Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naungana na Wabunge wenzangu kuchangia kwenye bajeti hii ya 2021/2022. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Baraza zima la Mawaziri pamoja na Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru sana Serikali kwenye suala hili la barabara baada ya kukubaliana na kilio cha Wabunge na kuweza kutenga pesa hasa upande wa TARURA. Nashukuru sana kwa sababu kama kilio cha Wabunge wote kilivyokuwa, ilikuwa ni tatizo kubwa sana kwenye maeneo yetu, nami mwenyewe kwenye Jimbo langu la Kahama nilikuwa mwathirika mkubwa sana wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara naomba kushauri kidogo kwamba zamani mpaka miaka ya 1990 barabara zilikuwa na mtu anaitwa Road Surveyor ambaye alikuwa anaamka asubuhi akiwa na baiskeli; mmoja anakwenda upande mmoja kilometa tano, mwingine anakwenda na baiskeli kilometa tano akiwa amebeba koleo au jembe akiangalia zile sehemu ambazo barabara imeumia. Hii ilisaidia sana barabara zile kuendelea kutibiwa yale maeneo ambayo madogo madogo yanaoonesha ubovu, lakini baadaye watu hawa waliondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wenzetu wa TARURA, kama wanaweza kuwarudisha tena. Maana yake kwa sasa hivi kwenye maeneo yetu TARURA inakuwa na wafanyakazi wawili au watatu. Kwa wingi wa barabara, haiwezi kuzi-repair zile barabara mpaka mwakani. Kama unaweza kuwarudisha watu hao na leo tuna pikipiki, inaweza ikatusaidia sana kuliko kusubiri mpaka barabara zote zimeharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wetu ni kama tembo aliyebebwa na sisimizi, lakini tembo huyu huwa hafahamu kama amebebwa na sisimizi. Mara nyingi akipata shida kidogo huwa anapenda sisimizi watoke. Nasema hili nikiangalia hili suala la machinga. Sisi ambao tunatoka maeneo ambayo miji yetu haina ajira rasmi; kwenye Jimbo langu watu walioajiriwa na mishahara kabisa katika watu 500,000 hawafiki watu 5,000; na wenye mshahara ambao unaweza kutosha kutoka tarehe 1 mpaka 30, hawafiki 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali inavyoendelea, Mheshimiwa Waziri inaonekana kama kuna mchaka mchaka dhidi ya machinga au wafanyabiashara wadogo wadogo kuja kuondolewa kwenye maeneo yao. Watu hawa tumekuwa nao zaidi ya miaka mitano, wametusaidia sana kwenye shughuli za kibiashara na wame-stable na wamepata ajira. Leo kama tutaona kwamba tuwatoe, linanipa shaka sana kwa sababu watu hawa wamesaidia sana maeneo mengi hasa kwenye shughuli za wakulima. Bidhaa wanazouza ukiacha zile za nje ni bidhaa za wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo viazi ulaya kwa wenzetu wa Kusini wameongeza ukulima mara tano zaidi lakini aliyesababisha viazi ulaya viende ni Mama Ntilie. Kwa sababu, leo huwezi kuipika chipsi nyumbani kwa sababu ukipika chipsi unahitaji zaidi ya lita mbili za mafuta, lakini mama ntilie na machinga wameendelea kupika chipsi hizo na kusababisha ulaji mkubwa sana wa viasi. Sasa sijui wenzetu wateule nini hasa kinachowabuguzi, maana yake leo mahindi wanayochoma ni mahindi ya wakulima, ina maana wamemsaidia mkulima na wao pia wamepata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanauza miwa wanaikatakata wanaikamu miwa wanawasaidia wakulima wetu lakini na wao wanapata ajira. Nafikiri wachumi wetu wajaribu kwenda kwa data ndani zaidi, leo hii ukiangalia uuzaji wa kuku wa kizungu, waliosababisha ulaji wa kuku leo, siyo matajiri wala siyo watu wa hali ya juu, walio sababisha ni watu wa hali ya chini ambao mpaka wamewezesha watu kula utumbo wa kuku. Kwa sababu, leo wanaweza kumkatakata kuku mpaka shilingi 400, 500 kwa hiyo wamepeleka biashara hiyo na wamefanya nyie mnachosema kitaalamu wame add value nafikiri hawa ndiyo walio add value kuliko mtu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea Serikali ikawape motisha lakini kama Serikali inang’ang’ana kwenda kuwatoa au kuwakataa na vijana wetu waliomaliza shule wote tunategemea waende kwenye kazi ya machinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye majimbo kama ya kwetu ambayo yameathirika sana na shughuli za migodini, ukiondoa wale wajane ambao wako kwenye Biblia na Quran, sasa hivi tuna wajane ambao wametelekezwa na wanaume na wana watoto kuanzia wanne mpaka watano mpaka saba, shughuli zao hawa wakinamama ni shughuli hizo hizo ndogo ndogo. Serikali yetu haina utaratibu wowote wa kumsaidia mjane, haina utaratibu wowote wa kumsaidia mama aliyetelekezwa na ana watoto atafanya nini unapomtangazia kiama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rahisi sana mtu ambaye anamaisha mazuri kutamka, kwamba machinga wanaleta uchafu, nirahisi sana lakini machinga wamekwenda Oyster Bay wanatamuuzia nani? Hakuna machingia ambaye yuko Oyster Bay, hakuna mashinga ambaye anakwenda Masaki, kama wako Kariakoo sisi wenye hali nzuri ndiyo tumewafuata, tumeenda kutafuta nini kule kariakoo? Maana sisi tuna maduka yetu kule Oyster Bay yapo, sisi tunaenda kutafuta nini Je, tunaripoti yoyote yenye lawama zidi ya wenye duka na machinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama sisi Kanda ya Ziwa hatuna ugomvi wa Wafugaji na Wakulima kwa sababu sisi tunazo ng’ombe zaidi ya miaka 200, lakini ugomvi uko kule Morogoro ambako wafugaji wameenda mara ya kwanza lakini machinga, hawajawa na ugomvi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kinanipa kigugumizi ni nani hasa ambaye anawaza kwamba hawa watu hawafai. Baada ya uhuru tulikuwa na wahindi na wa-Asia na waswahili kwenye miji yetu, lakini mwaka 1980 baada ya kuvunjika ujamaa na viwanda collapse watu walibaki kule mjini, hawa wamezaliwa kule mjini baada sehemu hiyo imevutia, tena watu wameenda kukaa kule, hii ni kabila mpya imeonekana mjini, hawa watu hawawezi kulima, hawawezi kufuga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, tunataka waende wapi hasa, labda Serikali wakati wa kuhitimisha watupe jibu kwamba watu hawa wanatakiwa kwenda wapi? Hawawezi kulima, hawajawai kulima, wamezaliwa mjini hata kabila zao ukiwauliza wanasema kwetu Mwanza, kwetu Moshi lakini hajawai kufika Mwanza utawafanya nini? Nafikiri wateule wetu wajaribu sana kuwa wabunifu, watu hawa ni resources nzuri sana ya uchumi, nzuri sana wamefanya mabadiliko makubwa mno ya uchumi ila uwezi kuyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye watu wa Mpesa sehemu zinazoongoza kwa kutuma Mpesa ni maeneo ya machinga peke yake ndiyo wanaongoza kwa kufanya biashara, hizi biashara bidhaa zote wanazouza, si Serikali amepata kodi. Lakini wao wanamlazimisha mtu kila mtu anatembea wanamlazimisha ina maana kazi wanayofanya ni kazi ngumu sana, sasa ni ajabu kama sisi tunaenda kungangana kuwatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, machinga ndiyo chuo kabisa original cha kutoa wafanyabiashara leo Watanzania, je, hii ya kwenu CBE imewahi kutoa mfanyabiashara yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana tunakwenda kufunga chuo ambacho kinatoa watu original, tunaenda kufungua vyuo ambavyo havitoi wafanyabiashara tunaomba sana wenzetu hasa Mheshimiwa Waziri alifikirie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)