Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti hii muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye mara zote amekuwa akitupa afya njema na uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia kidogo sana. Lakini kwanza kabisa nishukuru Wizara na kumshukuru Waziri kwa namna ambavyo mapendekezo yetu sisi Wabunge yamezingatiwa. Kwa hakika kila Mbunge huku nyuma amesema mambo mengi na mengi yameonekana kwenye bajeti hii. Kwa hiyo namshukuru sana lakini pia nampongeza sana yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mkuu, mpango mkuu kwenye bajeti hii unaeleza juu ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu. Hili ni jambo kubwa sana na mimi nataka nichangie ni namna gani sasa tunaweza tukafika huko ambako ndiko ambapo mkakati mkuu wa bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote wengi wetu tuna Majimbo huko na tunafahamu ili tuweze kufikia mkakati huu lazima tuwe na miundombinu bora na imara. Katika hilo kwanza nimshukuru sana sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha, kwa kuiwezesha TARURA kwa kutoa milioni 500,000,000 kila jimbo. Kwa hakika ametusaidia sana sana kuhakikisha baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki tunaweza tukapambana nayo ili walau yaweze kupitika kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo yapo mambo ambayo nataka nipendekeze. Nafahamu kila Jimbo linahitaji fedha lakini nafahamu kuna maeneo ambayo kiukweli hayapitiki. Moja ya maeneo hay ani majimbo yetu sisi ya vijijini. Sisemi kwamba watu wa Ilala wasipewe, watu wa Kinondoni wasipewe. Hapana. Nafikiria kwamba tumepewa milioni…

MWENYEKITI: Toa mchango wako huna haja ya kutaja Majimbo mengine.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetaja Ilala kwa sababu wewe ndiyo Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Toa mchango wako ndugu au utakaa sasa hivi hapa. (Kicheko)

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni moja, nafikiria kwamba ili tuweze kufikia malengo ya bajeti hii tunafikiria ni lazima tufungue maeneo yote ili yaweze kupitika kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Kanda ya Kati, kwa mfano jimbo langu ni wazalishaji wakuu wa alizeti, na sasa hivi tunaenda kufungua viwanda vya alizeti, kama tulivyosema, kwamba mkakati namba moja ni kuhakikisha tunaweka uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu. Katika mazingira hayo yapo maeneo ambayo wamelima alizeti lakini hawana uwezo wa kuzitoa kule kuingiza sokoni. Au, kwa kufanya hivyo, unayatoa kwa gharama kubwa kweli kweli. Maana yake sasa mkulima anazalisha, anatumia fedha nyingi lakini tija yake inakuwa ni ndogo kwa sababu hana uwezo wa kuyatoa au akiyatoa, anayatoa kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo mimi naomba pale TARURA tumeongezewa fedha. Ninakushukuru sana Waziri wa Fedha namna ambavyo umefikiria na umezingatia namna ambavyo tuliongea huku nyuma. Sasa fedha zile zikipatikana naomba basi mgao ule ulenge mahitaji. Tuangalie ni wapi sasa ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie mimi nimeshindwa. Tulielekezwa zile fedha tulizopewa walau tujenga barabara au tujenge kwa kiwango cha changarawe. Lakini ni ukweli kwamba kuna maeneo ambayo hata watoto hawawezi kwenda shule wakati wa mvua. Watakushangaa sana utato amilioni 500,000,000 zile ukajenge kilometa moja ya lami wakati kuna maeneo ambayo hawapo. Mvua zikianza lazima mvua ziishe ndiyo watoto waende shule. Katika kuzingatia hilo, mimi nimuombe sana Waziri wa Fedha, rafiki yangu wa muda mrefu, rafiki yangu wa muda wote. Naomba mnapotoa hizi fedha basi hebu jaribuni kuangalia ni namna gani tunaweza tukaifungua hii nchi kila eneo walau lifaidi au kila eneo walau liweze kupitika kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mimi nakufahamu ndugu yangu Mwigulu Nchemba, ni mtu mchapakazi, mwerevu, anaweza. Sasa tumeongeza fedha kwa ajili ya TARURA naomba basi zitoke, maana tunaweza tukaziongeza lakini kuziongeza na kuzikusanya ni jambo lingine lakini kuzitoa ziende TARURA pia ni jambo lingine. Nafahamu hilo lipo ndani ya uwezo wako Mheshimiwa Waziri. Sisi ambao tuna Majimbo ambayo yapo vijijini tuna changamoto kubwa sana. Naomba sana, fedha hizo zikikusanywa zipekwe huko ili walau zitusaidie kufungua vijiji na vitongoji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwangu peke yangu kwenye zile kilometa nyingi zinazotajwa nina kilometa zaidi ya 1,000 na zaidi za TARURA, lakini ambazo zinafanyiwa ukarabati au zinaweza kupitika ni asilimia 17 tu. Tafsiri yake ni kwamba maeneo mengi hayapitiki wala hayana uwezo, hata kama una biashara yako huwezi kufanya. Mimi nilitaka kuchangia hilo kuhusu barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba niongee kidodogo kuhusu kilimo. Waziri mwenyewe anakiri kwamba asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo, lakini ni ukweli kwamba hakuna namna ambavyo nchi yetu inaweza kwenda mbele bila kuwekeza kwenye kilimo ambacho ndicho kina watu wengi na hakuna formula zaidi ya hiyo. Ukweli ni kwamba ukitaka ku-solve quadratic equation lazima utumie quadratic formula, hakuna namna nyingine.

Nimejaribu kuangalia na kufanya tafiti kote duniani, ukweli ni kwamba lazima uwekeze kwenye nguvu kubwa, lazima uwekeze kwenye shughuli kubwa ya kijamii inayofanyika. Watanzania wengi ni wakulima lakini sisi tunawekeza kidogo mno. Bajeti yetu walau tungeisogeza ikafika asilimia 10 ya bajeti tungekuwa tunaamini kwamba sasa tunaenda kusaidia watu walio wengi ili waweze kuinuka kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hilo mimi Jimbo langu asilimia 95 ni wakulima, na ukitaka kumuuliza mtu anawezaje kupata fedha lazima asubiri wakati wa mavuno ndiyo anaweza kupata fedha na akatunza kwa ajili ya kuhudumia mwaka mzima. Sasa, katika mazingira hayo kuna changamoto kubwa sana kwenye. Moja ya changamoto kubwa sana ni masoko. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri kaeleza vizuri kwenye bajeti hii. Ameeleza namna gani ambavyo anaweza ku-deal na hilo suala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine kubwa, na mimi nafahamu ndugu zangu wenye majimbo hapa idadi kubwa sasa hivi ya watu vijijini ni vijana. Vijana ni wengi sana huko vijijini. Mimi nikienda vijijini nikiitisha mkutano nakutana na vijana wengi sana. Wapo vijana wenye degree mbili (Masters) wapo vijana wana degree moja, wapo vijana ambao hawana elimu, wako vijijini wamezubaa kule hawana cha kufanya. Tufanye nini sasa, kwa sababu tukifikiria kwamba waende kujiajiri, wanajiajiri vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri kama alivyosema kwenye bajeti yake ninamuomba sana Waziri hili jambo alifuatilie, tuangalie namna gani tunaweza kuwekeza mitaji kwenye hawa vijana. Otherwise tunaweza kutengenza mazingira magumu sana kwao na kwetu sisi ambao mara zote wenyewe ndiyo wanatusaidia kutupigia kura. Nilitamani sana niyaseme hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nilitaka kuongea kidogo kuhusu elimu. Niliwahi kusema huku nyuma, kuna changamoto kubwa sana kwenye Halmashauri hizi ambazo ni changa, Halmashauri ndogo kama ya kwangu mimi ambayo ukikusanya fedha mapato yote kwa mwaka ni bilioni 1.2 na ukiangalia uwezo wa ujenzi wa madarasa ni mdogo sana. Bado narudi kwenye hoja ile ile kwamba ni lazima tuangalie ni wapi. Wakati mwingine unajiuliza maswali makubwa sana kwamba kule Wizara ya Elimu wametoa fedha kwa ajili ya maboma lakini wametoa flat rate. Yaani mtu ambaye anakusanya bilioni 100 unampa flat rate na mtu anayekusanya bilioni 1.2 kwa mwaka. Hii haiwezi kuwa sawa na hatuwezi kuwa tunalenga sasa kuendeleza hizi halmashauri changa au watu walioko. Mimi nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, hili ulizingatie vizuri. Mimi naamini wewe unaweza na haya mambo unaweza ukayaweka vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)