mbili kuweka historia kuwa Itifaki ile ya Forodha tumeweza kuipitisha na tukawa katika mstari wa mbele kidiplomasia kushawishi wanachama wenzetu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi kupitia Mabunge yao kuhakikisha ile itifaki inapitishwa. Baada ya hapo tutakuwa na Kamati sasa inayotatua haya masuala ya NTBs. Haiwezekani leo kuona tuna changamoto ya bidhaa fulani mtu anatoka katika Wizara yake anakwenda kutatua, anaenda mipakani na wakati tayari tumeshajipangia inawezekana kuwa na Kamati ya Biashara kutatua changamoto hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaelekea katika AfCFTA ukanda wa Afrika nzima kuwa na biashara huru wakati East Africa pekee mpaka sasa hivi tunatafuta Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu waende kutatua matatizo haya. Kusema ukweli ile ndoto ya kuwa na Ukanda wa Afrika ya Biashara Huru, basi itakuwa ni ndoto tu. Kwa hivyo, nawaomba sana tuipitishe itifaki hii kuhakikisha Kamati ya Biashara inafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nataka niongee kidogo kwenye suala la ufugaji. Tanzania sisi ni wa pili katika kuwa na wanyama (cattle) wengi. Hata hivyo, ukitazama value katika wanyama hao, yetu iko chini mno.

Nimetazama kuna Mabara ya Japan wana steak inaitwa Wagyu, kuna wenzetu kupitia Scotland wanaitwa Angus. Ile nyama kilo moja inaweza kufika mpaka dola 200 sawasawa na ng’ombe mzima tunayeuza sisi. Sasa hebu tuwasaidie wakulima wetu kuhakikisha tunakuwa na prime steak pia. Leo katika hoteli zote za nyota tano nyama zinatoka Afrika Kusini, Argentina, New Zealand na sisi bado nyama zetu haziko katika quality za kuwepo katika five Star properties. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani hata siku moja tuwe wa pili katika Bara la Afrika na nyama zitoke nchi nyingine kwa sababu kiwango chake bado hakijafikiwa. Naiomba sana na naishauri Wizara husika kuhakikisha tunaelimisha wafugaji wetu kuweza kuwalea ng’ombe, mbuzi na wanyama wetu kuhakikisha wanakuwa wa kiwango, sio tu kwa kutumika kwenye hoteli zetu lakini kupitia ukanda mzima wa Afrika na dunia kiujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)