Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi pia na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, hasa kwenye bajeti hii kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukuwe nafasi hii kumpongeza sana Waziri na timu yake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya, aliongea Mheshimiwa Jerry hapa juzi kwamba umeupiga mwingi sana kama wa Morrison, nadhani na staili ya kuupiga ndiyo staili vijana wanaitumia zaidi, hata jana Mama aliyoyafanya Mwanza kule vijana wanapo- comment wanasema Mama anaupiga mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuseme kwa kweli kutoka ndani ya kilindi cha moyo wangu nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wako kazi mliyoifanya ni kubwa, bahati mbaya siku inasomwa bajeti sikuwepo nilikuwa na msiba kwa hiyo nikawa niko kwenye mazishi ya Babu yangu Biharamulo lakini nilipokuwa njiani narudi nikawa napitia comments nyingi sana kuna watu waliitisha press conference. Ukiona mtu anaitisha press conference anakosa kitu cha kukosoa humu kwenye bajeti anaishia kusema bajeti haijaongelea Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchuguzi uelewe kwamba umemaliza kila kitu. (Makofi)

Kwa hiyo niwapongeze juu ya hilo kazi iliyofanyika ni kubwa sana, pia nimpongeze Mama kwa kazi kubwa ambayo ameifanya tangu ameingiea madarakani ni muda mfupi lakini watu tunaona matokeo chanya kabisa kabisa hasa kwa niaba ya wananchi wa Biharamulo nishukuru kwa milioni 500 za ujenzi wa barabara ambazo zinaingia kupitia TARURA na tayari tumeshakubaliana tuongeze kilometa moja ya lami pale hili tuweze kuchochea maendeleo haraka zaidi. Hali kadhalika na suala la shule ya sekondari, kuna shule sasa tumekubaliana inaenda kujengwa pale Nyakaula pale ni eneo ambalo lilikuwa na wanafunzi wengi zaidi kwa hivyo tutaongezea shule ya pili ili maendeleo haya ambayo Mama anayasema kwa vitendo na wao wayapokee haraka zaidi ili waweze kuunga mkono juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya labda lipo jambo moja ambalo mimi ningependa nijikite nalo, mimi ni mdau wa viwanda kwa hiyo nadhani mchango wangu kwa sehemu kubwa una- base zaidi katika masuala ya viwanda, mpango wetu wa maendeleo wa miaka mitano ijayo 2021/2022 - 2025/2026 dhima yake kubwa inasema ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi tangu nimeanza kuchangia mara nyingi sana nimekuwa ninagusa masuala ya viwanda kwa sababu ni area yangu ambayo nimekuwa nikitumika kwa muda mrefu kwa hiyo napenda nichangie kitu ambacho nina experience. Kwanza ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, kwa hiyo nichukuwe pia nafasi hii sana kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo ambayo aliyatoa juzi hasa suala la Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niko kwenye Kamati na bahati nzuri tumefanikiwa kufika site pale kwenye ziara ya Kamati, mradi huu ni mradi ambao unaenda kuliinua Taifa hili na kutupeleka mbele zaidi. Ukipitia ripoti zote ripoti ya NDC inasema, lakini pia jambo moja ambalo nimekuwa nikiliona kwa upande wangu na upande profession yangu tunachokikosa hapa mpaka mradi huu unachelewa ni technology tu! Technology ndiyo inayotutesa leo tungelikuwa na uwezo tuna wataalam wa Kitanzania pale tungeshatia timu na hii kazi ingekuwa inafanyika leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiangalia ripoti NDC, total investment cost ambayo huyu Mchina anakuja kuweka pale ni three billion US Dollars. Sasa ukiangalia three billion US Dollars, tunajenga reli leo inatumia thamani kiasi gani? Wakati ule ni mradi wa kibiashara kwa sababu anaweka three billion USD, na income per year – hii ni ripoti ya NDC – income per year itakuwa ni 1.736 billion USD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani anaweka bilioni tatu mtaji, baada ya mwaka mapato ni 1.736 billion USD. Kwa hiyo baada ya miaka miwili tu alichokiwekeza pale kashakipata na kila kitu kinakwenda sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo unaweza kuona kwamba kinachotutesa pale mpaka leo ni transfer of technology. Ndiyo maana mimi kwenye michango yangu mingi sana nimekuwa naomba, tujaribu kusikiliza jinsi ya kulinda viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojaribu kulinda viwanda vya ndani hatulindi tu kwa sababu tunazuia wale watu wasilete au wasifanye nini, tunawawezesha vijana wetu wa Kitanzania kupata knowledge ya how they can work on these industries ili waweze wao wenyewe kesho na kesho kutwa kutumia experience waliyoipata kwenye viwanda watusaidie kujenga viwanda vingine hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, sasa niombe, na nadhani hapa tuko sawa, kwamba kuna watu wameweza kuelezea sana suala la importation. Nilichangia juzi nikielezea suala la importation of traders, sitaki sana kurudia kule, lakini tumeona kwamba viwanda vilivyokuwepo hapa vingi vilikufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tutakapokwenda kuvinyanyua viwanda hivi maana yake tuna-transfer technology hata kwa vijana wetu wanaosomea mechanical engineering katika vyuo vyetu, vijana ambao wanasoma VETA, maana tunafungua vyuo vya VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unafungua vyuo vya VETA tuna-invest billions and billions kwenye VETA halafu hatuna viwanda, hawa watoto tunawapeleka wapi baada ya hapa? Investment tuliyoifanya kwenye vyuo vya VETA tunaipeleka wapi baada ya hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunachoomba ni kwamba tujikite zaidi kwenye kuwezesha viwanda vya ndani. Kwanza niwashukuru na kuwapongeza, kwa mfano ishu ya tiles tunajua wengi sana wakienda madukani wanataka Spanish tiles. Sasa ili kulinda viwanda hivi ambavyo vimejengwa kwenye Mkoa wa Pwani, mmeona, mmeongeza asilimia 35, kwamba sasa import duty iwe 35%; unampa mtu chance ya kuchagua premium.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tajiri anayesema anataka akajenge kwa Spanish tiles maana yake anatuongezea asilimia kwenye import duty. Anavyoleta hapa zile tiles ili waweze kuzinunua hapa Serikali inapata kodi ya kufanya vitu vingine, lakini huku tukiendelea kuvilinda viwanda hivyo ambavyo vimejengwa hapa kwa ajili ya kuwaajiri Watanzania na kutumia malighafi za Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe sambamba na hilo, ninakumbuka hata ishu ya REA. Nilikuwa napitia ripoti ya REA hapa, wakati mnaanza miaka mitano iliyopita, wakati tunaanza kufanya miradi hii ya umeme nakumbuka walio wengi walikuwa na wasiwasi kwamba je, tutapata capacity? Tutakuwa na uwezo wa kuzalisha hivi vitu hapa nchini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unapoweka sera nzuri kinachotokea ni nini? Hili likishakuwa soko la tajiri fulani ambaye ana viwanda kule nje, anapoona soko lake halifanyi kazi, anachojaribu kukifanya lazima alifuate soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ambaye amesha-invest na anajua soko lake ni Tanzania, amekuwa anapata bilioni 50 au 30 kutoka Tanzania anapofanya biashara, yule mtu ukimwambia tumezuia importation au importation anaona inakuwa kubwa anashindwa ku-compete, anachokifanya anatoka kwenye nchi yake anakuja kuwekeza hapa. Akishawekeza hapa tayari anatutengenezea biashara kwa sababu anataka alinde soko lake ambalo amelipata Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunachoomba, lazima tujaribu kuangalia, mtusaidie kwenye hili. Lakini kipindi mnatusaidia kwenye hili, kwamba sasa tujaribu kuvutia wawekezaji na kuweka conditions ambazo zitalinda viwanda vya ndani, lakini vilevile twende step moja mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijaribu kuchangia hapa last time nikasema hatuwezi kujenga viwanda vyote Mkoa wa Pwani. Pwani haitaenea. Maana bada ya hapa na sisi vilevile huko mikoani tunahitaji viwanda viwepo. Tunapotamka viwanda hatutatakuja kila siku tunalia viwanda vijengwe Chalinze au Dar es Salaam wakati hata mimi huko Biharamulo, Kigoma na wapi, na sisi tunataka viwanda hivi. Ili sasa mwekezaji atoke aje kuwekeza Kigoma, Biharamulo, Arusha, Mtwara au Mbeya lazima tuoneshe kwamba kuna incentive fulani tunampa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, jana Mheshimiwa Mavunde kaongelea hapa suala la income tax. Tujaribu kuona, huyu mtu anapata advantage gani akija Kigoma? Maana atoe kontena Dar es Salaam, alipeleke Kigoma halafu amalize arudishe tena kuuza Dar es Salaam. Anafanya double kwenye transportation, hataweza kushindana na mtu aliyeko Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tujaribu kuona jinsi ya kuweza kuwasaidia. Hata kama ni income tax, mpe grace period. Mwambie labda akiwekeza Bukoba au Buharamulo mnampa chance ya kutokulipa income tax kwa miaka mitano au mingapi, au vinginevyo mpunguzie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yule mtu ataangalia, atapiga hesabu na benki yake then atajua aende akawekeze wapi. Hapo tutakuwa tunatanua uchumi na kusambaza viwanda kwa ajili ya watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa najaribu kulipitia hapa ni mazingira mazuri ya uwekezaji ili watu waweze kuwekeza. Hilo jambo mmeliahidi, Mheshimiwa Waziri ninaomba mkalisimamie maana kipindi cha nyuma kilio kilikuwa kikubwa. Lakini kwa sababu bajeti yako imesema na bajeti imesema mawazo ya Wabunge kwa kweli mimi sina budi kushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hata Wabunge tunaondoka hapa kifua mbele kwa sababu miezi mitatu tuliyokaa Dodoma tunaishauri Serikali, kwa sehemu kubwa mambo mengi yametekelezwa na mambo mengi yamekuwa incorporated hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata sisi tunaporudi huko nyuma, kesho na keshokutwa hata tunaporudi kwenye Bunge lingine tuna uhakika kwamba tunachokishauri hapa Serikali inasikia. Na hii ndiyo kazi yetu sisi, kuwashauri ninyi, ili ninyi msikie wananchi waliyotutuma muende mkayafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa kumalizia, niliongelea suala la trailers, naomba hili jambo ulichukulie serious kwa sababu nina experience nalo. Tumeongea, si mimi tu, naona watu wengi, nililianzisha lakini watu wengi sana wameweza kuliongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, import duty, unajaribu kuangalia magari yanazalishwa hapa, trailers hizi. Tunachojaribu kuangalia, tuvute wawekezaji waje, hata HOWO trucks. Tumeona HOWO ziko nyingi sana hapa. Ongeeni na yule mtu mwenye HOWO kule. Kwa sababu hii ni bandari ambayo ina-serve nchi zaidi ya tisa, tukimwambia aje awekeze hapa akaja na spea, akajenga kiwanda hapa cha kufanya assembling, kama leo wanavyo-assemble magari pale Kibaha, wana-assemble mabasi yameanza kutoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ataajiri Watanzania. Tunahitaji ajira kwa ajili ya Watanzania maana wanalipa SDL, wanalipa PAYE, wanalipa vitu vingi zaidi. Lakini chanzo kikubwa cha kutengeneza ajira milioni nane, tutazipata tutakapovutia wawekezaji wakaja hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe hilo jambo uliangalia, suala la duty kwa ajili ya trucks, hizi trailers, tuone jinsi tunavyoweza kuzipandisha nazo ili wawe competitive na waweze kushindana na watu wengine hapa. Maana huna haja ya kuichaji IST asilimia 25 halafu mtu anayeleta gari kubwa lenye thamani kubwa ya kutupa kodi kubwa bado anachajiwa asilimia kumi. Hili jambo naomba milaingalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze. Mimi sina jambo la kuongezea zaidi ya kushukuru kwa hotuba nzuri na yote ambayo mmeyaweka ambayo tumeyachangia hapa. Mungu awabariki sasa tunapokwenda kuyatekeleza ili sasa kwa sababu ninyi ndio wenye pesa, kuna mambo mengine ambayo tumeyasema hapa yanahitaji pesa, mkaweza kuzitoa hizi pesa kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa kumalizia; TBS tumewapa kazi nyingi sana. TBS leo ndio anayekagua magari, kazi iliyokuwa inafanyika Japan; TBS leo ameacha mkataba na SGR ndiye anayekagua pre-export verification anafanya yeye; TBS tumempa vinasaba ndiye anaanza kuweka vinasaba kwenye mafuta ya petroli. Kwa hiyo kwenye Bunge hili tumempa kazi nyingi sana TBS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachoomba, ili TBS asituangushe kwa sababu hizi kazi ni continuous, atahitaji bajeti ya manpower, atahitaji bajeti ya kununua vifaa. Ninaomba mtenge pesa na TBS apatiwe hizi pesa haraka ili isije ikawepo sababu sasa kwamba TBS tulimpa kazi na ameshindwa kufanya kazi huku akiwa anakwamishwa na ninyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)