Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii nami nipate nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii ya Makadirio ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi aliyonipatia kuweza kuzungumza tena siku ya leo katika bajeti hii kuu. Mwanzo kabisa niipongeze sana hotuba ya bajeti kuu iliyosomwa hapa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, akimwakilisha Rais na mimi naunga mkono hoja hii kwanza kabla hata sijazungumza kwa sababu yapo mambo mengi mazuri yaliyooneshwa kwenye hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shabaha za uchumi zilizoelezwa kwenye hotuba tunayoizungumzia hapa ni kuongeza kasi ya ukuaji wa kiuchumi kutoka asilimia 4.7 tuliyokuwa nayo kwenda kwenye asilimia 5.6, lakini vilevile imeonesha wazi kwamba tunataka kwenda kwenye asilimia 6.3 mwaka 2023 lakini mfumuko wa bei tunataka uwe kati ya asilimia Tatu (3) na asilimia (5) kwa mwaka huu. Vilevile mapato ya ndani tunataka yaongezeke na mapato ya kodi tunataka yaongezeke sasa inaonekana kuna kazi kubwa sana ya kufanya kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mahsusi ambayo matarajio yetu makubwa ya ukusanyaji wa kodi hii yanatakiwa yawafikie nayo ni barabara za mijini na vijijini TARURA, kuna maji safi na salama, kuna bima kwa wote, kuna habari ya shule tunatakiwa tujenge shule, ukienda kwenye afya tu unaona kuna maboma ya zahanati karibu 8,000 yanahitaji kukamilishwa. Lakini ukienda kwenye vituo vya afya hotuba hii inaonesha kuna vituo vya afya zaidi ya 1,500 vinatakiwa kukamilishwa kwa hiyo ni dhahiri kwamba tunahitaji fedha ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia vyanzo vyetu vya fedha ukiviangalia vya mwaka jana na mwaka huu vimebadilika kidogo sana japokuwa inaonekana kuna hii tumezoea kusema indirect tax, hii kodi ya LUKU iliyoongezeka na inayotoka kwenye LUKU mwa maana ya majengo (property tax), lakini na hii nyingine iliyoongezeka kupitia kwenye mitandao ya simu kwa matumizi ya siku tulizonazo. Ukiona kuna Trilioni Mbili imeongezeka hapa lakini tukiangalia kwa uhalisia vyanzo vile ukiangalia kwa percentage tumeongeza tu mapato ya ndani ya kodi kwa asilimia 72 vingine vimebaki kama vilivyokuwa tumepunguza kule kwenye mikopo ya ndani na ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hoja kubwa tuliyonayo ni ukusanyaji wa mapato, kwamba kazi kubwa tuliyonayo hapa ni ukusanyaji wa mapato lakini ukiangalia mikakati iliyowekwa kuna ile EFD Management System, kuna habari ya kuhakikisha kwamba ile blue print inatekelezeka na uwekezaji mwingine ambao tunauona kwenye maeneo hayo. Binafsi niishauri sana Serikali iongeze nguvu katika ukusanyaji wa kodi ni kweli tumesema tutakusanya kodi sahihi kwa sheria sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuongeze sana eneo hilo kwa sababu kama hatutakusanya kodi ya kutosha haya ambayo tunayaona leo kama hotuba nzuri sana tutakapokutana tena kuijadili tutaanza kulaumiana sisi kwa sisi, kwa nini. Nina mfano mzuri wa mwaka jana, tulikuwa na hotuba ambayo inaonekana imeandikwa kama nilivyosema inatofautiana kiasi na hii lakini nikienda kwenye kilimo, mfano kilimo tu development budget iliyotekelezwa mwaka jana ilikuwa kama 30 percent sasa tunataka kwenda mbele tunataka kuhakikishe kwamba tunakwenda kufanikiwa kusogeza uchumi kutoka asilimia 4.7 kwenda kwenye asilimia
5.6. Hoja ambayo ninaiona kwenye bajeti yetu hapa ambayo ningependa nitoe ushauri kwa Serikali zile sekta ambazo ni za uzalishaji kwenye bajeti hii hazina fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukiangalia percent ya hiyo Bilioni 294 ya kilimo kwenye development budget nzima utagundua ni 0.08 ambayo ni kama asilimia 0.8 haifika hata asilimia moja lakini hiyo inaajiri watu asilimia 65 wa nchi hii na tunataka sasa twende mbele, kama mchango wenyewe ndio huo yaani unataka kitu fulani kitokee lakini input yako ni ndogo kiasi hicho maana yake hata hawa Mawaziri wa Kilimo tulionao watajitahidi kadri wanavyoweza lakini hawataweza, kwa sababu hawana fedha ya kutosha wana mipango mingi tupate mbegu, wana mipango mingi tuanzishe mashamba darasa, tuanzishe tulime Alizeti kwa fedha hii tuliyonayo Bilioni 294 ambayo haifiki hata asilimia moja haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tufikirie ninajua tayari bajeti ipo mezani tutakwenda kuitekeleza lakini matokeo yatakayokuja huko mbele hayawezi kuwa ya kushangaza sana, hatutasogea sana kwa sababu asilimia 65 ya watu ambao tunagemea tuwawezeshe hawataweza na bahati mbaya sana hata viwanda vinawezeshwa na uzalishaji wa kilimo, sasa kilimo hakijawezeshwa vya kutosha maana yake na viwanda havitafanya vizuri, kwa hiyo mwisho wa siku tutakapokuja kuzungumza hapa tutagundua hata hao tunaotaka kuwatoza kodi watakuwa wachache. Kwa mfano, Halmashauri nyingi nchini zinakusanya ushuru wa mapato kutoka kwenye mazao, sasa kama fedha iliyokwenda kwenye kilimo ni kidogo tutakusanya nini kutoka kwenye Halmashauri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawatakusanya sana watakwenda hapo hapo, mwaka huu tumeongeza Bilioni 200 kwenye malengo yetu Je, watazitoa wapi? Kwa sababu hatujachakata kuwaanzishia ili waweze kufanya uzalishaji mkubwa na tukusanye hivyo, vivyo hivyo kwenye uvuvi, vivyo hivyo kwenye mifugo, bado kile ambacho tumekitoa ni kidogo kwa hiyo tuangalie kile ambacho tunakiweka mahali kwa ajili ya kuzalisha, tukiweka kidogo tutapata kidogo na mwisho wa siku tuhakikishe kwamba development budget tunayoipeleka kule iende kama tulivyo i-plan mwaka kesho tutaanza kuulizana tulipanga iende asilimia 100 imekwenda asilimia 25 matokeo yake tutakuwa hatujafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee sehemu ya pili ambayo nilitaka kuizungumzia eneo la madini, tunategemea madini yachangie tufike kwenye pato la Taifa asilimia 10, changamoto ambayo ninaiona sasa miundombinu tuliyonayo binafsi nimekuwa ninazungumzia barabara ya kutoka Geita kwenda Bukoli kupita Runguya kwenda Kahama, hii barabara inapita kwenye migodi, haipitiki sasa! Kama haipitiki hiyo ndio hata makinikia yanayoulizwa humu ndani yanapita barabara hiyo, sasa tutakwendaje kufanya hii shughuli ambayo tunataka kufanya wakati miundombinu haipo? Lakini niseme…

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Magessa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi.

T A A R I F A

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda nimpe taarifa mzungumzaji kwamba barabara hii inayotoka Geita - Bukoli, Bukoli - Kakola, Kakola-Kahama ni barabara ambayo kimsingi iliahidiwa kupewa kiasi cha dola milioni 40 na Mgodi wa Bulyanhulu, fedha hizo bado hazitolewa na Serikali sijui ni kwanini lakini pia barabara hii imekuwa ni adha toka makinikia yameanza kusafirishwa na magari haya yanayobeba makinikia yanatembea makundi kwa makundi gari zisizozidi 40 vumbi limekuwa ni kubwa sana, kwa ruhusa yako…

NAIBU SPIKA: Subiri kwanza unamuongezea mchango kwenye hoja ipi aliyokuwa anazungumza?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya barabara inayotoka Geita - Bukoli…

NAIBU SPIKA: Yeye alikuwa amemaliza kuzungumza hoja yake.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, alimaliza!

NAIBU SPIKA: Au wewe umeamua umalizie ili yeye asimalizie mchango wake?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, alimaliza na nilitaka kumuongezea kwa sababu kwa ruhusa yako nimekuja na sampuli ya vumbi limo kwenye begi humu, nilitaka uniruhusu niweze kumkabidhi ili aliachie humu vumbi aone namna gani wananchi wa Bulyanhulu…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi naomba ukae.

Waheshimiwa Wabunge, kuna nyakati mtu anakuwa ana mtiririko fulani hivi wa mchango wake usimkatishe kabla hajaweka nukta, ukimkatisha maana yake kuna jambo labda anakosea unataka umrekebishe labda yeye kasema 10 kumbe ni tisa, sasa wewe unamkatisha ili wewe ndiyo useme vizuri jambo lake kabla Mbunge hajasema yeye hoja yake, yaani unakuwa kama unaonesha kwamba yeye hajaweza kumalizia hoja yake vizuri wewe ndiyo unataka umsaidie, sasa haikai vizuri kwa hiyo tusubiri awe anamaliza sentensi yake ndiyo wewe uingie hapo.

Waheshimiwa Wabunge, mtu anayetaka kuchangia jamani sisi huwa tunawapa nafasi kama kwenye orodha haupo andika hapa mbele utapewa fursa ya kuchangia, ukimkatisha Mbunge mwenzio hizi zinakaa kwenye Taarifa Rasmi za Bunge kila tunachokizungumza humu ndani, sasa sisi wenyewe tuwekeane mazingira mazuri ya kuachiana nafasi za kuchangia kama hakuna jambo ambalo kweli unataka wewe kuchangia kwenye hiyo taarifa unayotaka kuitoa, maana nimeona wengi huwa unataka kuiseme barabara yako basi unasema hilo lililoko huko na huku hivi hivi ahaha!

Mheshimiwa Magessa malizia mchango wako.

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa hayo ambayo umeyasema. Niseme tu naendelea na hiyo barabara kwamba kumekuwa na mazungumzo ambayo umri wake ni zaidi ya miaka minne ya hiyo dola elfu 40 ambayo wadau kwa maana ya Barrick waliridhia baada ya mazungumzo barabara hiyo ianze kujengwa lakini nashangaa miaka minne Wizara ya Fedha, Wizara ya Madini wanazungumzia nini kwa miaka minne? Kwa hiyo kuna mahali fulani wananchi wanakaribia kupata mafanikio lakini mazungumzo yanachukua muda mrefu sana, kwa hiyo barabara hii imekuwa sasa vumbi kama alivyokuwa anataka kuchangia ndugu yangu hapa, vumbi lake linatisha. Leo hii ukimkaribisha mgeni kutoka Geita ukamwambia njoo Dodoma unitembelee akifika hapa utafikiri umekutana na ninja alitaka kuvamia mahali kwa sababu pua zote zitakuwa zimejaa vumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme wazi kama makinikia yanapita hapo na dhahabu kuchenjua tunategemea ipite hapo nimshukuru nimpongeze sana Mheshimiwa Rais amefungua na amezindua kiwanda cha kusafisha dhahabu refinery pale Mwanza wamesema kuna sehemu itakuwa kwa ajili ya kukopesha wachimbaji wadogo, sasa hii dhahabu tutaitoaje huko Runguya tutaitoaje huko Msalala, tutaitoaje huko Geita ili iende Mwanza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama barabara tu inazungumziwa miaka minne na wadau wanataka kuweka fedha lakini haieleweki inaishia wapi, kwa hiyo niseme wazi ili tuendelee kuzalisha vizuri na dhahabu iendelee kwenda wamesema kuna kilo 400 kwa siku inatakiwa kilo 400 lakini baadaye inatakiwa kilo 900, kilo 400 ni karibu nusu tani, lakini kilo 900 ni karibu tani moja itapatikana wapi hii, lakini nijielekeze tena kwenye kodi…

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)