Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti yetu ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niwashukuru wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini kwa kuendelea kuniamini ili mimi niweze kuwatumikia lakini pia ninaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa inayofanya, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia Serikali kwa sababu imetuwezesha sisi Wabunge kwenye majimbo yetu kwa kutupatia zaidi ya shilingi 500,000,000 kwa ajili ya kushughulika na barabara ambazo zimekuwa kero kubwa sana kwa Watanzania.

Pia naipongeza Serikali kwa sababu ilisikiliza kilio cha Wabunge na mawazo yao kwa muda mrefu ambayo tumekuwa tukiyazungumza hapa. Kwa mfano mimi Jimbo langu la Bunda Mjini, takribani muda mrefu uliopita nyuma barabara zangu za mitaa zilikuwa haziwezi kupitika kwa namna yoyote ile hata kama ungeenda na trekta zilikuwa haziwezi kupitika. Lakini kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita ni Serikali sikivu imetoa fedha na sasa barabara zimeanza kupitika hata kama sio zote lakini mwanzo umeshaanza kuonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita imetufanyia mambo makubwa pale Bunda Mjini. Kwa muda mfupi huu tumeshapata taa za barabarani pale mjini, tumeshapata fedha za kujenga shule za sekondari zaidi ya sita, na kwa muda mfupi tumeshazifungua lakini pia na shule za msingi ziko zinaendelea kujengwa. Kwa hiyo kwa bajeti hii ambayo imewasilishwa na Wizara ya Fedha Mheshimiwa Mwigulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo muhimu sana ambalo mimi ninaliona hapa ni kuhakikisha kwamba Wizara ya Fedha inasimama vizuri katika kuhakikisha kwamba makusanyo yale yanayopatikana yanatumika vizuri kwa ajili ya shughuli za maendeleo za wananchi. Wananchi wa nchi yetu tuzipowazoesha suala la kulipa kodi wakalijua, kwamba kila mfanyabiashara anayefanya biashara kulipa kodi ni wajibu wake kuna siku watakuja kudai maendeleo pasipo wao kutaka kutoa kodi. Kwa hiyo hili nilipenda niishauri Wizara ya Fedha ikasimame nalo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, kwa sababu ya makusanyo yetu tunayoyakusanya hayatoshelezi mahitaji yetu, bajeti yetu kwa mwaka ni trilioni 36 lakini makusanyo yetu yako chini. Kwa maana hiyo, fedha hii tunayoikusanya kidogo ni vizuri Wizara ya Fedha ikazilinda vizuri fedha hizi ziweze kutumika kwa shughuli mahsusi. Wasipofanya hivyo, fedha tunayopata ni kidogo na matumizi yakaenda nje na utaratibu unaotakiwa, kile tunachokilenga kwenye shughuli za maendeleo hatutakifikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wabunge tumesema hapa tukaiomba Wizara ya Fedha kutusaidia fedha kwenye TARURA na wametupa fedha. Lakini kama watu hawatalipa kodi fedha hizo pia tunaweza tukazungumza hapa kuanzia asubuhi mpaka jioni na fedha zisipatikane. Kwa hiyo muhimu ni kuwajenga wananchi wetu kwenye maeneo yetu ili wafahamu kwamba kulipa kodi ni sehemu ya maisha yao ni sehemu ya biashara zao. Wakilipa kodi wanarudi kuidai Serikali maendeleo. Kama hawatalipa kodi kuidai Serikali maendeleo haitawezekana. Lakini pia hatuwezi kupata maendeleo kwenye nchi yetu tukifikiri tu kwamba tunaweza tukapewa fedha za misaada halafu zikatuletea maendeleo kwenye nchi yetu. Hiki kitu hakitawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuishauri Wizara ya Fedha; Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA inafanya kazi nzuri lakini suala kubwa ambalo mimi ningewaomba wajitahidi kutoa elimu kwa wafanyabiashara. Waweke mazingira ya kodi wazi, kila yule anayetaka kulipa kodi ajue uwezo wake wa kulipa kodi na kodi anayotakiwa kuilipa ni ipi. Wakishafanya hivyo, watu walio wengi wataenda kulipa kodi wao wenyewe kwa hiari yao. Lakini na wao wananchi wakishalipa kodi kwenye Serikali wanaidai Serikali maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hilo ni muhimu sana ambalo Wizara ya Fedha inapaswa kulishika vizuri ilisimamie vizuri na kwa sababu fedha yetu haitoshi shughuli zetu za maendeleo kwa mwaka, kidogo tunachokipata tuweze kukitumia vizuri. Mimi nimeshangaa kuja kuona kwamba wapo watu baadhi wanaweza kwenda kwenye bomba la mafuta la Serikali wakaenda wakachimbua kwenye bomba la mafuta ya Serikali halafu wao wakapeleka yale mafuta kwenye maeneo yao wakaenda kuuza, raia wa nchi hii. Kama tunataka maendeleo kwenye nchi hii ni lazima sisi wenyewe Watanzania tuwe wazalendo kwa mali zetu sisi wenyewe. Wale watu wanaofanya hayo kwa kuhujumu miundombinu ya Serikali, wanatuambia sisi Wabunge tunachokizungumza hapa au kile ambacho Serikali inakipanga hakitafanikiwa kwa sababu wao wanakihujumu. Kwa hiyo, lazima Serikali isimame kidete kwenye jambo hili ili kwamba wale watu wanaofanya mchezo ule wauache mara moja kwa sababu sio jambo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mtazamo wa nchi kwa sasa wana mpango mkubwa wa kufanya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania ambalo wao leo wakiona watu wa Dar-es-Salaam au watu walioko bandarini wanafanya vitu vya namna hiyo, kuna watu watajifunza vitu viovu kupitia kwao, halafu matokeo yake kile tunachokikusudia tusikifikie kwa makusudi ya watu wachache, kundi la watu wachache wasiozidi 10 au 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mtazamo wa nchi kwa sasa wana mpango mkubwa wa kufanya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania ambalo wao leo wakiona watu wa Dar-es-Salaam au watu walioko bandarini wanafanya vitu vya namna hiyo, kuna watu watajifunza vitu viovu kupitia kwao, halafu matokeo yake kile tunachokikusudia tusikifikie kwa makusudi ya watu wachache, kundi la watu wachache wasiozidi 10 au 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara ya Fedha, leo tunazungumza na Mheshimiwa Waziri hapa, tunaipongeza sana bajeti yake ni nzuri na imekidhi vigezo vizuri vya wananchi wetu, lakini itakuwa nzuri pale yale yote tunayoyatarajia yafanyike kwa wananchi yatakapofanyika. Nje na hapo tutakaporudi mwaka kesho au kwa muhula mwingine tutaanza kumsema Waziri vibaya, lakini fedha ikipatikana bajeti itakuwa nzuri na shughuli za maendeleo za wananchi zitakwenda vizuri na kile tunachokusudia kitafikiwa. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri kudhibiti suala hilo kupitia Serikali ili kwamba, yale mapato yetu madogo tunayoyakusanya yaweze kutusaidia kwenye shughuli zetu za maendeleo. Nje na hapo Mheshimiwa Waziri, leo tutampongeza na kesho tutarudi kuja kulaumu kwake tena kwamba, mbona hakufanya yale ambayo tulikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda nichangie hayo mambo machache katika bajeti hii ili niweze kusema hilo nililoliona. Nakushukuru sana. (Makofi)