Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii nami kuweza kuzungumza kwenye Bunge lako hili Tukufu. Nitoe pongezi zangu za dhati kwa Waziri Mheshimiwa Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri, rafiki yangu Mheshimiwa Hamad Masauni, bila kuwasahau Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na wataalmu wote wa Wizara hii ya Fedha na Mipango kwa uandaaji na uwasilishaji mzuri wa taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, niende moja kwa moja. Kwenye wasilisho langu nitazungumzia zaidi kuhusiana na uchumi. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina uchumi wa Muungano. Uchumi huu unajumuisha na uchumi ule wa Zanzibar, ndiyo maana kila taarifa ya mwezi kutokea BoT inatambua uchumi wa Zanzibar, lakini utaratibu huu hautumiki pale ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapowasilisha taarifa zake za kifedha kule nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye mataasisi ya kifedha, kwa mfano IMF na World Bank, taarifa hizi haziendi moja kwa moja kwa sura ya kipekee ya kuitambua kama Zanzibar, isipokuwa inatambulika kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Utaratibu huu unaleta madhara makubwa sana kwa uchumi wetu wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, hivi karibuni tu tulitoka kwenye janga kubwa la Corona, Tanzania nayo pia imeathirika kwenye janga hili la Corona, lakini Zanzibar nayo imeathirika zaidi kwenye janga hili. Ukiangalia Zanzibar, uchumi wake mkubwa sana asilimia 82 pato lake la Taifa inategemea kupitia utalii, lakini Bara ni asilimia kama 17 hivi na kidogo ndiyo inategemea utalii. Kwa hiyo, madhara haya yanakuja kutokezea endapo hizi taasisi za kidunia; World Bank, IMF yanapotoa fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi ambazo zimeathirika kifedha, inaleta madhara makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna nchi zetu za karibu hapa kwa mfano Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika, zimepata misaada kifedha, lakini Zanzibar haijaonekana. Kwa sababu uwasilishaji wa taarifa za kifedha kupitia World Bank pamoja IMF, Zanzibar haitambuliki. Hivyo Mheshimiwa Waziri, pamoja na Naibu Waziri, nawaomba sana, tunapopeleka taarifa zetu za kifedha, basi lazima tutambue Zanzibar nayo ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii makusanyo ya fedha ambayo yamepatikana Zanzibar kwa miaka miwili ambapo Zanzibar imeathirika zaidi na Corona, ndiyo maana kufikia kile kiwango cha fedha kwenye bajeti ni asilimia kama 70 tu, mpaka sasa hivi Zanzibar ndiyo ishaanza kupitia tozo tofauti tofauti. Kwa hiyo, hali hii ina athari kubwa sana.

Kwa hiyo, naiomba sana Wizara, tunapowasilisha taarifa zetu za kifedha nje, basi tupeleke taarifa zetu ambazo zitakuwa na sura ya Kizanzibar. Hii itasaidia sana. Naiomba sana Wizara tuzingatie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo lingine la wafanyabiashara. Kuna wafanyabiashara wapo Tanzania Bara na wengine Zanzibar. Changamoto ambayo tunayo, tuko kwenye nchi moja; wapo wafanyabiashara ambao wapo Bara ambao tayari wame invest kwa eneo kubwa, lakini wapo pia Wazanzibar ambao wame-invest kwa eneo kubwa. Changamoto inayopelekea Mzanzibar au Mtanzania wa kutoka mainland kwenda kuwekeza bara au wa labda wa Zanzibar akija bara wa bara akienda Zanzibar kunakuwa na changamoto namna ya kupata leseni. Akienda Mzanzibar, Mtanzania anaonekana kama foreigner. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Wizara, hii ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wanapokuwepo wafanyabiashara ambao wamekuwa interested na kuja ku- invest aidha pande hizi mbili za Muungano, basi kuwe kuna exemption ya kuweza kumtambua kama Mtanzania; iwe baadhi ya kodi asikate, asirejee tena kwa ajili ya kukata leseni. Akija Zanzibar, basi apate exemption ndogo au hata atambulike. Isipokuwa anaweza akachangia kodi kutokana na mazingira gani ambayo anafanyia biashara. Hii itasaidia sana; mojawapo linaweza likakuza uchumi wetu wa Tanzania pamoja na kuu-boost.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, itatengeneza ajira kwa vijana wetu; na tatu, itatengeneza variety commodities pamoja na production. Hii itasaidia sana. Leo hii Mzanzibar akija Bara, anaanza process upya kwa ajili ya kupata leseni. Tuondoe hivi vikwazo ili tutanue wigo wetu sasa wa kukusanya kodi, lakini pia angalau tuonee huruma wafanyabiashara wetu waweze kuwekeza wanapokuja upande wa pili wa Muungano. Hii itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, naipongeza sana Wizara kwa kulitambua hili kwamba sasa hivi makusanyo ya visa ya pande zote mbili za Muungano, basi upande ambao utapata fedha, itasaidia sana. Hii itainua uchumi wa Zanzibar, ambao kwa asilimia kubwa sana tunategemea uchumi wa vitu vidogo vidogo. Sasa tukiweka mwanya huu, itasaidia sana ku-boost ule ukusanyaji wa pato kupitia hii visa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi zetu hizi mbili, huko nyuma tulikuwa tunakusanya zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya visa, lakini sasa hivi Mheshimiwa Rais ameliona hili jambo. Kwa hiyo, kutawanya hizi visa itasaidia kwa upande wetu Zanzibar na pia kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maana kwamba huku Bara nao pia wataweza kukusanya fedha vizuri kwa kupitia hii visa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nampongeza sana Mheshimiwa Mama Samia kwa kuidhinisha pesa kila Jimbo kwa ajili ya Mfuko wa TARURA. Naiomba sana Wizara hii ilichukue jambo hili, ituangalie na upande wa pili wa Zanzibar, isiwe wenzetu tu, Watanzania Bara ndio wanaonufaika na huu mfuko wa fedha, bado na sisi kwa upande wetu wa Zanzibar tuna changamoto kubwa. Shilingi milioni 500 ukinipatia kwenye Jimbo langu, utaenda kunisaidia sana na kuwasaidia akinamama ambao sasa hivi wanatembea masafa marefu kwa ajili ya kupata huduma ya afya, akina mama ambao wanabebwa kwa vitanda kama Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba alivyozungumza hapa, watatusaidia sana sasa hivi kusafirishwa kutoka sehemu walipo kwenda hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo, machache naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)