Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. Pia namshukuru sana Mwenyezi Mungu kupata nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu sana katika uongozi huu wa Awamu ya Sita na pia katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ikiwa ni bajeti ya kwanza ya miaka mitano 2021/2022 na 2025/ 2026. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kumpongeza mama yetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Tunamwangalia kiongozi siyo katika maono tu na katika level ya usikivu, huyu mama ni msikivu pamoja na Serikali yake yote wamekuja na bajeti ambayo imejibu matamanio mengi makubwa ya Watanzania, pia imejibu hoja mbalimbali ambazo kwa umoja wetu Wabunge tumekuwa tukichangia na tukiishauri Serikali katika Wizara zote ambazo tumechangia, imejibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuipongeza pia Wizara yote, Waziri wetu, Naibu Waziri, Kamati pamoja na Watendaji wa Wizara hii kwa umakini mkubwa kutetea bajeti hii njema. Napongeza vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimetufanya kuendelea kuwa na amani mpaka tumefanya mambo yote haya kwa utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali yetu kuendelea kutambua na kuthamini mchango muhimu sana wa watumishi katika kuchangia pato la Taifa. Tumeona jinsi ambavyo Serikali imejibu kwa ujumla wake, kwa mwavuli wake kuhusu maslahi ya wafanyakazi. Sitachambua moja moja, yapo dhahiri kwenye bajeti na wenzangu wameyachangia, lakini kuna suala zima la utengaji wa karibu shilingi bilioni 449 kwa ajili ya upandashaji wa madaraja. Ni jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali, katika upandishaji wa madaraja haya; natoa mfano, unakuta kuna kada moja ya taaluma na level sawa ya elimu, lakini unakuta mmoja ameajiriwa mwaka 2014 mwingine 2020 lakini wamekuja kupandishwa daraja pamoja 2020, wanakuwa level moja ya daraja. Hii inavunja morali kwa kwa yule aliyetangulia. Kwa hiyo, naomba nishauri, mnapopandisha madaraja kwa hizi bilioni zilizotengwa, karibia watumishi 92,000 wameshahakikiwa, lakini suala la seniority tulizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo Halmashauri zisizopungua 184 na tafiti zinaonesha karibia asilimia 80, Halmashauri zetu tunategemea ruzuku ya Serikali Kuu. Hata hivyo, naomba niipongeze Wizara ya Fedha na Mipango, mwaka 2018 mlikuja na miongozo ya uandaaji wa miradi ya kimkakati katika Halmashauri zetu ili kujijenga kimapato na baada ya kujijenga kimapato Halmashauri zetu ziweze kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wetu kule kwenye grassroot. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa napongeza kwamba katika miradi ya kimkakati yote iliyowekwa, miradi sita imekamilika, miradi 32 bado ipo kwenye hatua ya ukamilishaji. Hata hivyo, tafiti zinaonesha miradi hii ya kimkakati ina changamoto nyingi sana. Mojawapo ni changamoto za kiutendaji ambayo ni pamoja na ukosefu wa wataalam wa kuandika yale maandiko. Ukosefu wa hatimiliki za ardhi na changamoto za kimuundo nyingine na kitaaluma na taasisi, ni ukosefu wa watalaam husika wa kusimamia miradi ile kwa maana ya ma-engineer na wazabuni na vitu vya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwamba imeendelea kuajiri walimu na watumishi wa afya, tunashukuru sana. Naomba nishauri, kada nyingine nazo mziajiri kwa sababu nia njema ya dhima ya bajeti hii ya kujenga uchumi na viwanda kwa maendeleo ya watu, ni kule kwenye watu chini kwenye Halmashauri. Nia yenu njema ya kuja na mikakati hiyo ya kuboresha na kujenga kimapato Halmashauri zetu, changamoto hizi tuziangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri wadau wanaohusika na utekelezaji wa miradi hii ya kimkakati mkiwemo ninyi Wizara ya Fedha na Mipango, ikiwepo TAMISEMI, Sekretariati za Mikoa na Halmashauri, mkae kwa Pamoja. Kuna vigezo vimewekwa ambavyo siyo rafiki na siyo halisia na uwezo wa baadhi ya Halmashauri. Nia ni njema, lakini nashauri mkae mziangalie tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Serikali imekuja na mpango mzuri sana wa afya kwa wote, nia na makusudi ni kwamba kaya zisizopungua 12,000 zipate bima ya afya, lakini pia katika hizo kaya 12,000 asilimia 20 ndiyo kaya za watu ambao hawana uwezo kabisa na Serikali inasema kila mwaka itakuwa inatakiwa ipate zaidi ya shilingi bilioni 140 na kila mwaka ili angalau katika miaka hii ambayo lengo lake ni katika 2034/2035 kila Mtanzania awe amefikiwa na Mfuko wa Bima ya Afya, yaani kila mwaka iwe inapata zaidi ya shilingi bilioni 149. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna changamoto ya mfuko huu, lazima uwe unapata michango kutoka sekta binafsi, sekta zisizo rasmi na sekta rasmi, najua changamoto ipo kwenye sekta ambazo siyo rasmi. Kwa hiyo, naishauri Serikali itafute mbinu nzuri sana za kuhakikisha kwamba sekta zisizo rasmi zinashiriki kikamilifu katika kuchangia mfuko huu ambao una nia njema sana ya kwamba kila Mtanzania apate bima ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)