Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Humphrey Herson Polepole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Nami naomba niungane kwanza na Wabunge wenzangu kuunga mkono kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupeleka maendeleo kwa watu wetu wa Tanzania.

Kwa upekee mkubwa sana, napenda kumpongeza kwa dhati mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa matukio makubwa ya kihistoria ambayo ameyafanya katika ziara yake ya Mwanza kwa siku tatu mfululizo. Hapa napenda kuweka msisitizo katika uzinduzi na ufuatiliaji wa miradi mikubwa ya kimkakati itakayokwenda kubadilisha maisha ya watu wetu Watanzania na hasa katika kanda ya ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameshuhudia utiwaji saini mikataba mitano ya ujenzi wa meli kubwa katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na bahari ya hindi. Meli hizi, katika uchumi kuna njia kama tatu za usafiri; ya kwanza ni usafiri wa maji; pili ni usafiri wa reli; tatu ni usafiri wa barabara; nne ni usafiri wa ndege. Zimepangika hivyo kwa maana ya unafuu wa njia za usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira njema ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwekeza zaidi katika usafiri wa kwenye maji, unadhihirisha mwelekeo mzuri wa kusafirisha mizigo mikubwa kwa bei nafuu; na hapa ninaangazia soko lote la Afrika Mashariki. Tutaweka wagon ferry pale yenye kubeba tani 2,800 maana yake hiyo ni sawasawa na kuingiza treni kama tatu hivi za mizigo zitakazotoka Tanzania kwenda Kenya au kwenda Uganda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile itajengwa meli ya kubeba uzito hivyo hivyo wa tani zaidi ya 2,800 ambayo sasa ninaona makaa ya mawe kutoka kusini mwa Tanzania mpaka bandari ya Mtwara kama alivyosema pacha wangu pale, yatatembea kwa maji kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam na mpaka Tanga Cement badala ya kutumia usafiri wa barabara ambao unagharimu nchi yetu fedha nyingi kwa kufanya routine maintenance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka jiwe la msingi la kuzindua ujenzi wa reli ya kutoka Mwanza mpaka Isaka, reli ya kiwango cha Kimataifa, Standard Gauge Railway. Hapa nataka nimtie moyo kwamba akifika Isaka atusaidie kutafuta fedha akamilishe kipande kutoka Isaka mpaka huku Dodoma; na tutoke Dodoma mpaka Tabora - Kaliua hiyo mpaka Kigoma na tukitoka Kaliua twende mpaka Mpanda, tukitoka Mpanda twende mpaka Kalema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kupeleka meli mpaka Kalema ni kwasababu tayari ameshaweka meli pale, itaanza kujengwa hivi karibuni na tutapitisha kwenye bajeti hii. Maana yake, meli itakayokuwa inabeba mizigo katika Ziwa Tanganyika yenyewe zaidi ya tani 2,800 itatoka Bandari ya Kalema itakwenda Bandari ya Kalemii upande wa DRC Kongo na huko ndugu zetu wale ambao hawana masoko sasa hivi, watatumia masoko yetu ya dhahabu katika eneo la Kalema na mizigo ya mbao. Kwa hiyo, meli italeta hapo Kalema tutabeba na Standard Gauge Railway na italetwa mpaka Dar es Salaam kwa kwa ajili ya kupeleka ng’ambo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda ifahamike kwamba reli tunayoitumia sasa hivi ni narrow gauge, inaweza kubeba ujazi kama wa tani 1,200 hivi. Pia reli ya TAZARA nayo inabeba kama 1,200 mpaka 1,400 hivi. Kipindi fulani tumezungumza na balozi ya nchi ya kimagharibi sitamtaja hapa, alisema “The East Africa sub-region is too small to support two standard gauge railways,” akimaanisha Afrika Mashariki uchumi wake ni mdogo sana ku-support Standard Gauge Railway mbili kwa maana ile ya Kenya na hii inayojengwa hapa Tanzania. Yule hakuwa na dhamira njema na alikuwa muongo. Kwa sababu sijamtaja nina hakika sijakosea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukiwa na mzigo wa tani 50 Mbeya au Kapirimposhi, Zambia unataka kuuleta Dar es Salaam, itakuchukua zaidi ya miezi sita kuusafirisha na wakati huo utakuwa umeshakosa masoko huko mbele ya safari. Kwa hiyo, kujenga Standard Gauge Railway, ndiyo njia muafaka ya kuchagiza na kuchochea ukuaji wa kiuchumi katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshmiwa Mwenyekiti, napongeza pia kazi kubwa ameifanya alipotembelea daraja la Kigongo, Busisi. Jana Mheshimiwa Kanyasu alisema vizuri sana kwamba wale ambao wamekuwepo pale wanaweza wakaelewa tatizo lililokuwepo sasa hivi la kutumia vivuko vya maji. Wakati mwingine foleni pale ni masaa matatu kuvuka, lakini sasa tunabadilisha maisha ya watu kwa kuvuka kwa dakika nne tu. Hilo ni jambo kubwa sana katika ustawi wa maisha ya watu wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ningependa kusema baada ya pongezi, niendelee kumpongeza pia Mheshimiwa Rais, Mheshmiwa Mama Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Awamu ya Tano. Yapo mambo yaliyofanyika mwaka jana 2020 ambayo ni vizuri tukayafahamu ya kwamba mama yetu ndiye alikuwa ndiye mshauri mkuu wa Rais wa Awamu ya Tano. Mafanikio yale hatuwezi kumtenganisha nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nieleze jambo moja. Mwaka 2020 dunia ilikumbwa na janga la Corona na Tanzania iliamua kutoka na suluhisho lake la ndani la kukabiliana na Corona. Nakumbuka Serikali ilitoa maelekezo kwamba tufanye mambo makubwa matatu; moja, tumwombe Mungu; pili, tuzingatie ushauri wa wataalamu wa afya na Serikali; na tatu, tuendelee kuchapa kazi. Hakufungiwa mtu ndani hapa, wala hatukuweka measures ambazo ni gandamizi na zinarudisha watu wetu nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda ieleweke kwamba Ndugu Bashiru yuko hapa, Katibu Mkuu Mstaafu, mwaka jana, 2020 alitoa maelekezo kwamba humu ndani msitoke, mwendelee kujadili mpaka mpitishe bajeti, hakuna cha Corona; na mlipitisha na wengine tumewakuta kipindi hiki. Hakuna sababu ya kuogopa jambo hili. Mwaka 2020, kwa mbinu tulizozitumia hapa nyumbani, wakiwemo ndugu yangu hapa, alitoka na ile dawa moja inaitwa Bosnia na nyingine nyingi tu; na Covido na akina nani, zimefanya maisha yamekwenda vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusisitiza ni kwamba nchi nyingine zote walitumia mbinu zilizoelekezwa na ndugu zetu wa Magharibi. Nikwambie, wote waliotumia mbinu za Magharibi waliharibikiwa vibaya mno. Hizi taarifa siyo longo longo, ni taarifa za kiutafiti na ziko. Nitatoa mfano ambao ni halisi. Nchi zinazotuzunguka, ninyi mnafahamu, zilitumia mbinu za kimagharibi kukabiliana na ugonjwa wa Corona. Wote wali-experience negative growth mwaka 2020 by end of December. Ni Tanzania peke yake iliyotumia local solutions iliyobaki na uchumi chanya, kwa takwimu za Benki ya Dunia na kwa takwimu zetu za NBS. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali, yako mambo tulifanikiwa sana mwaka 2020, msiyaache, tuyatumie mwaka huu pia kupiga hatua kwa maana hiyo. Bajeti ambayo tunakwenda kuipitisha hapa iliyoletwa na ndugu yetu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa maelekezo ya mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imepokelewa vizuri sana na Umma kwa sababu inakwenda kufanya mkate mdogo kuu-share na watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu, tunapo-share mkate, ni vizuri tukajiwekea utaratibu mzuri wa kusimamia nidhamu ya makusanyo na matumizi. Tusipofanya hivyo, tutaumaliza mkate na tusiweze kuwekeza mkate mwingine na kuifanya dhamira njema ya mama yetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan isifike. Sisi tuko hapa kama askari wake wa mwamvuli kuhakikisha ya kwamba tunafika huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haraka haraka nitoe rai pia kwa Wizara ya Fedha, hawa wanaoitwa micro, small and medium enterprises ulimwenguni ndiyo wana-constitute asilimia 90 ya chumi zote. Hapa Tanzania tuwawezeshe zaidi, ndiyo walipa kodi. Mpaka takwimu za mwaka 2010 ambazo ndiyo tunazo, ziko zaidi ya micro, small and medium enterprises kama milioni tatu na zinamilikiwa na watu 2.7 million.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa hapa walipa kodi ni milioni tano, kama tukiwajengea mazingira mazuri ya kuweza kupata fedha, mitaji na mikopo nafuu; nami nakumbuka kulikuwa kuna maelekezo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, nina uhakika katika majumuisho litawekwa sawa, kwamba ile mifuko yote ambayo inatoa fedha hapa nchini inakaribia 20 haisomani, haitambuani na hairipoti kwa wakati mmoja. Ijumuishwe ili hilo fuko lote la fedha tulisukume kwa wajasiriamali wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali, unajua wakati mwingine wala siyo tunachohitaji ni benki hapa. Hapa tunahitaji fuko moja kubwa la fedha ambalo litaweza kusukuma kazi za wajasiriamali wadogo ama kwa kuwapatia fedha au kwa kuwapatia guarantee kwa maana hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie jambo moja hapa. Sasa tupo katikati ya kipindi kingine tunaambiwa Corona inaendelea. Rai yangu ni kwamba Wizara ya Afya; hapa mimi ningepeleka Wizara ya Afya zaidi na Wizara ya Fedha. Ilani ya uchaguzi imeeleza katika fungu la 84 kwamba lazima tutengeneze kiwanda cha kimkakati cha kuchakata mimea dawa. Hatujatenga fedha vya kutosha. Ilani inasema kuanzisha kituo kikubwa cha utafiti na uchunguzi wa mimea dawa na kuanzisha kiwanda cha kimkakati cha kuzalisha dawa zitokanazo na mimea yetu. Mbona tunatibiwa, tutapona na hizi mimea dawa? Rai yangu, hiki kiwanda msikiweke huku uraiani, mkakifiche sehemu fulani kwenye Kambi ya Jeshi ambako hakuna mtu anaweza kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni vita, wakijua mnatengeneza dawa hapa za kupambana na UVIKO watakuja kutuhujumu, lakini tukikificha sehemu mahsusi, hakuna mtu anaweza kufika, tutatengeneza dawa, tutatengeneza tiba, watu wetu watakaoonekana wamepata tatizo, watapewa dawa hizo na hakuna mtu atakuja kutuzingua hapo baadaye. Ila tusipokuwa makini, umeshasikia wakubwa jana wamesema tupewe chanjo bilioni moja, tuje kudungwa hapa.

Mheshimwia Mwenyekiti, nilikuwa natoa rai, tuwekeze vya kwetu, local solutions, for local problem.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)