Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii niliyopewa ya kuchangia. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa nafasi hii kwa kusoma mstari wa Zaburi ya 136:1 katika Biblia, unasema; “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana Fadhili zake ni za milele.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninapenda sana kuipongeza Serikali kwa ujumla, hasa Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Mawaziri wote, pamoja na Waziri wa Fedha kwa bajeti nzuri sana ambayo imewekwa mezani petu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii inatoa matumaini makubwa kwa Watanzania pamoja na Wanakilolo ambao kwa kuiangalia tu tayari tumeshaanza kupata matunda ya Awamu ya Sita kwa zile milioni 500, tumeshazipokea kwa ajili ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunajua tunakaribia kupokea shilingi milioni 600 kwa ajili ya shule za sekondari. Yote hayo tunajua ni juhudi ambazo zinafanyika katika kulikwamua Taifa letu, likiwemo Jimbo la Kilolo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Rais, nami nikaitafakari wakati alipokuwa akiongea na vijana. Tafakari yangu hasa ililenga kwenye kuwawezesha vijana kimitaji. Mheshimiwa Rais amekuja na wazo zuri sana la kuanzisha benki ya vijana. Hapa niliona ni vema nikatoa ushauri wangu. Ushauri huu unatokana na haya yafuatayo:- (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo benki mbalimbali zilizoanzishwa kwa malengo maalum. National Microfinance Bank (NMB), hata kwa maneno yake, ni benki ya mikopo midogo midogo (microfinance). Tunayo Mwalimu Commercial Bank iliyoanzishwa kwa ajili ya walimu. Vile vile tulikuwa na Tanzania Women Bank. Kinachozitesa hizi benki ni riba. Kama riba ingekuwa ndogo, hatuhitaji kuanzisha benki nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu, tuna benki zenye mtandao nchi nzima. Hizi benki nilizozitaja zote zilikuwa Dar es Salaam, kama zimeenda mbali sana, zitakuwa Arusha au mahali pengine katikati ya miji. Tunazo benki zilizosambaa mahali pote. Pendekezo langu na ambalo nafikiri ningeweza kushauri ni kuanzisha madirisha maalum kwenye benki ambazo hata Kilolo zipo, lakini riba isiwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba kama kuna fedha kwa ajili ya kuanzisha hii benki, hatutawekeza kwenye kodi ya majengo, hatutawekeza kwenye miundombinu, hata wafanyakazi hatutawekeza, tayari wapo. Tuangalie benki ambazo tayari zina mitandao ili vijana hata kesho kama hiyo hela ipo ikiwekwa, wafundishwe hao wafanyakazi kwenye hizo benki ambazo zipo tayari ili vijana waweze kupata mikopo na waweze kufanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti katika benki pia yakipunguzwa, hawa vijana hata hii benki ikianzishwa kama wataambiwa wapeleke collateral ya nyumba, hawana. Kama wataambiwa wapeleke collateral ya viwanja, hawana. Kwa hiyo, kinachowatesa siyo benki, ni riba na masharti ya hizo benki. Kama likianzishwa dirisha maalum na hilo dirisha likaondoa hayo masharti, basi kazi itakuwa rahisi sana kuwawezesha vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuongelea suala zima la Madiwani. Tunashukuru Madiwani sasa watalipwa kwa kupitia Serikali Kuu, lakini sisi wote tunafahamu, nami nafahamu hata Mheshimiwa Waziri, nawe ni Mbunge, kuna Madiwani kule Jimboni kwako. Hawa Madiwani wote wanafanya kazi kubwa sana katika kuwahudumia wananchi. Hii posho inayolipwa, bado ni ndogo sana. Napendekeza kwamba kuwe na nyongeza pia ya posho yao licha ya kulipwa kutoka Serikali Kuu. Ikiongezwa tutawasaidia sana ili waweze kufanya kazi vizuri na kutimiza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee hapo hapo, hizi Halmashauri zilikuwa zinalipa hii posho, tumewapa hiyo nafuu. Hii hela ambayo tumeiokoa ningependekeza yatolewe maelekezo maalum ielekezwe kwenye nini? Nafahamu kwenye Jimbo langu kwa mfano itaokolewa karibu shilingi milioni 10 kwa mwezi au zaidi. Hii fedha inatosha darasa moja la Shule ya Msingi, inatosha kupaua majengo yale ambayo ni maboma. Tusipotoa maelekezo maalum au wasipokuja na mpango maalum wa kuzitumia zile fedha ambazo tumeziokoa kwa Serikali Kuu kulipa, matumizi haya hayataeleweka na huku kuokoa hakutakuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza TAMISEMI itoe maelekezo maalum kwa fedha zilizookolewa kutokana na Serikari Kuu kulipa posho za Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kuzungumzia misamaha ya kodi kwa taasisi za dini. Ninakushukuru kwanza Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali mmekuja na msamaha mzuri. Napenda nikwambie kwamba kuna kigezo kilichowekwa cha kusema kuwe na mkataba kati ya Serikali na mtoaji msaada ndipo msahama utolewe. Kuna taasisi ndogo nyingi za dini ambazo zinatoa misaada na nitakupa mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye Jimbo langu Kilolo kuna container lenye dawa, lenye vitanda kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Kilolo, lina miaka mitatu pale bandarini na lilitolewa na Kanisa na suala ilikuwa ni msahama ambao ulichukua zaidi ya miaka miwili kupatikana. Sasa hivi tunashughulikia storage na mpaka sasa sijui itatolewa lini? Ni kwa sababu ile ni taasisi ndogo, lakini imetoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaweza pengine kufanikiwa kuingia mikataba na taasisi zote, lakini zile taasisi ambazo zimesajiliwa na tunajua zinatoa msaada, tukisema kwamba lazima tuingie mikataba, tutachelewa. Hapa sisi wote kwenye maeneo yetu tuna taasisi za dini ambazo zinasaidia na mara nyingi zinakwama kwenye misamaha na wakati huo huo zinachelewesha na kama nilivyozungumza hapa, lile ni kontena la dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuna nchi hapa kuna kontena lilipuka na moto ukaunguza nusu ya mji, lakini tumeacha kontena lenye dawa ambazo najua zime-expire lipo bandarini na halijapatiwa msamaha hadi leo. Sasa ni storage, wakati huo huo tunajua lina viashiria vya hatari kwa sababu hatujui zile dawa ziki-expire zitafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa huo mfano ili kuona umuhimu wa kuharakisha misamaha hasa tunapopokea misaada ambayo tunaihitaji. Kwa sababu sasa pale Kilolo vitanda na dawa tunanunua, Serikali inatoa hela. Kama tungepokea vile, tungekuwa tumeokoa hela nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango mzuri sana.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nashukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)