Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Mussa Azzan Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana, naanza na kauli ya Waziri wa Nishati alipotoa kauli kuwa nchi nzima umeme utakuwa ni 27,000/= lakini kwa Ilala hiyo bei hakuna. Jiulize kwa nini Ilala itozwe laki tatu, laki nne, kuunganisha umeme, lakini nchi nzima mikoa yote ambayo Mwanza, Arusha, wanalipa bei ya chini zaidi ya Ilala; tatizo liko wapi na kwa nini kuna formula kama hiyo kwa kuletewa watu wa wilaya hii yetu ya Ilala? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ada ya tozo ya fire. Tulitoa taarifa yetu ndani ya Bunge kuwa ni kubwa mno, sio kwa mjini tu maeneo yote nchini, tozo ya ada ya fire kwa majumba ya ghorofa ni zaidi ya 250,000 kwa mwaka, ni kubwa zaidi ya kodi ya majengo, kitu ambacho wananchi hawawezi. Tulikubaliana itolewe na ipunguzwe isiwe 250,000 ishuke mpaka 10,000 kwa mwaka kutokana na extraction ambazo hawa watu wa fire wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naingia kwenye mitandao ya simu. Kuna mambo mengi yanazungumzwa kwenye mitandao, kuna kashfa nyingi zinapitishwa kwenye mitandao, kuna taarifa nyingi ambazo si za ukweli ziko kwenye mitandao kuhusu gharama na ada mpya ambayo Serikali na kodi inaitaka kwenye simu nchini mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina watu zaidi ya milioni 55. Walipaji kodi kwenye nchi hii hawafiki milioni tano, hawa milioni tano kwa kweli, kodi wanayolipa wao inaweza ikabeba maendeleo ya nchi hii kwa watu milioni 50? Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tujitoe muhanga, lazima tukubaliane na mabadiliko ya nchi yanavyokwenda. Yesu Kristu kipindi chake na kwenye kitabu alichokujanacho alisema ya Kaisari yaende kwa Kaisari na ya Mungu yaende kwa Mungu. Mtume Muhamad (SAW) na kwa waislamu alianzisha vita na mataifa ya kiarabu kwa kutokutaka kutoa zakaa. Unachukua kwa mwenye nacho unampa asiyekuwanacho. Leo wananchi wanalilia barabara, wanataka maji, wanataka elimu, wanataka bima za afya, pesa zinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe wananchi huu utaratibu wa kwenye mitandao wa kutoa maneno ya kashfa, kutukana viongozi, kitu ambacho mnashindwa kuelewa kila uki-post tangazo lako la matusi au tangazo la kashfa ujue unalipa kodi. Kila ukitukana, kila uki-post, elewa unalipa kodi hiyo ndio nia yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi juzi Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameweka vizuri sana kwenye miamala hii kodi hii ya simu ameweka kuanzia 10 mpaka 200. Hebu tuchukue kwa wale ambao watalipa 20 kwa siku, 20 tu ambayo ni 600 kwa mwezi kwa watu milioni 30 ni bilioni 216. Tumejaribu kupanua wigo wa kodi hata yule mwananchi wa kawaida naye awe na mchango wa barabara, awe na mchango wa bima, awe na mchango wa masuala ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaposema vijana wengi wako katika mitandao vijana hawa wazazi wao wanataka kwenda hospitali. Vijana hawa Ndugu zao wanataka kwenda kujifungua. Vijana hawa wanataka bima kwa wote. Vijana hawa wana wazazi wao wagonjwa. Vijana msipotoshwe na taarifa ambazo zinatolewa ambazo hazina ukweli. Sasa mtu kama mimi niliyekubuhu hata nikipigwa madongo sijali, wala siogopi, sababu najua wananchi wanataka maendeleo. Maendeleo yatakuja na kodi. Isipokuwa Waziri wa Fedha, nikuombe, ada hizi za simu, kodi hii maalum ambayo Wabunge wote tumekubaliana, lazima ui-ring fence; inakwenda kwenye maji, inakwenda kwenye barabara, inakwenda kwenye bima kwa wote, isiwe pesa hii inatumika kwenye posho, isiwe pesa hii inatumika kwenye semina, isiwe pesa hii inatumika kwenye mambo ambayo hayana tija kwa … (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mheshimiwa Rais, Mama Samia Mama yetu, amempa kila Mbunge milioni 500 kwa jimbo. Kila shule, kila kata isiyokuwa na sekondari, nampongeza Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa TAMISEMI, leo ametutangazia kila kata isiyokuwa na sekondari milioni 600 wanapewa. Hizi hela zitatoka wapi kama sio kodi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na tuna uwezo wa kulipa hizi kodi kwa kiwango cha kila mtu. Yule mwenye uwezo mkubwa atalipa kodi kubwa, the rich will pay more, the rich will be taxed more and taxes are collected they are not paid; kodi inachukuliwa hailipwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, watu tujiandae na mabadiliko ya kufunga mikanda kusaidia Taifa letu liende mbele. Tuna miradi ya SGR inataka hela, tuna miradi ya bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere linataka hela, tuna miradi mipya ambayo Serikali inataka hela kwa hiyo, lazima tulipe kodi tupate hela. Kuna barabara za vijijini, tunataka mazao ya wakulima yafike kwenye masoko kwa uhakika, kuna maeneo ambayo barabara hazipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wananchi wa Ilala ndio walionituma, nawazungumzia wao, najua hawa wote wanaopondaponda kwenye mitandao hawakai Ilala, wao wanakaa Kivule, Bombambili, sijui Majimatitu, sisi watu wa Ilala tunataka maendeleo. Tunataka barabara, tunataka miundombinu ya mifereji, tunataka lami kwenye majimbo yetu ya mjini tuweze kuchangia pesa za kutosha tusaidie majimbo ambayo hayana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Ilala tunakusanya 1,100,000,000 kwenye ada ya ku-park magari. Parking za magari kwenye Wilaya ya Ilala one billion kwa mwezi Mheshimiwa Waziri na hizi pesa wala haziji kwetu zinakwenda kusaidia maeneo mengine. Sasa tuboreshe maeneo yetu ya mjini, ili tuweze kusaidia… (Makofi)

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zungu kuna Taarifa.

T A A R I F A

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kumpa Taarifa Mheshimiwa Zungu kwamba, kodi hii ya simu imejibu kilio cha muda mrefu cha Watanzania cha kutaka kila Mtanzania alipe kodi kwa usawa. Kwa hiyo, kodi hii ya simu Wabunge tunalipa, viongozi wakubwa wanalipa, mpaka mtu wa chini analipa kwa usawa. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Nadhani uli…

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea Taarifa. Na kulingana na matumizi yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hakuna mtu anaandikiwa barua, leo hakuna mtu ananunua stamp, leo hakuna mtu anakwenda posta. Leo sio lazima ukamtembelee Ndugu yako kulipa nauli ya 2,000 ya nauli ya basi, unapiga simu unazungumza naye, watu hawayaoni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo uko Mwanza unauliza bei ya soko ya ng’ombe Pugu, huna haja ya kumtuma mtu aje Pugu unauliza kwenye simu kwa hiyo, simu hizi ni chocheo kubwa la maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Serikali kuanzisha kodi hii, isipokuwa matumizi ya pesa hizi yalindwe yasiende kutumika kwenye maeneo ambayo hayastahiki kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Serikali ina mpango wa bima kwa wote. Wananchi wetu wanalalamika dawa hakuna, wananchi wanalalamika wanakwenda kujifungua maisha magumu, wananchi wanalalamika huduma za hospitali zinapungua. Kwa ada hii na pesa hizi ambazo tutazipata ndio kimbilio la wananchi wetu kupata maisha bora. Ndio kimbilio la uzazi salama kwa mama zetu. Ndio kimbilio la lishe salama kwa mama zetu. Tukubaliane, tusaidiane, tuunge mkono jitihada za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanaokataa kodi hii wanataka kuirudisha nyuma Serikali hii, hilo hatutakubali. Hatutakubali kurudi nyuma tunakwenda mbele, mbele kwa mbele. Tumetoka katika matatizo makubwa sana ya kutokuwa na mapato, sasa tunaanza vyanzo vipya, lipa kodi yako ya simu, tumia simu yako unavyopenda ukitumia kidogo utalipa kidogo ukitumia sana utalipa sana wala halina mjadala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitandao sasa hivi kuna tools za kujua every user kwa kila mtu wa mtandao wa simu. Kwa hiyo, wale ambao mapato yao ni madogo watalipa kidogo, lakini wanachangia Taifa lao kwenye maendeleo ya barabara. Atatoka Kivule, Bombambili, atakuja mjini mapema, atakaa Tabata atakuja mjini mapema sababu barabara ni safi za lami kwa hiyo, tuungane na Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema tena na wale wanaoendelea …

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, mnanipotezea muda sasa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zungu kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tarimba.

T A A R I F A

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimpe Taarifa Mheshimiwa Zungu kwamba, kodi hii kwa Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza, hata Marekani wanatoza kodi kama hii, hivyo, Watanzania wasipate wasiwasi kwamba, sisi tumejitengenezea kodi ambayo ya kumuumiza, bali inachukua at least 19% ya consumer bills katika nchi ya Marekani hivyo Watanzania… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ongea Kiswahili, hatujaelewa hapo ulipoongea kingereza, ongea Kiswahili.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, sijui tafsiri ya consumer bills. Natoka Kinondoni na sijui.

NAIBU SPIKA: Sasa kama wewe hujui na ndio mnasema Kiswahili kifundishwe Watanzania…

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, consumer bills ni gharama za matumizi ambayo ni karibu asilimia 19 ya wamarekani wanalipa kodi hii. Hivyo, Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kuweza kulipa kodi kama hii, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Sasa hebu ngoja Taarifa yako tuielewe vizuri, samahani Mheshimiwa Zungu. Kule wanalipa asilimia 19 hapa tutalipa asilimia ngapi?

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, hapana, hizo asilimia 19 ni gharama nzima za matumizi ya wananchi wa Marekani katika utilities. Inaonekana ni asilimia 19 imo katika kodi kama hii.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zungu, malizia mchango wako.

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nakubali Taarifa yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo sasahivi Mkoa wa Dar es Salaam wanataka kuzitengeneza ni zaidi ya bilioni 700. Na hizi pesa zinataka zilipwe, hizi pesa zinakopwa, hizi pesa zinakuja kwa niaba ya Serikali yetu ambayo inasifika kwa kulipa madeni yake na lazima tuchangie tulipe deni hili ili barabara zetu ziweze kuboreka, ili miundombinu ifurahishe na watu waweze kutembea na waweze kupata huduma bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Narudia kusema wanaoendelea kutukana kwenye mitandao mnalipa kodi mjue hivyo. Ahsante sana. (Makofi)