Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii iliyopo mbele yetu ambayo imewasilishwa ili tuweze kuijadili na kuendelea kuweka mapendekezo yetu ambayo tungependa kuona Serikali inayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa namna ambavyo ina watu makini. Naamini haya tunayoyaongea watayachukulia kwa uzito wake na kwenda kuyafanyia kazi. Kipekee pia niungane na wenzangu kumpongeza Mama yetu, Mheshimiwa Samia. Mimi ni mmoja kati ya watu wanaoamini kwamba mama hajawahi kufeli. Kwa hiyo, nina matumaini makubwa kwamba mama atatuletea mambo mazuri ambayo yataenda kuleta mabadiliko katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najivunia kutoka katika Mkoa wa Songwe, mkoa ambao ndiyo unaoongoza kwa ukusanyaji kodi kwa ile mikoa ya ukusanyaji kodi wa kati, Mkoa wa Songwe ndiyo unaongoza. Kwa hiyo, nilitaka nitunze hiyo kumbukumbu vizuri. Kwa hiyo, ninapokuwa nachangia haya nataka kuonyesha kwamba Mkoa wa Songwe ni katika maeneo ambayo Serikali inaweza ikapata fedha nyingi kama wataamua kuufanya mkoa wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote, nilitaka kuongea kwamba ujenzi wa dry port kwa Mkoa wa Songwe eneo la Mpemba pale Tunduma ni kitu kisichoepukika. Tunayasema haya tukiwa tunaamini kabisa Kariakoo na Bandari ya Dar es Salaam kumeshakuwa busy sana. Kama Reli ya TAZARA itatumika ipasavyo, ikawezeshwa na dry port ikajengwa Mpemba, niwaambie kabisa, Kariakoo nyingine itaenda kuota pale Tunduma. Pale itakuwa chanzo cha kuweza kutengeneza free market katika eneo la Tunduma. Kwa maana hiyo, uchumi unaoendelea Kariakoo utakuwa umehamia Tunduma. Kwa hiyo, tutakuwa tumeongeza maeneo ambayo yanaipatia Taifa letu kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo la dry port pale Tunduma, napenda pia kuongelea suala la kupunguza msongamano wa magari pale Tunduma. Ni kweli kuna mkakati wa ujenzi wa barabara, lakini ipo haja ya kufanya haraka kuhakikisha barabara ile ya pale Tunduma inayoingia mpakani inatanuliwa ili magari yasipate msongamano wa kuelekea Zambia. Kwa sababu kwa kitendo cha magari kukaa njiani muda mrefu pale, kwa namna moja au nyingine yanaiingizia hasara Taifa kwa maana ya kwamba magari hayavuki mengi kwa wakati ipasavyo; na pia hakuna barabara ya mchepuko endapo barabara ile itapata breakage, hakuna barabara ya kutoa magari yapite njia mbadala yaweze kwenda kuingia boda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo mambo pia naomba kama Wizara yayachukulie kwa u-serious wake na kuyafanyia kazi haraka. Uchumi wa Taifa hili kwa upande wa Tunduma kama kweli patapewa kipaumbele, naamini kabisa Taifa litapata mapato mengi kutoka eneo la Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye suala la VAT. Sheria ya Ongezeko la Thamani inasema kwamba ili mtu aweze kusajiliwa kuwa Wakala wa kukusanya VAT, awe na mzunguko wa shilingi milioni 100. Ukijaribu kulitazama kwa kina hili jambo linakuwa ni kama ni gumu katika utekelezaji wake kwa wale Maafisa Mapato wanaokuwa wamepewa hii kazi. Unapoongelea mzunguko wa shilingi milioni 100 ni kitu cha kawaida kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kupata mzunguko wa shilingi milioni 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposema hiyo shilingi milioni 100, ina maana unawalenga wale watu wanaofanyabiashara ya rejareja. Unaposema ongezeko la thamani, hatuna maana kwamba bidhaa hiyo moja iweze kuongezeka thamani kila inapoenda kwa muuzaji mwingine.

Ushauri wangu ulikuwa ni kwamba, tungependa kuiona Serikali inafanya mabadiliko katika eneo hili. Kutoka shilingi milioni 100, basi iende kufanya kuwe na shilingi milioni 300. Unapomwongelea mfanyabiashara mwenye mzunguko wa shilingi milioni 300, huyu ni stable person ambaye yeye kwa shilingi milioni 300 yake hiyo anakuwa ni supplier wa bidhaa na siyo yule mfanyabiashara wa rejareja. Kwa hiyo, kama kweli Serikali ikiweza kuliona hili na kulifanyia kazi. Ina maana kwamba kwa namna moja Serikali itapunguza mgogoro na wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu kule mpakani tuna mgogoro mkubwa sana kati ya TRA na wafanyabiashara. Wafanyabiashara wengi hao wenye mzunguko wa shilingi milioni 100 wamekuwa wanalazimika kufunga biashara zao kwa sababu tu hawawezi kulipa hilo ongezeko la thamani. Kwa kitendo cha kuwaingiza wao kwenye ongezeko la thamani, ina maana kwamba unawafanya washindwe ku- compete kibiashara katika lile eneo la Tunduma, kwa sababu wapo ni registered wapo ambao ni un-registered. Wale wanaokuwa registered ina maana kwamba sasa wanashindwa kuuza bidhaa zao kwa ile bei ambayo ipo sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo la kuongeza kutoka shilingi milioni 100 hadi kwenda shilingi milioni 300, kinachofanyika ni kwamba, wafanyabiashara wengi pia wanafilisika, kwa sababu kinachokuja kutokea yale malimbikizo inakuwa kama wanapokwa zile fedha zao kiasi kwamba wanakuwa hawezi tena kuendesha biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuongelea suala la ushuru wa forodha wa vitenge. Kuwepo kwetu mpakani tunaendelea kujifunza mengi. Kwa wastani kontena karibu milioni 500 zinapita kuelekea Zambia na Kongo pale katika mpaka wa Tunduma. Mwisho wa siku nikuhakikishie, pakifanyika uchunguzi zile kontena 500 sidhani kama zote zinatumika kwa Zambia au kwa Kongo, zinarudi tena Tanzania. Changamoto iliyopo ni kwamba kodi ya vitenge kwa Tanzania ni asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote ni mashahidi kwamba vitenge vinavyotengenezwa nchini havina quality hiyo ambayo tunataka kuvilinda. Vingekuwa ni vitenge vizuri, ambavyo vina mvuto, naamini kabisa ingekuwa sawa kweli kuweka hiyo kodi ambayo ipo. Mwisho wa siku ukienda Zambia unakuta wao wana kodi ya asilimia 20, ukienda Kongo ni asilimia 25. Unapopitisha kontena la fourty fits kwa Tanzania unalipa zaidi ya shilingi milioni 100, lakini kwa Zambia na Kongo inakuwa ni chini ya shilingi milioni 30. Katika hali ya kawaida gap ya shilingi milioni 70 siyo ya kitoto, ni fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku, pale mpakani tuna watumishi 12 tu ambao wana-deal na mpaka Maafisa Kodi, hawawezi kukimbizana na kontena 500 zote hizi kwa mwezi.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza sasa kwamba kupitia hilo ni kweli kabisa na jambo hilo limesababisha wafanyabiashara ambao walikuwa wanafanya biashara Kariakoo ambao walikuwa ni majirani zetu; Zambia, Malawi, Rwanda na Burundi ambao walikuwa wanajaa pale Kariakoo kununua bidhaa hii ya kitenge, sasa hivi hawaji na wafanyabiashara hawa wamehama, wanaenda kwenye nchi hizo hizo kwenda kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ni kweli kabisa hata Kariakoo wamekimbia, kontena moja shilingi milioni 300. (Makofi)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niseme tu, taarifa yake naipokea na hali halisi ndiyo ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema heri nusu shari kuliko shari kamili. Kitendo cha kwamba tunapoteza fedha nyingi kisa tu, kuhakikisha tunalinda viwanda vyetu vya ndani ambavyo havifanyi vizuri, tunakuwa hatujitendei haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niseme, sisi wenyewe ndiyo tunahamasisha magendo; na kwa…

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa. Niko hapa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa kweli niungane na hawa waliopita kuhusiana na masuala ya vitenge. Kweli kuna jambo inabidi tuliangalie vizuri sana. Nasema hivyo kwa sababu hata mimi nililifuatilia na nikalishughulikia suala hilo kwa muda mrefu. Kuna changamoto kubwa na wale akina mama wamekuwa wakilipa kodi ya kutosha. Tunalinda viwanda vya ndani ambavyo na vyenyewe ukivichunguza wanadai kwamba wanaenda kununua huko huko nje, halafu wanarudi wanasema wametengeneza ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliangalie hilo suala kwa umakini kwa faida ya nchi yetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Taarifa hiyo, Mheshimiwa Neema.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Manyanya. Tunachohitaji ni pesa za kuendesha Taifa letu. Tuangalie namna zote ambazo zinazuia tusipate pesa. Suala la vitenge nimeona kwenye hotuba inasema kwamba wanamwachia Kamishna. Tuwe wakweli, kumwachia Kamishna wa TRA ni kuongeza urasimu na kutengeneza mianya ya rushwa. Kwa maana hiyo, nilitamani hili wakalitafakari na waje na percent, ile asilimia ambayo kweli kama Taifa tutakuwa tunajua hiki tutapata na hiki kitatuongezea kitu kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme kabisa magendo kwa nchi hii tusiendelee kuhamasisha kwa kuweka kodi zisizolipika; na pale mpakani nimeshasema watumishi ni 12, sidhani kama wata-deal na sukari, wata-deal na magendo yote yanayopita pale, hawataweza. Otherwise iongezeke timu ya kufanya kazi katika mpaka ule. Ule mpaka ni wa faida, ule mpaka una pesa, ule mpaka unaweza ukalisadia Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nirudi kusema kwamba nina maombi mengine maalum kwa Wizara. Songwe tungependa kuona kilimo cha Alizeti na Ufuta kinapewa kipaumbele. Nimeona wameitaja mikoa mitatu. Taifa hili tunahitaji mafuta, tunahitaji mbegu za mafuta zilimwe kila sehemu. Songwe tumekuwa tunalima mahindi, ndiyo yenyewe hayauziki. Hatuna kilimo ambacho tunaweza tukajivunia kwamba hiki ni kilimo cha biashara. Naomba watuzingatie watu wa Mkoa wa Songwe kwa kuhakikisha zao la alizeti na ufuta linapewa kipaumbele na wananchi wanahamasishwa ili tuweze kuchangia uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuongelea suala la TFS. TFS kuna changamoto kubwa. Wanatoa vibali kwa wananchi vya uvunaji wa mkaa, mvunaji wa mkaa anapata nafasi ya kuweka watu wake wa kumvunia mkaa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia kidogo, samahani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuvuna mkaa vibali vya kutoa mzigo porini watu wautoe kwa wakati havitolewi kitu ambacho wafanyabiashara wengi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema, unaweza ukamwandikia Waziri wa Fedha kwa sababu wengine watakosa nafasi.