Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa uzima ili niweze kusimama hapa leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kuzungumzia Mkoa wa Ruvuma, Mkoa wa Ruvuma kwa maana ya kuugawa. Tunapozungumzia maendeleo, ukuaji wa uchumi katika nchi yetu ya Tanzania, imetosha tu kwamba tuzungumzie pia na mikoa ambayo ni mikubwa sana, mikoa ambayo kwa ukubwa wake inasababisha huduma za msingi zinashinda kufika kwa wakati na kuweza kutosheleza kwenye maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Ruvuma una population ya watu 1,376,891 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 na sisi kule watu wa Ruvuma tunazaana sana, mpaka sasa hivi maana yake wakija kufanya sensa tunaweza tukawa tumefikia watu 2,000,000. Kwa misingi hiyo, naomba sana Mkoa wetu wa Ruvuma uwe ni miongoni mwa mikoa inayoenda kugawiwa ili tuweze kupata mikoa miwili sasa uwe Mkoa wa Ruvuma na uwe Mkoa wa Selou na vigezo vipo na niseme tu kwamba hii ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipokuja Mkoani kwetu Ruvuma alizungumzia kuugawa huu mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoa huu kwa kukuthibitishia tu naomba nitoe vigezo vya mikoa mingine ambayo ina population ya watu wachache sana, lakini imepata mikoa. Nataka nizungumzie Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Katavi una population ya watu 564,000 tu, tofauti na Mkoa wa Ruvuma ambao kwa sasa una watu 1,376,891. Mkoa wa Njombe una population ya watu 702,000 tu, Mkoa wa Lindi una population ya watu 964,000 kwa hiyo ni wazi kwamba Mkoa wa Ruvuma unakidhi vigezo vya kuongeza mkoa, kwa hiyo tunaomba tupate mkoa mwingine mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Waziri wa Miundombinu ya barabara, lakini pia nimshukuru Waziri wa Fedha kwa namna ambavyo ametuheshimisha Wanaruvuma na niseme tu kwamba nampa big up sana Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Peramiho ambaye barabara hii ya Likuyufusi – Mkenda inapita kwenye jimbo lake. Kwa pamoja yeye akifuatilia kwa ukaribu kabisa sambamba na mimi winga machachari ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimekuwa nikiizungumzia sana barabara hii yenye urefu wa kilometa 124 inayotoka Likuyufusi kwenda Mkenda ambayo inaunganisha Nchi ya Tanzania na Mozambique.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha akumbuke kwamba, sasa hivi hii ni bajeti yake ya kwanza akiwa Waziri wa Fedha na kikubwa kinachotakiwa ni kuendelea kujenga nchi yetu ya Tanzania iendelee kukua kiuchumi. Kwa hiyo barabara hii atakapoijenga itaendelea kufungua fursa nyingi za kiuchumi na kodi italipwa na nchi yetu itaendelea kukua, wananchi watapa ajira na wananchi wetu wa Mkoa wa Ruvuma wataendelea kunufaika na rasilimali za nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nataka nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mama yetu jemedari Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya, mwanamke shupavu, mwanamke mahiri, kwanza Mungu kamjalia, kwanza kabisa ukimwangalia sura yake nzuri, sura ya upole, mama mwenye upole, mama mwenye upendo. Kwa misingi hiyo mama huyu ana upendo mpaka ndani ya moyo wake, kwa bajeti hii ambayo imeletwa safari hii, ni bajeti ya kupigiwa mfano, bajeti nzuri ambayo imeenda kugusa moja kwa moja kwa wananchi wanyonge na kukwamua matatizo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe kupitia Bunge lako Tukufu, Watanzania wote waweze kumuunga mkono Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kulipa kodi. Watakapolipa kodi ndipo hapo tutapata maendeleo kupitia ujenzi wa barabara, umeme, maji, afya na elimu. Kwa misingi hiyo kulipa kodi ndiyo maendeleo ya nchi yetu. Niseme tu, kupitia malipo mazuri ya kodi, basi maana yake itakwenda kuboresha hata sisi Wabunge hapa, amesema mama yetu Mheshimiwa Samia kwamba anaanza na kuboresha mishahara ya watumishi, maslahi ya watumishi ikiwa pamoja na kuwaongezea vyeo vyao ili waweze kuendana na wakati huu wa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu, atakapoboresha baada ya kodi kulipwa na sisi Wabunge hapa tutakwenda vizuri, mambo yetu yatakwenda vizuri. Itoshe tu kusema kwamba ikimpendeza Mungu panapo majaliwa kama jina litarudi wakinipa hawa nafasi maana yake nitasimamia katika kamisheni ya Bunge kuhakikisha kwamba maslahi ya Wabunge kupitia safari za kwenda nje ya nchi, kwa sababu Mbunge kama Mbunge ni lazima upate exposure, kwa maana ya kwenda kujifunza nje ya nchi katika nchi ambazo zimefanikiwa sana kwenye miundombinu, afya, elimu na mambo mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo bila Mbunge kupata exposure maana yake tunakuwa tuna mawazo ya kwetu tu hapa ndani ya nchi bila kwenda nje ya nchi. Hii niwaambie tu ndugu zangu kama mkiniwezesha mambo hayo yakakaa vizuri maana yake nitasimama kindakindaki. Mjue kabisa kwamba uwezo ninao wa kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nizungumzie suala la namna ambavyo Mama Samia ameboresha kwenye masuala ya Madiwani. Madiwani sasa hivi wanakwenda kulipa pesa zao kupitia Serikali Kuu. Kwa msingi huo kulipwa tu kupitia Serikali Kuu haitoshi, ilitosha tu hawa Madiwani waongezewe pesa. Madiwani hawa ndio ambao wanafanya kazi asubuhi, mchana, jioni wao ndio wanakutana na wananchi kule chini kwenye grass root kwa hiyo hawa Madiwani katika utendaji wao wa kazi bado mzunguko wa maeneo yao waliyonayo ni mkubwa mno kiasi ambacho sasa yule Diwani, wakati mwingine unakuta Diwani ana vijiji 12, 15, vijiji nane, vijiji tisa au vijiji 20. Kwa hiyo, naomba kupitia bajeti hii itoshe tu kwamba Waheshimiwa hawa Madiwani waweze kutengenezewa utaratibu wa kupata mkopo kwa ajili ya kupata usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo usafiri utawasaidia kama vile ambavyo Makatibu Tarafa wameweza kusaidiwa usafiri, wakapata pikipiki, lakini pia Watendaji wa Kata wameweza kusaidiwa wanapata posho. Waheshimiwa Wabunge mengine hatuwezi kusema hapa, mkinipa kale ka mambo kale ndio nitasema vizuri huko na nataka niwaahidi kwamba nitakuwa shujaa wenu na sisi Wangoni tulishakuwa mashujaa, kwa hiyo huu ni mwendelezo tu, tulikuwa mashujaa, tumepigana vita na Wajerumani na hata nyie mkawa mna nafuu huko mliko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, naunga mkono hoja. (Makofi)