Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Narudia kumpongeza sana Waziri wetu wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri Engineer Masauni. Naomba pia nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ndugu yangu Mheshimiwa Daniel Sillo, lakini na Makamu Mwenyekiti CPA Mheshimiwa Omari Kigua kwa kutuwakilisha vyema kama Bunge kwenye Kamati ya Bajeti na hasa katika vikao vya mwisho vya majumuisho ya bajeti hii. Tunawashukuru sana Kamati ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono bajeti hii na mapendekezo yake yote. Naiunga mkono bajeti hii kwa sababu inakwenda kuendelea na kukamilisha miradi ya maendeleo au miradi mkakati ambayo inafanyika sasa hivi Stigler’s Gorge, SGR na mingine mikubwa. Bajeti hii inaenda kuendeleza na kukamilisha miradi hiyo, lakini inaenda pia kuanzisha miradi mipya ambayo tumeainishiwa katika bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bajeti hii inaelekea kwenda ku-trickle down economic na ku-stimulate economic activities zilizopo kwa wananchi wake. Kwa nini nasema hayo bajeti hii pia leo tumeambiwa inakwenda kupandisha madaraja ya wafanyakazi. Naomba niseme hapa mpaka leo hii wafanyakazi karibu zaidi ya 86 wameshapandishwa madaraja na automatic wanaenda kupandisha mishahara yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ya upandishaji wa mishahara hii itaigharimu Serikali bilioni 300, lakini pia malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi karibu bilioni 96 yanaenda kulipwa. Kwa hiyo ndiyo maana naipongeza Serikali na wafanyakazi maslahi yao yakitazamwa na yakipanda maana yake ni nini? Hawa ndiyo spender wakubwa na hawa waki-spend ndiyo Serikali inakusanya kodi yake. Hizi kodi zote tunazozisema hapa za simu sijui za nini tulizozipendekeza watumiaji wakubwa wakiwemo pia wafanyakazi, ndiyo wanafanya miamala mikubwa, ndiyo wanaotumia hela nyingi kupeleka sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake wanayoiongoza. Tangu Mheshimiwa Rais ameapishwa Samia Suluhu Hassan katika wilaya yetu ya Namtumbo katika kipindi hiki toka Aprili mpaka sasa hivi ametuletea bilioni mbili na milioni mia saba sabini na saba na milioni thelathini katika miradi ya elimu, afya, program endelevu ya maji safi na mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametuletea pia milioni 500 za barabara kwa ajili ya TARURA, lakini pia tunategemea kupata milioni 600 kwa ajili ya sekondari zetu za kata, naomba sana nimpongeze Rais wetu na Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye aya ya 110 katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, alizungumzia eneo la utamaduni wa kuheshimu mali na rasilimali hapa nchini; mali za Umma na binafsi. Naomba nimnukuu: “kwa upande wa Mali za Umma lazima tutangulize uzalendo na uadilifu tunapotekeleza majukumu yetu. Serikali inapoteza fedha nyingi kwenye kutekeleza Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kutojali thamani ya fedha kwa miradi. Watumishi wa Serikali wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kuongeza gharama za miradi ikilinganishwa na gharama halisi ingawa wanafuata taratibu zote za manunuzi. Taratibu za manunuzi zinapokamilika, watumishi na wafanyabishara hawa hugawana fedha na kiasi kidogo tu kilichosalia ndicho kinaelekezwa kwenye miradi husika na hatimaye miradi hiyo kuwa chini ya kiwango.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno alisema Waziri wa Fedha katika hotuba yake. Ni kweli, nakubaliana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hili. Kuna haja ya kukazia eneo hili, kuheshimu kutunza Rasilimali za Umma, kwani ni kweli Serikali inapoteza fedha nyingi kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa, tumepata zaidi ya shilingi 2,700,000,000 zinakwenda katika Halmashauri zetu. Miradi hii inaongozwa na bajeti au inaongozwa na mwongozo wa kuhudumia miradi hiyo kwa Force Account. Mwongozo unasema, kuna Kamati ya Ujenzi, Kamati ya Manunuzi, Kamati ya Mapokezi na Kamati ya Ufuatiliaji. Kamati hizi ni za wale wananchi husika pale, lakini watumishi wa Halmashauri wanakuwa Wajumbe kama washauri na kusimamia ili shughuli iende sawa sawa kwa mujibu wa taratibu na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo inajitokeza baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu, wao sasa ndio wanachukua majukumu yale ya kufanya ununuzi na kufanya ujenzi. Sasa hii inasumbua sana na inaleta audit query kwenye Halmashauri zetu. Leo hii sisi tuna audit query pale zaidi ya milioni 120 kwa ajili ya mradi tu ambao haukufuata taratibu hizi. Kwa hiyo, naishauri Serikali, tunaomba mumpe nguvu Mkuu wa Mkoa wawe wanasimamia miradi hii ya maendeleo. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa isimamie kama taratibu zinafuatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni aya ya 75; Serikali katika eneo la kilimo, imependekeza katika miradi ya umwagiliaji kwamba itakuwa inatoza 5% ya mavuno katika miradi ile ya umwagiliaji. Nia ni njema, naiunga mkono kwa ajili ya kuendeleza kufanya service miradi yetu ya umwagiliaji. Hata hivyo, nina mapendekezo mawili. Kwanza, kuangalia hii miradi yote. Kuna miradi ambayo fedha nyingi za umwagiliaji zimeingia kule, lakini haijakamilika miaka nenda, miaka rudi. Naamini katika kanzidata ya Serikali inaonesha kwamba kuna fedha zimepelekwa katika miradi lakini miradi ile haikukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri hapa, kwamba kwa wale wasiokuwa waaminifu, hawakukamilisha miradi, sasa tozo hii lazima yatoke maelekezo kwamba kwanza tukakamilishe ile miradi ndipo tozo zianze kuchukuliwa. Maana yake tukitoa tu tozo, miradi isipokamilika na ile ambayo hai-perform vizuri, tozo zitaanza kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima ifanyike tathmini ya miradi ambayo haijakamilika ili tuikamilishe ndiyo tozo hizi ziweze kuwapa wale wakulima wananchi kule, kuliko kupeleka tozo, wataenda kukamatwa hawajalipa tozo, wakachukuliwa tozo zao, miradi ile haikukamilika. Pili, tozo hizi tuelekeze wazi wazi zinakwenda wapi? Kama zinakwenda kwenye Tume ya Umwagiliaji, tujue; zisije kuwa tozo hizi zinakwenda kuchukuliwa tu kwenye Halmalshauri halafu zinaanza kupangiwa matumizi mengine baada ya matumizi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nami niungane na wenzangu, kwanza kabisa kwenye hili suala la Madiwani, Watendaji na Makatibu Tarafa kupewa na Serikali fedha zao na posho, naunga mkono kabisa. Naipongeza sana Serikali kwa kuamua kufanya jambo hili jema sana kwa ajili ya watumishi hawa. Ushauri wangu ni kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)