Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa pumzi alizoweza kunipa siku ya leo lakini nami niweze kuchangia katika bajeti hii. Kwa leo, nishukuru kwa kidogo, wanasema usiposhukuru kwa kidogo hata kwa kikubwa huwezi kushukuru. Niweze kushukuru kwa mawazo haya yaliyochukuliwa kwa sababu nimekuwa ni mdau wa barabara nimekuwa nikichangia kwenye barabara katika TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi nimejikita sana kwenye barabara. Kwa hiyo, nimeona hapa mrejesho uliokuja umekwenda kuleta suluhu kama tutakwenda ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleza jinsi Serikali inavyopoteza wawekezaji, nikaeleza jinsi inavyoweza kufikia kukosa pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja kama hatutatengeneza miundombinu thabiti ya barabara. Lakini nikaeleza ni jinsi gani tutashindwa kwenda kufikia kauli mbiu ya Tanzania ya Viwanda kama hatutatengeneza miundombinu; nikaeleza ni jinsi gani hatutafanya kilimo chenye tija kama hatutatengeneza miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoongea hivi narejea kwenye hotuba ya bajeti kwenye ile para ya 39. Nimeona pale kwamba Serikali inakwenda kuomba mikopo ya bei nafuu kwenye Benki ya Dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeainisha pale kiasi cha dola za Kimarekani milioni 120 imeelekezwa itakwenda Dar es Salaam. Ikaelekezwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 300 zitakwenda mikoani kwa lengo la kukuza uchumi. Lakini pale ikaelekezwa milioni 50 dola za Marekani Serikali itakwenda kuweka pale; lakini mwisho wa siku tunapata jumla ya dola za Kimarekani milioni 470. Tukienda kubadilisha kwa fedha zetu za Kitanzania kwa rate ya leo ni shilingi 2,300 tunapata trilioni 1.081. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukihama twende ile para ya 88 ambapo kuna tozo ya mafuta. Serikali inaendelea kutafuta fedha mbadala ili tuweze kupata suluhu ya kero ya barabara. Kwenye tozo ya mafuta ya petrol na diesel tumesema pale kila lita moja itatozwa shilingi 100. Serikali ikadadavua ikapata 322,158,000.20, ukijumlisha unapata trilioni 1.403 fedha hizi ni nyingi sana na zote zinatakiwa zielekee TARURA ndio lengo la Serikali. Na ukiangalia asilimia ya barabara zetu za vumbi ni asilimia 72.4 Nchi nzima kwenye mtandao wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi ni nyingi naomba nishauri jambo. Kwa sababu fedha hizi ni nyingi na zikiwekezwa kweli kwenye TARURA zitaleta tija, ninaomba fedha hizi ziwekwe kwenye ring-fence ili zisitumike kwenye matumizi mengine lakini jinsi zilivyotengwa ziende eneo husika. Namba mbili, fedha hizi jinsi Mheshimiwa Waziri alikuja hapa akadadavua vizuri aje hapa wakati wa kuhitimisha fedha hizi zianishe barabara zinazokwenda kujengwa. Lakini pia zianishwe zinakwenda kujengwa kwa kiwango kipi cha lami, cha changarawe au kiwango kipi ili tuangalie thamani ya fedha zetu zinakwenda kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikifanya hivyo ninarejea pale ambapo Serikali iliona inakwenda kukuza fursa ya kiuchumi ndio maana fedha hizi zikaelekezwa zile dola milioni 300 zikaenda mikoani. Kuna mfano wa barabara ambazo ni kwikwi tutakuwa tunaimba mapambio hapa kila siku kama hatutekelezi wajibu wetu na kutenda kile ambacho tunachokisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo barabara za mikoani ambayo mikoa inalima, inalima mazao ya biashara, inalima mazao ya mbogamboga, kwa mfano; kama Morogoro kuna barabara ile ya Bigwa – Kisaki ile barabara ni kwikwi lakini wakulima walioko kule ni wengi na barabara ile ikijengwa inaweza kuleta tija ni kwa Mheshimiwa Babu Tale. Lakini ipo barabara ile ya Iringa ambayo inapita Lujewa, Madibila mpaka Mafinga ile barabara ni ya kibiashara kule wapo wakulima, wapo watu ambao wako pale wanalima mahindi ikitengenezwa vizuri inaweza kuimarisha pato la mtu mmoja mmoja lakini kuimarisha pato letu la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara ya Njombe – Kibena kuelekea Lupembe mpaka Madeke kule kuna wakulima wa parachichi. Tunaachaje kutengeneza barabara hizi za kimkakati. Kama lengo letu ni kukuza fursa za kiuchumi na kibiashara twende tukaangalie hizi barabara za kimkakati. (Makofi)

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, TAARIFA.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumpa taarifa Mheshimiwa mzungumzaji anayezungumza hivi sasa kwamba barabara ile ya Kibena stop Lupembe, Madeke barabara ambayo inaunganisha mkoa na mkoa. Kweli kuna umuhimu sana wa barabara hizi kujengwa kwa kiwango cha lami na Serikali ipo hatua nzuri ya kutengeneza barabara hizi kwa kiwango cha lami. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa hiyo.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hii kwa sababu ni kati ya wadau ambao wanalalamika juu ya barabara hizo. Niendelee, naendelea kuainisha barabara za kimkakati kwenye mkoa ule wa Kagera kuna barabara ya Mulushaka, Ukwenda, Mrongo, barabara hii inaelekea mpaka mpakani mwa Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea haya sehemu hizo tumefika sisi wanasiasa tumetembea mtaa kwa mtaa, mkoa kwa mkoa, kwa hiyo tunafahamu kero za nchi hii. Barabara hii ukifika kule mpakani kuna wakulima wa ndizi, kuna wakulima wa kahawa, barabara hii ikitengenezwa tunakwenda kukuza pato la Taifa lakini pato la mtu mmoja mmoja ambayo ndio dhamira yetu ambayo Wabunge tuko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema pia bajeti hii iainishe madaraja. Kuna madaraja ambayo ni sugu watu wanaongea huku kipindi hicho cha bajeti ya Wizara ya Ujenzi na TAMISEMI watu wengi wanaongea juu ya madaraja, vilio kwa kina mama wajawazito wanajifungulia barabarani. Tuainishiwe na madaraja haya ili tuweze kujua fedha zetu inakwenda kutumika vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sasa naelekea Dar es Salaam. Katika Mkoa wangu wa Dar es Salaam, Dar es Salaam ni mkoa wa kimkakati na ni mkoa wa biashara na ni kitovu cha biashara Nchi nzima. Dar es Salaam huwezi kusikia mtu anasimama hapa anaomba viatilifu, anaomba mbolea, anaomba pembejeo. Dar es Salaam tunaomba miundombinu thabiti. Tunaomba miundombinu kwa sababu mpaka Dar es Salaam inaibuka katika Majiji yote kwamba ndio Jiji ambalo linakusanya ushuru mwingi kila siku na kimkoa inashika namba moja ni kwa sababu Dar es Salaam ndio mkoa wa biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam kuna tatizo la miundombinu, nikipita kwako kwenye mitaa ile ya Ilala, ninaona barabara za mitaa bado haziko sawa. Pia maji taka Dar es Salaam ni asilimia 14 tu tumeunganishwa katika mfumo wa maji taka, asilimia 86 ule mfumo wa maji taka umeingiliana na maji masafi huko huko tunakutana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo la mlipuko wa magonjwa ya kipindupindu na magonjwa ya homa ya matumbo. Kila mwaka kipindupindu kinaazia Dar es Salaam, siyo kwa sababu nyingine bali ni mfumo wa maji taka ambayo siyo rafiki. Niombe wakati Waziri anakuja, aje na utaratibu mzuri kwa jinsi gani maji taka yataelekezwa baharini au sehemu nyingine kuliko ilivyo hivi sasa. Dar es Salaam mvua ikinyesha ndiyo wakati wa wananchi wa kupumua na kuanza kucheulisha vyoo vyao na yale mambo yanatapaa barabarani, kwa hiyo siyo salama sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa sababu Dar es Salaam ndio Jiji la kimkakati, wawekezaji wanapokuja kitu cha kwanza wanaangalia miundombinu, kama miundombinu siyo rafiki wawekezaji wanatukimbia. Na Dar es Salaam ndipo wawekezaji wanaanza kushukia pale, kwa hiyo wanaangalia mandhari, pia wafanyakazi wa Dar es Salaam ni uchovu kwa sababu mvua ikinyesha inakuwa ni jam kunakuwa na foleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe wakati Mheshimiwa Waziri unakuja kuhitimisha, uje na mkakati wa miferiji Dar es Salaam, mifereji ambayo inasababisha barabara zetu za lami zinakatika, hakuna miundombinu thabiti ya mifereji, mvua ikinyesha mafuriko watu hawapiti mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii, ahsante sana. (Makofi)