Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Serikali. Kwanza kabisa ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya njema, nimeweza kusimama hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeisikia bajeti iliyoletwa na Mheshimiwa Waziri, yapo maeneo ambayo niseme yamefanya vizuri, lakini yapo maeneo ambayo yana changamoto na inabidi zifanyiwe marekebisho kutokana na mapendekezo ya Wabunge na michango ya Wabunge inayoendelea katika Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia kwenye suala zima la wafanyabiashara na TRA, hii imekuwa ni changamoto kubwa sana na ya muda mrefu, kwa wafanyabiashara kugongana na watendaji wa TRA, lakini naamini baada ya kauli ya mama, lakini pia katika bajeti hii inaonyesha sasa wafanyabiashara wanakwenda kufanyabiashara zao kwa utulivu, kwa amani na kwa salama zaidi kuliko ilivyokuwa hapo nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo nyuma ilikuwa mfanyabishara ana wasiwasi na mteja akiingia dukani anajua huyu sijui katumwa, huyu sijui namna gani, lakini mwisho wa siku sasa wafanyabiashara wamekuwa na amani na biashara zinaenda kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii pia imezungumzia maslahi ya wafanyakazi. Kimekuwa ni kilio kikubwa sana kwa Waheshimiwa Wabunage wengi wanaposimama kuhusiana na maslahi ya wafanyakazi. Jambo hili limeonekana na niseme tu bado kuna vitu vidogo ambavyo vikifanyiwa marekebisho naamini kabisa wafanyakazi wetu nao sasa watafanya kazi kwa amani na mambo yao yataenda vizuri kama ambavyo wamekusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Ubunge lakini pia mimi ni mwanamichezo. Niseme tu kwamba Serikali imeondoa kodi kwenye hizi nyasi bandia, lakini kwenye hili naomba niiambie Serikali isiondoe kodi hizi kwenye majiji peke yake kwa sababu ukiangalia majiji yako sita tu na majiji mawili tayari yanavyo viwanja vyenye nyasi bandia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye hili nashauri kwamba, iwe ni kwa nchi nzima kwa sababu mimi natokea Mkoa wa Tabora. Pale katika Mkoa wetu wa Tabora tuna kiwanja chetu cha Ali Hassan Mwinyi, kiwanja kile ni kikubwa, kiwanja kizuri, lakini kimetelekezwa, kimeachwa kwa muda mrefu sana. Ni imani yangu hizi nyasi bandia zikiletwa, angalau na sisi pale Tabora sasa tutaweza kucheza michezo mizuri hata hii michezo ya ligi kuu itakuwa inaletwa katika uwanja wetu pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe tu na nishauri kwa Serikali, utaratibu wa vibali basi wawape BMT ili waweze ku-control uagizaji wa nyasi hizi hili kusiwe na vurugu ya hapa na pale ya wafanyabiashara kutaka kuweka mambo yao mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuishauri Serikali, hizi fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika maeneo yetu tungeomba sana zisiwe kwenye makaratasi. Fedha hizi ziende ziende zikafanye kazi ambazo zimekusudiwa. Leo mimi hapa ninavyozungumza katika Mkoa wetu wa Tabora tumeletewa maji ya Ziwa Victoria. Maji yamefika lakini bado hayajasambazwa kwa wananchi, kwa hiyo niombe sana fedha hizi zipelekwe ili ile miradi ambayo inahudumia wananchi wengi iweze kufanyika, baada ya bajeti hii watu waweze kupata ile huduma ambayo inatakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama ambavyo tumeshauri kwenye bajeti za Wizara mbalimbali kuna masuala ya zahanati, Vituo vya Afya, hospitali za wilaya kwenye wilaya ambazo hatuna hospitali za wilaya, tungeomba sana fedha hizi ziende na zikawe kipaumbele ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora kama ambavyo mama amepanga na anataka huduma hizi zifanyike hasa huko chini zikiwepo huduma za afya, elimu na maji. Kwa hiyo naomba sana fedha hizi zisiwe kwenye makaratasi za kufurahisha watu lakini ziende sasa zikafanye utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la ushirikishwaji wa Wabunge wa Viti Maalum katika fedha zinazopelekwa za miradi ya maendeleo kwenye maeneo yetu. Wabunge wa Viti Maalum tumekuwa vinara wakubwa wa kueleza changamoto zinazotukabili katika mikoa yetu na maeneo yetu. Kama unavyofahamu sisi Wabunge wa Viti Maalum tunatumikia mikoa sio majimbo peke yake na tunapozungumza hapa tunazungumzia mikoa yetu na sio majimbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo changamoto zinazoletwa katika Bunge zinapokelewa, zinachukuliwa, katika utekelezaji wake Wabunge wa Viti Maalum tunawekwa pembeni. Juzi zimepelekwa shilingi milioni 500 kwenye kila jimbo, Wabunge wa viti maalum hatujashirikishwa. Juzi nimemsikia wifi yangu Ummy Mwalimu akizungumzia kuhusiana na fedha zitakazokwenda kujenga mashule, katika majimbo. Mheshimiwa Ummy amesema kwamba watakaa na Wabunge wa Majimbo ili waweze kuona ni kata zipi ambazo zitakwenda kupeleka hizo shule.

Sisi wanawake wa Viti Maalum tumeshiriki kwa namna moja ama nyingine kuzungumzia changamoto zilizopo za mashule, tunaomba tushirikishwa na sisi hili tuweze kusema kwamba wapi shule hizi ziweze kupelekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkoa wangu una majimbo 12 Wabunge wa viti maalum tupo watatu inashindikana nini kutuingiza kwenye hizo fedha hili na sisi tuweze kushiriki katika fedha hizi za maendeleo ambazo tunazipigania hapa Bungeni. Jambo hili kwa kweli linaumiza na niseme tu linaonyesha kwamba kama Wabunge wa Viti Maalum hatuna chochote ambacho tunatakiwa kukipata. Wabunge wa majimbo wana fedha za majimbo wanapata, wanafanya kazi, Wabunge wa majimbo miradi ya maendeleo inayokwenda wanapewa inakwenda kufanya kazi, sisi Wabunge wa Viti Maalum tunatumia fedha zetu wenyewe kufanya majukumu yetu na kutekeleza majukumu yenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinapofika kipindi cha kampeni, Wabunge hawa wa majimbo wanatutegemea sana sisi Wabunge wa Viti Maalum tuwasaidie kwenye kampeni ndio wanashinda majimbo hayo. Wasituogope tunakwenda kufanya kazi pamoja ili tuweze kuleta maendeleo katika maeneo yetu. Naiomba sana Serikali, sisi ni Wabunge, tunaomba itushirikishe na sisi tunahitaji kufanya maendeleo katika maeneo tunayotoka na ndio maana tumekuwa tukichangia sana kuhakikisha kwamba maeneo yetu, barabara, miundombinu ya hospitali, shule na kila kitu tunaizungumzia hapa. Kwa hiyo ningeomba sana tushirikishwe, fedha za maendeleo zinapokwenda na sisi tuwe ni sehemu ya fedha hizo kwa sababu tunaziombea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nikizungumzia sana kuhusiana na sekta ya viwanda kipindi cha bajeti za nyuma. Niseme tu kwamba, bado tuna changamoto kubwa sana katika sekta hii. Bado ni baadhi ya viwanda vichache tu ambavyo vinaweza kutoa kodi kubwa kwa Serikali tofauti na ambavyo tunaambiwa viwanda vilivyo vingi. Kwa hiyo ningeiomba Serikali na kuishauri kuangalia namna bora ya kuwezesha viwanda hivi ili viweze kuwa na tija katika Taifa letu kwa kuongeza kipato cha Taifa letu kwa maana ya kuongeza pia kodi za makusanyo ya kila mwaka katika nchi yetu. Naomba sana sekta hii ya viwanda iangaliwe vizuri, kwani ni sekta kubwa ambayo inaweza ikawa na mchango mkubwa sana katika pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kidogo suala zima la sekta ya utalii. Zipo changamoto kidogo katika sekta hii. Ni sekta ambayo Serikali inategemea kuleta kodi na kipato kwa Serikali, lakini ina changamoto kubwa sana katika maeneo mbalimbali ya hifadhi zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto za miundombinu katika baadhi ya hifadhi zetu. Hiyo inapelekea kukwamisha watalii wengi kuweza kufika katika maeneo yetu. Bado tuna changamoto pia ya kuona ni namna gani tunavyoweza kuboresha maeneo yetu ya utalii kwa ujumla yaweze kuendana na hali halisi ambavyo watu wanaisikia Tanzania na utalii jinsi ilivyo. Kwa hiyo, naomba sana katika bajeti hii tuweze kuboresha kwenye sekta hii ya utalii ili basi sekta hii iweze kuongeza pato zaidi ambalo limekuwa likipatikana kwani sekta hii inategemewa sana na nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)